Nguvu za Dowans ni kali, zapofua uongozi Tanesco
2009-03-03 11:01:11
Na Muhibu Said
Nguvu za kampuni ya kuzalisha umeme ya Dowans, zimeifumba macho menejimenti ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kiasi cha uongozi huo kuipuuza Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika hilo la umma, Nipashe imeelezwa.
Habari za kiuchunguzi na vyanzo vya habari ndani ya Tanesco vimeithibitishia Nipashe kwamba Menejimenti ya shirika hilo pekee na kongwe la kuzalisha nishati ya umeme nchini, ilitangaza mapendekezo yake ya kutaka kununua mitambo ya kufua umeme wa dharura ya Dowans huku ikijua fika Bodi ilikuwa imetoa maelekezo kadhaa ya kuzingatiwa kabla ya tangazo hilo.
Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya Tanesco kinaeleza kuwa miezi minne iliyopita bodi ilitoa maagizo matatu muhimu kwa menejimenti ya Tanesco, lakini hadi mwezi uliopita uongozi huo uliposema bado unafukuzia mitambo ya Dowans, ulikuwa haujatekeleza hata agizo moja.
Hatua hiyo ya menejimenti ya Tanesco ambayo imeibua mjadala mkali miongoni mwa Watanzania na kuwagawa wabunge makundi mawili kupitia Kamati za Bunge, inaelezwa kuwa imeishtua Bodi hiyo.
Kikao cha Bodi kilichofanyika Desemba 12, mwaka jana, kilihitimishwa kwa kwa kuiagiza menejimenti ya Tanesco kuteua wajumbe wawili kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa ajili ya safari ya kwenda Houston, nchini Marekani kuangalia bei ya mitambo kama ile inayomilikiwa na Dowans.
Ilielezwa kuwa agizo hilo lilitolewa kutokana na taarifa ambazo Bodi inazo, kwamba mitambo kama ile inayomilikiwa na Dowans, inauzwa kwa Dola za Marekani milioni 14 wakati mitambo ya kampuni hiyo, ambayo ni michakavu Tanesco wanataka kuinunua kwa Dola milioni 30, yaani zaidi ya mara mbili ya bei halisi.
``Hata hivyo, menejimenti ya Tanesco haikutekeleza agizo hilo,`` kilieleza chanzo chetu ndani ya Tanesco.
Mbali na agizo hilo, Bodi pia iliitaka menejimenti ya Tanesco kukumbuka ushauri uliotolewa kwake na wanasheria wa shirika hilo kwamba kampuni ya Richmond ni hewa na mkataba na mitambo ya Dowans imetokana na kampuni hiyo, hivyo chochote kinachotokana na Dowans pia kitakuwa na utata.
Chanzo hicho kimesema kwamba Bodi waliiagiza menejimenti ya Tanesco iwasiliane na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupata uhalali wa mitambo ya Dowans, ambayo imeirithi kutoka Richmond, pia waombe marekebisho ya sheria ya manunuzi.
``Lakini menejimenti ya Tanesco hawakufanya hivyo, badala yake wakaamua kutoa tangazo kwenye vyombo vya habari kutaka Bodi iidhinishe ununuzi wa hiyo mitambo ya Dowans. Bodi imeshtuka sana,`` kilieleza chanzo hicho.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Adola Mapunda, alipoulizwa na Nipashe jana, alisema hawezi kuzungumza lolote kwa vile suala hilo liko mahakamani.
Kutokana na kauli ya Mapunda, hata uongozi wa Tanesco haukupaswa kuzungumzia wala kutangaza mipango ya kununua Dowans hadi kesi dhidi ya shirika hilo imalizike.
Wakati hayo yakijiri, habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana zinaeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa leo kukutana na viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, ikiwamo menejimenti ya Tanesco na huenda hoja kuhusu Dowans ikawemo katika orodha ya mambo yatakayojadiliwa katika kikao hicho.
Jumamosi wiki iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Idris Rashid, alitoa taarifa kwenye vyombo vya habari kueleza hali ya umeme katika Gridi ya Taifa pamoja na mambo mengine, akapendekeza kuwa mtambo wote wa Dowans ununuliwe na serikali pamoja na vifaa vyote vya kuunganishia kwenye gridi.
Hata hivyo, wakati Tanesco ikitoa taarifa hiyo, Mbunge wa Kyela Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, alikaririwa na Nipashe akisema kuwa ni vigumu kununua mitambo ya Dowans kwa sababu licha ya kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma na maazimio ya Bunge, kampuni hiyo imefungua kesi dhidi ya serikali na Tanesco katika mahakama ya usuluhishi huko Paris, Ufaransa.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Mwakyembe alisema anashangazwa na hatua ya Tanesco kung`ang`ania mitambo ya Dowans, wakati tayari wamiliki wake wamewashtaki serikali na Tanesco huko Ufaransa.
Wakati Dk. Mwakyembe na kamati yake wakipinga vikali suala hilo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, wiki iliyopita alikaririwa na vyombo vya habari akibadilisha msimamo wa awali wa serikali wa kutonunua mitambo ya Dowans kwa kusema kwamba, uamuzi huo si ufisadi.
SOURCE: Nipashe