Hivi majuzi tu Chama cha Kikomunisti cha China CPC kimesherehekea kutimiza miaka 100 tangu kiasisiwe mwaka 1949. Ambapo kililazimika kusubiri kwa miaka 28 hadi kuingia madarakani na toka hapo kimeongoza watu bilioni 1.4.Katika miaka 100, chama na nchi imepitia vita vya wenyewe kwa wenyewe, mapinduzi ya kiutamaduni, mageuzi na ufunguaji mlango, China kurejeshewa Hong Kong na Macau na kumalizika kwa vita baridi.
Ukitembelea vijiji na miji mikubwa ya China kama vile Shanghai, utapata kuona nchini imefikia wapi. Licha ya zama za ustaarabu wa China, nchi inaonekana kuwa kitendawili kwa nchi za Magharibi na hata kwetu sisi pia. Kweli tunaweza kutegua kitendawili cha China?
Kama umesikiliza hotuba za viongozi wa China, basi kila mara utasikia wakitaja alama kubwa za siku za nyuma kama vile Ukuta Mkuu wa China. Nchi inapata msukumo wake kutokana na vitu vya nyuma.
Kama China imeweza kujilinda na wavamizi kwa kujenga ukuta wenye urefu wa kilomita 700, kweli itashindwa kuchukua hatua kama hiyo hivi leo, yaani kusimama kidete dhidi ya nchi za Magharibi?
Kwa miaka mingi China imekuwa na shida kadha wa kadha, kama vile vita vya kasumba na uvamizi wa Japan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Inawezekana kuwa sasa imeazimia kuhakikisha kwamba matukio kama hayo hayarejei tena. Uhusiano wa China na matukio ya nyuma unaokena kwenye ujenzi wa makumbusho. Kwa kupata msukumo wa nyuma, China inakabili siku za mbele kwa kujiamini.
Ingawa wasomi wa Magharibi na wachambuzi wa sera wanaishutumu China kwa kuchagua vitu vizuri tu ambavyo vilisisitizwa zamani, lakini hawana tofauti na watu wengine. Kwa mfano sisi Wakenya tunasisitiza ukoloni lakini tunasahau ustaarabu mkubwa uliokuwepo kabla ya hapo. Kila jamii ya Wakenya ilikuwa na mfumo wake wa kisiasa na sheria ambao uliendelea kwa karne kadhaa. Lakini mfumo huo umeondolewa na ukoloni. Kwanini tusichanganye na utamaduni wetu?
China imefanya hivyo, imechanganya tamaduni zake na mambo ya kisasa. Wachina wanaongea Kichina cha Mandarini, Wachina wanaohamia nchi za Magaharibi mara nyingi wanachagua majina ya Kiingereza ili kutoa urahisi. Lakini hayo hayakuizuia China kurusha chombo cha anga ya juu na kutua kwenye mwezi. China sasa ni kiongozi wa akili bandia AI na sayansi za aina nyingine, hadi Wamarekani wameanzisha sheria maalumu ya kupambana na ukuaji wa kushangaza wa China.
Ukuaji wa China pia upo kwenye msingi wa kutumia sayansi na teknolojia. Hata viongozi nao pia wamo. Angalia historia ya marais wengi wa China akiwemo wa hivi sasa, wengi wao ni wahandisi au wanasayansi. Rais Xi Jinping amesomea uhandisi wa kemikali katika chuo kikuu cha Tsinghua. Wanafunzi wa China hawaendi nchi za magharibi kusomea elimu ya binadamu (anthropolojia) au sayansi ya siasa. Bali wanasomea sayansi, teknolojia, uhandisi, na hesabati (STEM) na kurejea nyumbani.
Wachina wanaonekana kujua kwamba masomo haya ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabati lazima yatakuwa na mhimili wa falsafa au itikadi.
Itikadi za magharibi zinasisitiza uhuru wa mtu binafsi, ambao umetekelezwa tangu kipindi cha kuchipuka upya. Lakini China ilifuata upande tofauti, kudhibiti maisha ya mtu binafsi ikiwa ni pamoja na idadi ya watoto wanaozaliwa. Hivi sasa imelegeza sheria hiyo ili kupata nguvu kazi za kukuza uchumi katika siku za mbele.
China inataka kuepuka mtego wa nchi za Magharibi wa kupunguza idadi ya watu, ambao imevuta wahamiaji. Kinachoifanya China iwe ni kitendawili ni kwamba wakati uchumi wake unapokuwa, tulitegemea na demokrasia itakua pia. Hilo halijatokea. China inaonekana kujua “hatari ya kuharakisha demokrasia” Mimi naona siku moja China itakuwa nchi ya kidemokrasia lakini sio katika wakati ambao tunautarajia.
Hatimaye, China inaonekana kwamba karibuni tu itakuwa nchi yenye nguvu kubwa duniani ikisaidiwa na mafanikio yake katika kugeuza wimbi la COVID-19. Lakini itafanya kwa kasi yake yenyewe, ambayo inaweza kufadhaisha juhudi za nchi za Magharibi na kupelekea kuipunguza kasi. Kwa nchi nyingine hasa za Afrika zinaweza kuiangalia China inavyoinuka na kujifunza kutoka kwake.