Leo Salehe Amemaliza kabisa, angalia hii hapa chini;
NAONA AIBU KUKUMBUKA, NAOGOPA HATA KUOTA MAMBO YA TANGA-COASTAL VS YANGA
Na Saleh Ally
HAKUNA kitu Watanzania wengi hawakipendi kama ukweli. Ukikisimamia, basi wewe ndiye adui namna moja wa wengi, lakini mimi naendelea tu na leo nipo Tanga.
Kwanza nianze kulaani kitendo cha mashabiki waliokua kwenye Uwanja wa Mkwakwani wakati Coastal Union ikipambana na Yanga katika nusu fainali ya Kombe la FA kumpiga mwamuzi msaidizi hadi akazimia.
Hakika ameumizwa na mara nyingi nimekuwa nikilalama kuhusiana na vurugu za uwanja huo, hadi imefikia sipendi hata kuangalia mpira hapo.
Ingawa safari hii, unaweza ukasema ni kama nyuki waliochokozwa, si kama siku nyingine. Mwamuzi msaidizi aliyekuwa ameshika kibendera upande wa mashariki ya uwanja. Alifanya mambo mawili makubwa na mabaya katika mpira wa nchi hii.
Hakuna anayeweza kukataa hata kidogo kama Coastal Union waliutawala hasa mchezo huo. Walikuwa bora mara mbili ya Yanga, wachezaji vijana na wazalendo walikuwa bora mara tatu zaidi ya wakongwe na wageni wanaolipwa mamilioni ya fedha ukilinganisha na wao.
Coastal Union wenyewe wanapaswa kujilaumu kushindwa “kuua” mchezo mapema kabisa. Walikuwa na uwezo wa kwenda mapumziko na bao tatu na Yanga, walikubali kabisa. Lakini hawakuwa makini na mambo yakawa magumu kabisa.

Bao la Coastal Union lililofungwa na Yossouf Sabo raia wa Cameroon lilikuwa bora na bomba kweli. Lakini mabao yote mawili ya Yanga yalijaa utata na lile la pili linaonyesha ni uonevu wa dhati, dhahiri shahiri kwamba mwamuzi huyo alipanga kuona Yanga inashinda. Huu ni upuuzi wa hali ya juu ambao tunataka tukae kimya na kuuachia upite kwa kuwa kila mmoja anahofia kulaumiwa na mashabiki wa Yanga kama atasema ukweli.
Yanga ilikuwa na mabao 2-1 hadi mwamuzi anavunja mchezo baada ya vurugu. Lakini uhalisia unaonyesha “hapana”. Bao la kwanza alilofunga Donald Ngoma, lina utata mkubwa wa kuotea, Ngoma anafunga lakini hata yeye anaonyesha hajiamini kama anapaswa kushangilia au la.
Bao la pili la Tambwe, dhahiri anausukuma mpira kwa mkono kila mmoja akiona wazi. Lakini mwamuzi anaamua kusema bao. Hakika hii ni aibu na Wanayanga wanaochukia watu kusema ukweli watakuwa ni wanaojidanganya kwa kuwa bingwa wa michuano hiyo atashiriki michuano ya kimataifa ambako hakuwezi kuwa na waamuzi wazembe kama hao wa mechi kati ya Yanga dhidi ya Coastal Union.

Mwisho wa hili. Adhabu inaweza kuangukia kwa Coastal Union na Yanga ikasonga ikionekana haina hatia. Lakini macho yetu yanapeleka ujumbe ndani ya mioyo yetu kwamba Coastal Union wameonewa au wamedhulumiwa.
Dhuluma hiyo unaweza kuikataa kinafiki, lakini kama ni muungwana. Kamwe hauwezi kuwaza hilo, badala yake utakasirishwa kabisa hata kama utakuwa Yanga wa kulialia.
Lazima kuwe na “fea” game. Kama Coastal waliitoa Simba, mwamuzi akatoa penalti dakika ya mwisho kwa kuwa yalikuwa ni maamuzi sahihi, hicho ndicho kinachotakiwa kwa kuwa tunahitaji bingwa halali.
Angalia mechi ya Mwadui FC dhidi ya Azam FC ilivyokuwa tamu. Angalia ushindani wa juu na mshindi mwisho kapatikana kwa mikwaju ya penalti.

Mechi ya Tanga; gumzo lake sasa ni uamuzi mbovu. Hakika hili ni jambo baya katika soka nchini kwetu na haitakuwa ni kuisaidia Yanga, pia uzembe wa mwamuzi huyo hauwezi kuwa na faida katika mchezo wa soka na TFF wanapaswa kuchukua hatua kali pamoja na maumivu ya kipigo alichopata, lakini apumzishwe kabisa.
Sitaki hata kukumbuka kilichotokea, naona aibu. Jana usiku, nimejitahidi nikilala nisiote ndoto ya mechi hiyo, naogopa!
