Ninyi wa Serengeti hata msilalamike! Mnajiponza wenyewe na mapenzi yenu kwa CCM! Mnavuna mnachopanda!
ccm ni sehemu tu ya matatizo mengi yanayochangia kurudisha nyuma maendeleo ya wilaya yetu ya Serengeti.
SAGANKA nakushukuru kwa kuleta hoja hii, najaribu kukusoma jinsi ulivyokereka kutokana na lugha uliyotumia lakini ujumbe wako umefika, na ndugu yangu
Mwitongo nimekusoma hoja zako ni za kweli kabisa.
Mimi nimezaliwa na kukulia Kijiji cha Kibeyo, kata ya Kisangura wilayani Serengeti, kwahiyo ninaifahamu vizuri sana wilaya yetu ambayo nimefanikiwa kufika/kuitembelea karibu kona zote; kuanzia Machochwe, Mbirikili, Bonchugu, Rwamchanga, Miseke,Robanda, Bwitengi, Natta, Issenye, Ring'wani, Masinki, Kisaka, Kenyamonta, Majimoto, Iramba, Mara Somoche, Kebanchebanche, Merenga, Nyansurura, Mbalibali na kwingineko kwa kutaja vijiji vichache.
Cha kwanza kabisa kilichoturudisha nyuma, kwa upande wetu wilaya ya Serengeti ni mapigano ya koo. Kulikuwa na mapigano baina ya wangoreme na wanyabasi + watimbaru tangu miaka ya sabini huko ambayo yaliua watu wengti sana, hadi miaka ya hivi karibuni mapigano yamepungua sana lakini chuki na uhasama baodo upo. Tumeshuhudia mapigano mabaya sana miaka ya 80s baina ya wanyabasi + watimbaru dhidi ya wakira + walenchoka, tumeshuhudia mapigano baina ya wanyabasi + watimbaru dhidi ya waikoma + wanata + waisenye. Kama hiyo haitoshi, kulikuwa na uhasama mkubwa sana baina ya wakurya na wamaasai toka mkoa wa Arusha ambao walikuwa wakiiba ng'ombe kwa wingi sana toka wilayani kwetu hadi mwishoni mwa miaka ya tisini ndipo hali hiyo imekaoma kabisa baada ya kufanyika jitihada kubwa na mazungumzo baina ya wamaasai na wakurya.
Kama nilivyodokeza hapo awali sasahivi mapigano baina ya koo hizi yamepungua sana kama si kuisha lakini bado kuna chuki miongoni mwao na watu hawa hawaaminiani sana. Kipindi chote cha mapigano kwa ujumla koo zote zilishindwa kuweka mazingira mazuri ya elimu na afya. Hawakuweza kuwekeza vya kutosha katika elimu, hawakusomesha watoto wao bali walijikita katika kuwafundisha ujasiri wa kupambana na kulinda koo zao. Na ikumbukwe kwamba katika mapigano yote yaliyokuwa yakitokea baina ya koo kama nilivyotaja hapo awali, wizi wa mifugo hasa ngo'mbe, mbuzi na kondoo walikuwa wakiibiwa/kutaifishwa kwa wingi sana toka upande ulioshindwa vita, na kwakuwa koo zote za wilayani serengeti kwa sehemu kubwa ni wafugaji kwahiyo wakajikuta wakiishia kuwa fukara.
Jambo jengine ambalo lilisababisha kuendelea kuwepo kwa mapigano baina ya koo zetu ni viongozi wa kisiasa na vyombo vya dola, ambao walinufaika sana na hizi vurugu kwakuwa walitumia mwanya huo kupora mifugo ya wananchi kwa kisingizio cha kukabiliana na wizi na hatimaye kujigawia wao wenyewe. Viongozi wakubwa walionufaika sana na uporaji huo walikuwa ni wakuu wa wilaya-hapa namkumbuka marehemu Makunenge na mwingine mmoja akiitwa Zuberi ama Omary aliyefariki ghafla akiwa amelala, makamanda wa polisi wilaya(OCDs), wenyeviti wa baraza la madiwani-hapa namkumbuka mwenyekiti mmoja wa baraza la madiwani mwishoni mwa miaka ya 80 hadi mwanzoni mwa miaka ya 90 aliyekuwa akitokea ngoreme akiitwa Luge(nadhani alikuwa mwanajeshi mstaafu) alifaidika sana na ng'ombe wa koo za kikurya (wanyabasi, watimbaru na wakira).
Kwahiyo hiyo utaona ni kwa kiasi gani wananchi walikosa kabisa muda wa kufanya kazi za kujiletea maendeleo. Katika hali kama hiyo hata walewachache waliokuwa wamefanikiwa kusoma na kutaka kuwekeza nyumbani walishindwa kwakuwa hali ya usalama ilikuwa ni ndogo sana. Nakumbuka majengo mengi sana yaliyokuwa yameanza kujengwa mjini mugumu miaka ile ya themanini yote yaliishia kuporomoka kufuatia vita mbaya sana baina ya wanyabasi + watimbaru dhidi ya wakira + walenchoka, hii ilitokana na ukweli kwamba watu wengi waliokuwa na uwezo na kuanza kufanya ujenzi mjini mugumu walikuwa ni wanyabasi na wakira, sasa katika mazingira yale ya vita hakuna mtu aliyekuwa na uwezo wa kufanya ujenzi.
Ni miaka ya tisini ndipo sasa mji wa mugumu ulianza kujengwa kwa kasi sana baada ya kumalizika kwa uhasama mkubwa baina ya koo hizi na watu kujielekeza katika shughuli za maendeleo. Ndipo watu wakapata mwamko wa kuanza kuwekeza katika elimu, shule ya sekondari ya Serengeti ambayo wananchi wote wa wilaya walikuwa wameichangia tangu miaka ya sabini ndipo ikapata kufunguliwa na kuanza kupokea wanafunzi. Ikumbukwe kwamba kabla ya hapo wilaya yetu ilikuwa na shule moja tu ya sekondari ambayo ni ngoreme secondary.
Jambo jingine lililopelekea wilaya yetu kuwa nyuma sana kimaendeleo ni jamaa zetu waliofanikiwa kimaisha hasa waliosoma kwakuwa miaka ile wasomi ndio walikuwa na uwezo mzuri wa kufanya uwekezaji, wakaamua kususia nyumbani kwao, wakaamua kuwekeza huko wanakofanya kazi na kusahau kwamba nyumbani nako kunawahitaji. Na kwakuwa hawakuwekeza nyumbani kwao japo kujenga nyumba nzuri tu za kuishi, hata wanapostafu utumishi wao wanalazimika kuendelea kuishi huko huko mijini walikojenga majumba mazuri na kufanya uwekezaji kadhaa. Labda sasahivi ndio watu wanajitahidi kukumbuka kwao, nimeona wasomi wa siku hizi japo si wengi wanapofanikiwa wanakumbuka kurudi nyumbani na kujenga ingawa si kwakiwango kikubwa, na hivyo inabidi tuendelee kuhamasishana ili kila mmoja aone wajibu wake wa kukumbuka kwao.
Kwa sasa niishie hapa, nikipata muda nitachangia sababu nyingine nyingi zilizosababisha kurudi au kuwa nyuma kimaendeleo kwa wilaya yetu ya Serengeti.