Kwa sisi wageni tunaoishi China, linapokuja suala la unywaji wa kahawa, mara nyingi tunajiuliza: Wachina walifanyaje hadi kahawa ikawa kinywaji kinachopendwa katika nchi ambayo kwa maelfu ya miaka inajulikana zaidi kwa chai yake? Hata hivyo, katika miongo miwili iliyopita, mapinduzi ya kahawa yamekuwa wazi. China ya leo, ambayo vijana wake wanaleta mabadiliko ya mitindo ya maisha kwa kasi, kahawa imekuwa kinywaji maarufu, ikibadilika kutoka bidhaa ngeni hadi kuwa desturi ya kila siku kwa wengi.
Katika safari yangu mkoa wa Yunnan, swali langu la muda mrefu lilipata jibu. Baada ya kutembelea chuo kikuu cha kilimo cha Yunnan, na kwenda moja kwa moja kwenye kitivo kinachofanya utafiti na uendelezaji wa kahawa, Naibu Mkuu wa Chuo Profesa Li Hong, alinieleza kwa kina kuhusu kilimo cha kahawa na namna wanavyoboresha kahawa yao.
Profesa Li Hong alisema: “Mkoa huu sio tu unajulikana kwa milima yake mikubwa na utamaduni wake uliosheheni, bali pia ni kitovu cha sekta ya kahawa nchini. Hivi sasa, Yunnan ina mashamba ya kahawa takriban hekta laki moja, ikizalisha tani 170,000 za buni kwa mwaka. Kahawa yake inafurahiwa na wanywaji ndani na nje ya nchi.”
Kahawa ya Yunnan inapandwa katika eneo la milimani kusini-magharibi mwa China, linalojulikana zaidi kwa chai kuliko kahawa. Kwa miaka mingi, kahawa ya China ilikuwa haijulikani sana, huku kahawa za Afrika na Amerika Kusini zikitawala. Lakini siku hizi kahawa ya Yunnan imeanza kufuatiliwa sana kutokana na sifa yake ya kipekee. Kahawa hii inayolimwa katika mwinuko wa juu na kunufaika na hali ya hewa ya kipekee, imekuwa ikizalishwa kwa wingi katika maeneo kama Baoshan, Pu'er, na Lincang, na kuchangia zaidi ya 95% ya uzalishaji wa jumla kitaifa.
Umaarufu wa kahawa ya Yunnan haukuja bure, bali unatokana na juhudi kubwa za serikali, wakulima, wajasiriamali na taasisi za utafiti. Katika miaka ya karibuni, kahawa hii imefanikiwa kubadilika kutoka "malighafi inayouzwa nje" hadi kuwa "chapa maarufu ya Yunnan". Utafiti wa chuo kikuu pamoja na taasisi za utafiti umewezesha kupatikana kwa aina mbalimbali za kahawa zipatazo 22, huku aina zenye ubora kama Geisha na Catimor zikipanuka kwa kasi.
Kuhusu usindikaji, Profesa Li Hong alinifahamisha kuwa kuna maeneo manne ya usindikaji wa kina yaliyoanzishwa: Baoshan, Kunming, Pu'er na Dehong. Maeneo haya yameongeza kwa kiasi kikubwa kiwango cha usindikaji. Ili kujiboresha zaidi, mkoa wa Yunnan umeanzisha chapa zake, na makampuni makubwa ya kahawa kama Starbucks, Luckin, Cotti na mengineyo yanashirikiana na Yunnan, kusaidia kahawa ya Yunnan kuelekea kwenye soko la kimataifa. Kufikia mwaka 2025, kahawa ya Yunnan iliuzwa katika nchi na maeneo 43, na kuwa alama mpya inayowakilisha ladha ya China.
Kinachonivutia zaidi ni kuwa katika zao la kahawa hakuna kinachotupwa. Kuanzia magamba ya buni yanayotengenezwa chai (wanaiita chai ya kahawa), majani ya mbuni yanayotengenezwa chai, hadi mabaki yote yanayotokana na mchakato mzima tangu kuvuna hadi kupatikana kwa kahawa, yote yanatumiwa kutengeneza vitu vingine kama vile pombe ya kahawa, juisi ya kahawa, na kahawa ya maua. Jambo lingine muhimu ni kwamba wanafunzi wa kitivo hicho, mbali na mambo mengine, pia wanapatiwa mafunzo ya utaalamu wa kuandaa na kuhudumia kahawa kitaalamu — wanaitwa “Barista.” Ndio maana mkoa wa Yunnan, hasa mji wa Kunming, umebarikiwa kuwa na mikahawa mingi inayotengeneza kahawa kwa mitindo mbalimbali ya kuvutia na yenye ubora wa juu.
Kuongezeka kwa utamaduni wa kahawa nchini China kunaonesha mwingiliano wa kuvutia kati ya mila na mambo ya usasa. Kadri China inavyokumbatia mwenendo huu, kahawa inakuwa si kinywaji tu bali ni jambo la kitamaduni linalokita mizizi katika maisha ya kisasa ya Wachina. Funzo kubwa nililolipata ni kwamba nchi za Afrika zinahitaji kutumia zaidi teknolojia katika uzalishaji wa kahawa, hasa katika hatua ya kusafisha, kukausha na kusaga buni viwandani. Ubora wa kahawa hautegemei aina tu kama Arabica, Robusta au Liberica, bali pia uchachushaji na usindikaji. Kama Profesa Li Hong alivyosema, kama unataka kujifunza teknolojia hizi zinazofanya buni iwe na ubora wa juu, ni lazima uje China kujua zaidi kuhusu teknolojia zake na soko lake.