Jana Mh. Zitto Kabwe akiongea na wanahabari, aliweka wazi takwimu za vifo vinavyosababishwa na Covid 19 kwa sasa nchini mwetu, na kwamba kwa sasa ni vifo 509 kwa wiki, ikimaanisha ni wastani wa vifo 73 kwa siku.
Takwimu hizi zinafahamika kwa watawala, maana chanzo chake ni kwenye mamlaka za Serikali, ikiwemo Wizara ya Afya, lakini wote wamepatwa na kigugumizi kuziweka wazi kwa kuhofia aibu watakayoipata baada ya muda mrefu kutangaza kuwa Covid 19 haipo Tanzania au ipo kidogo sana. Lakini wasichojua ni kuwa mficha maradhi, kilio humwumbua.
Ifahamike kuwa hivi ni vifo vilivyothibitika kwenye hospitali, bado wale wanaofia majumbani na kwenye zahanati. Na hili halishangazi, linaonekana wazi kutokana ja kuwepo taarifa za misiba kila mahali, na kila siku.
Kwa wastani wa vifo 73 kwa siku, Tanzania itakuwa ndiyo inayoongoza kwa vifo vya Covid 19 barani Afrika, na ya tatu Duniani baada ya Mexico (vifo 172) na Thailand yenye (vifo 149) kwa mujibu wa takwimu za leo.
Yaani wakati Dunia ikishuhudia kupungua kwa kiwango kikubwa cha vifo vinavyosababishwa na Covid 19, Tanzania inapaa kwa mwendo wa ajabu kwa vifo vya Covid 19. Haitachukua muda, kwa namna tunavyoenda, Tanzania itaongoza kwa vifo vya Covid 19 Duniani.
Kila mwenye akili achukue tahadhari, mjinga ataangamia na ataangamiza wengine kwa ujinga wake.
Tunawomba Mungu akaweke baraka katika jitihada tunazozifanya kwa dhamira.