Katika taarifa yake kuhusu ajali ya pale Inyala Mkoani Mbeya iliyoua watu kadhaa pamoja na DED wa Igunga, Gazeti la Mwananchi limetoa taarifa kwamba ajali hiyo imetokea ikiwa ni siku tatu zimepita baada ya Makamu wa Rais Dkt. Mpango kutoa maagizo kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuanza ukaguzi wa magari ya mizigo katika eneo hili.
Sasa nashindwa kuelewa busara ya Makamu wetu wa Rais kwamba suluhisho la kuzuia ajali pale Inyala ni kuyakagua magari ya mizigo kabla hayajapita kile kipande cha barabara. Hili nalipinga kwa dhati. Nimeshindwa na hata kuchukizwa na jinsi watu walio na madaraka nchini kama Dkt. Mpango wanavyoyachukulia mambo mazito kirahisi namna hivi.
Hili ni eneo ambalo karibu kila wiki panatokea ajali mbaya sana, na Dkt. Mpango anasema kagueni magari kabla hayajapita hapa. Hii ni busara kweli?
Anapaswa kuelewa nini kinasababisha ajali pale kabla ya kutoa kile tunaita utatuzi wa kisiasa kwa tatizo la kisayansi.
Kwa kumsaidia tu na kumpa ushauri wa bure usio wa kisiasa, ni kwamba kuna sababu kubwa tatu zinazosababisha ajali pale;
- Barabara imeharibika sana na kuweka matuta ya lami kudidimia ambayo mara nyingi yanakulazimu kupita upande usio wako wa barabara au kupoteza control ya gari unapopanda tuta kwa sababu gari zinayumba sana kwenye haya matuta
- Hiyo sehemu ina mlima/mteremko wa umbali mrefu
- Hiyo sehemu ni ya solid line ambayo huwezi ku-overtake gari nyingine (japo madereva wa mabasi hawajali hili)
Sasa Dkt. Mpango anapaswa kutoa wazo la kuzuia ajali pale kwa kuangalia hizo sababu tatu. Na kwa mawazo tu, haya yanapaswa kufikiriwa na Serikali ili kuzuia vifo na ajali za kila wakati eneo hili;
- TANROAD waamrishwe kutengeneza hili eneo haraka sana. Matengenezo yanayotakiwa hapa ni kama yale yaliyofanyika mteremko wa Kitonga katika kuzuia barabara kuweka matuta kutokana na uzito wa malori.
- Kwa kuwa hili ni eneo la mlima/mteremko wa umbali mrefu, pawekwe climbing lane ili kuwepo na njia tatu na ambayo moja itatumiwa zaidi na malori yanayopanda taratibu sana eneo hili
- Zaidi ya kuweka climbing lanes, eneo hili liwekwe "lay-by" kadhaa (yaani michepuko katika barabara iliyo kama sehemu ya kituo cha basi) ili madereva wanaopanda au kuteremka wawe na eneo la kuingia pale wanapoona gari lao linaanza kuleta matatizo na kulifanyia marekebisho, badala ya kusimamisha lori barabarani eneo la hatari.
Mwisho, ninawaomba sana viongozi wetu jaribuni kuwa serious na matatizo yanayowakabili Wananchi, hasa yale yanayosababisha vifo. Msitangulize kukimbia gharama za kutatua matatizo kama haya na kupendekeza majibu ya kisiasa ambayo hayatatusaidia. Kama tatizo ni fedha, tunakatwa sana tozo, tumieni hizo pale Inyala kama suala la emergency.