KWANINI NELSON MANDELA HAKUMSAMEHE MKEWE WINNIE MPAKA ANAKUFA??
Nilipata nafasi ya kufuatilia matangazo ya moja kwa moja ya kuagwa kwa mwili wa Winnie Mandela kutoka kwenye uwanja wa Orlando(SOWETO)mahali ambapo ilikuwa chimbuko la harakati za kupinga ubaguzi wa rangi Afrika Kusini(Apartheid Regime).
Serikali ya Afrka Kusini ilichagua eneo la SOWETO(Southern Western Townships) sababu ndipo hasa Waafrika wengi waliothirika na ubaguzi wa rangi wanaishi.Hapa ndioo ilikuwa kitovu cha vuguvugu na harakati zote za kupambana na ubaguzi wa watu wachache (makaburu).Wale tuliowaimba kwenye nyimbo za mchakamchaka miaka hiyo tukiwa shule,ili waiachie Afrika Kusini na kuleta utawala wa watu wengi.
Wameichagua SOWETO, sababu licha ya umaarufu wake na nafasi yake kama eneo la harakati za makabwela weusi, lakini ndiyo eneo ambalo mtalaka wa Nelson Mandela, Winnie Mandela aliendelea kuishi na kuweka makazi ya kudumu, akiwa amejenga nyumba yake katikati ya eneo la watu duni na masikini, katika eneo ambalo waliishi na Mandela enzi za ujana wao kabla hajafungwa gerezani. Wapo wanaosema Winnie aliamua kujenga na kuishi Soweto ili kuendelea kupata nafasi ya kuungwa mkono na watu weusi ambao wengine walianza kumtenga baada ya yeye kuachwa na Nelson Mandela.
SOWETO ni eneo lenye historia yenye jasho na damu ya mahangaiko ya mtu mweusi katika kulinda utu wake, eneo lililoundwa na makaburu maalumu kwa ajili ya watu weusi ili wasichangamane na watu weupe, weusi waliokuwa wengi waliobaguliwa na weupe wachache.Eneo hili liliundwa na vitongoji vitatu vya Moroka, Jubavu na Orlando(mahali ambapo Winnie anapewa heshima zake za mwisho)
SOWETO ndio eneo lilolozaa wazo la kuwa na siku ya mtoto wa Afrika, maana June 16 1976, tunapokumbuka siku ya Mtoto wa Afrika, basi tunakumbuka askari wa kikaburu waliowauwa mamia ya watoto weusi walioandamana kudai usawa wa elimu, watoto wa shule wa jamii ya watu weusi kwa mamia waliuwawa kwa risasi za moto.Hii ndio siku ambayo vitabu vya historia viliita "Soweto Massacre".Maana yalikuwa ni mauwaji ya mamia ya watoto wasio na hatia.
Imekuwa ni nafasi nzuri kwetu kwa Mungu kutupa nafasi nyingine ya kushuhudia mwisho wa maisha ya wapigania ukombozi wa Afrika Kusini.Wale ambao tuliwasoma na kuhadithiwa mashuleni, sasa tunapata nafasi ya kuona miisho yao.Winnie ni mmoja kati ya magwiji wa harakati za ukombozi wa mtu mweusi wa Afrika ya Kusini. Maisha yake yamefikia tamati.
Mwanamke jasiri, mpiganaji, Mama na mwanaharakati ambaye historia na harakati zake juu ya utu wa mtu mweusi inafunikwa na mzozo wake wa mahusiano ya ndoa na mumewe Nelson Mandela na hatimaye talaka iliyoshuhudiwa mbele ya vyombo vya habari. Maisha ya ndoa na mfarakano wa Winnie na Mandela, ina nafasi kubwa ya kutufunza sisi tuliobaki.
Inasemwa Nelson kabla ya kuwa na Winnie, alikuwa na mke wa kwanza aliyeitwa Evelyn, huyu alikuwa mcha Mungu na mkristo mwenye msimamo, hakupenda kuona Mandela anajihusisha na harakati za kumkomboa mtu mweusi, alitamani wakae na kulea watoto. Mandela hakuwa tayari, alitaka kuendelea na harakati zake dhidi ya ubaguzi wa rangi na manyanyaso ya mtu mweusi. Hivyo alipewa chaguo, ni ama aikumbatie siasa au mapenzi kwa familia na mkewe Evelyn,Mandela alichagua moja, siasa na harakati za kupigania utu wa mtu mweusi.
Msimamo huu wa mkewe wa kwanza, ulimfanya Mandela awe ktk mchakato wa kutafuta mke mwingine. Mandela na Winnie walikutana kwenye kituo cha basi, wakati huo Winnie akiwa na miaka 22, akiwa kama Afisa Ustawi wa Jamii (Social Worker). Nelson alimualika kwa chakula cha usiku, na walipokutana,basi mahusiano yao yakaanzia hapo.
Nimepitia Gazeti la [HASHTAG]#Mwananchi[/HASHTAG] on line,na baadae mtandao maarufu wa kijamii(Social Forum) wa Afrika Kusini unaoitwa "My Broadband" vyote vimejaribu kukumbushia simulizi ya "KWANINI NELSON MANDELA HAKUMSAMEHE MKEWE WINNIE?".
Vyanzo vyote hivyo vya habari, kwa maana ya gazeti na mtandao, vimenukuu na kutafsiri kwa kiasi kikubwa maandishi ya Mwandishi maarufu ajulikanaye kama John Carlin kwenye kitabu chake cha "KNOWING NELSON MANDELA".
John Carlin ni mmoja wa waandishi wachache waliopata bahati ya kufanya mahojiano ya muda mrefu ya uso kwa uso na Nelson Mandela na baadae mtalaka wake Winnie, na akatoka na kitabu chenye simulizi tamu ya kwanini Mandela licha ya ujasiri wake wa kuvumilia mateso ya jela kwa miaka 27, kuwasamehe waliomfunga na kumtesa na hatimaye kuunda tume ya maridhiano kati ya mtu mweusi na mweupe Afrika Kusini, lakini alishindwa kumsamehe mkewe Winnie.
John Carlin katika kitabu chake cha "KNOWING NELSON MANDELA" anatusimulia kuwa, baada ya miaka miwili ya Winnie na Mandela kukutana, Mandela alikamatwa na kufungwa gerezani kifungo cha maisha akamuacha Winnie huku nyuma akitaabika na watoto wao wawili. Katikati ya manyanyaso na ukatili wa serikali ya kibaguzi, Winnie mara kadhaa alikamatwa na kuwekwa kuzuizini au hata kufungwa na serikali ya makaburu.
Muda wote huu,Winnie alikuwa peke yake, mpweke na mwenye kunyanyasika na makaburu. Hata alipopata nafasi ya kwenda gerezani kule kisiwani kumsalimia Mandela kila aliporuhusiwa, maongezi yao yalitengenishwa na ukuta mkubwa wa kioo. Waliishia kuonana kupitia kioo. Hivyo wakaishia kusalimiana na kupeana moyo,huku Winnie akiwa anaendeleza mapambano kutokea SOWETO.
Wanaharakati wengine kama kina Thabo Mbeki, Walter Sisulu na Jacob Zuma walikimbia nchi na kuishi uhamishoni wakitumia hati bandia za kusafiria kutoka sehemu moja kwenda nyingine, Winnie aliendelea kubaki SOWETO akipambana na makaburu uso kwa uso
Baada ya Mandela kutoka gerezani,Winnie alianza kuandamwa na "skendo" nyingi zilizomuumiza Mzee Mandela. Moja ya skendo kubwa ilikuwa ni mauwaji ya kijana mdogo wa miaka 14, aliyefahamika kwa jina la Stomple Moeketsi, ambaye walinzi wa Winnie walimuua wakisadikishwa kuwa alikuwa "kibaraka" anayepeleka siri za harakati zao kwa makabaru. Jambo ambalo baadae ilithibitika kuwa si kweli na huku tayari kijana yule alikuwa ameuwawa kwa msaada wa Winnie.Jambo hili lilimuumiza sana Mandela.
Skendo iliyokuja kumtibua Mzee Mandela, ni ile ya kugundulika kuwa Winnie alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na kijana mdogo ambaye alimzidi zaidi ya miaka 30, huyu alikuwa mwanasheria na mtetezi wa kesi za Winnie Mandela, aliitwa Dali Mpofu. Dali Mpofu alikuwa anashirikiana na Julius Malema kumtetea Winnie katika kesi zake.
Mahusiano yao yanatajwa kuwa yalianza wakati hata Mandela hajatoka gerezani,lakini makomredi wa ANC waliogundua mahusiano ya wawili hawa, walifanya siri sana ili kutunza heshima ya Mzee Mandela na Winnie.Julius Malema mara kadhaa alijitahidi kutetea na kusema Mpofu hawezi kutembea na Winnie ambaye ni kama Mama yake.
Lakini wakati Malema akikanusha,wapambe wa Mzee Mandela walishakuwa wamempenyezea siri zote za Winnie na wanaume aliokuwa nao wakati Mzee akiwa gerezani. Hivyo katika kifua chake, Mandela alikuwa na dukuduku la "kusalitiwa" na Winnie hadi kwa vijana wadogo wa umri wa watoto wa kuwazaa.
Mandela mwenyewe katika kitabu cha "KNOWING NELSON MANDELA" anasema, wakati akiwa gerezani, hakutarajia wala kumlazimisha Winnie awe mseja, lakini alimtaka awe msiri na kufanya mambo kwa staha. Kitu ambacho Winnie hakukitimiza.
Mandela alisisitiza kuwa ndoa yao imeharibika kiasi kwamba haiwezi kukarabatiwa, tangu alipotoka gerezani hakuna hata siku moja ambayo Winnie aliingia chumba cha kulala huku Mandela akiwa macho. Mandela ansema na mara zote chumbani ndipo mipango hupangwa kabla ya kulala, lakini mambo mengi aliyotaka kujadili na kupanga na Winnie yanayowahusu yalishindikana,maana Winnie hakuweza hata kumtazama usoni.
Moyo ulimuuma zaidi Mzee Mandela baada ya kupenyezewa barua ya kimapenzi iliyoandikwa na Winnie kwenda kwa mpenzi wake Dali Mpofu. Barua ile ilidakwa na wapambe wa Mzee Mandela wakamfikishia na kuivujisha kwenye vyombo vya habari.
Katika barua ile,Winnie analalamika kukosa penzi la Dali Mpofu kwa muda mrefu, Winnie aliandika kwa malalamiko anasema;
"Before I am through with you, you are going to learn a bit of honesty and sincerity and know what betrayal of one’s love means to a woman … Remember always how much you have hurt and humiliated me … I keep telling you the situation is deteriorating at home, you are not bothered because you are satisfying yourself every night with a woman. I won’t be your bloody fool, Dali.”
Kwa Tafsiri isiyo ya moja kwa mojaWinnie anaandika anasema
"Kumbuka ni namna gani kila mara uliniumiza na kunidhalilisha.Naendelea kukueleza kwamba hali ya uhusiano inazidi kuzorota nyumbani, wewe hujali kwa sababu umeridhika mwenyewe na huyo mwanamke, Siwezi kuwa mpuuzi Dali"
Barua hii na maandishi haya yalimuumiza sana Mzee Mandela,lakini bado washauri walimsihi kuwa avumilie maana yeye na Winnie ni mfano wa harakati za utu wa mtu mweusi katika jamii ya watu weusi na Afrika kwa ujumla. Apige moyo konde,lakini majaribu yakawa mengi na kumfika kooni.
Mara nyingine Winnie alikuwa na safari ya kwenda Marekani,akaondoka bila Mzee Mandela lakini akataka kuondoka na Mpofu kama msaidizi wake, na kwa kujua mahusiano yale ya Winnie na Mpofu, Mandela akamuonya Winnie asiandamane na Mpofu kwenda Marekani.
Winnie akakubali kutokusafiri naye.Usiku mmoja akiwa Marekani, Mzee Mandela alimpigia simu Winnie, bila kujua, Dali Mpofu alipokea ile simu,na aliyepiga akasikika akisema "Tata Madiba", Mpofu alipojua anaongea na Mandela akakata simu. Mzee Mandela akawa tayari amejua kuwa usiku ule, Winnie alikuwa na usiku wa pamoja na Dali Mpofu Marekani,na lile katazo la kusafiri na Mpofu,Mama Winnie Mandela alilipuuza.
Machi 1996, Nelson Mandela akaamua kumuacha Winnie. Aliita vyombo vya habari na kusoma kusudio lake akiwa na huzuni kubwa sana. John Carlie anamnukuu mzee Mandela akisema:
“During the two decades I spent on Robben Island she was an indispensable pillar of support and comfort… My love for her remains undiminished.We have mutually agreed that a separation would be the best for each of us… I part from my wife with no recriminations. I embrace her with all the love and affection I have nursed for her inside and outside prison from the moment I first met her.He rose to his feet. “Ladies and gentlemen. I hope you ‘ll appreciate the pain I have gone through and I now end this interview.”
Kwa tafsiri isiyo ya moja kwa moja Mandela anasema ;
"Katika kipindi cha miongo miwili nilichokuwa ktk gereza la Robben Island, Winnie alikuwa nguzo imara ya msaada na faraja. Mapenzi yangu kwake yatabaki bila kupungua.
Tumekubaliana kwamba uamuzi bora kwetu ni kutengana.
Ninaachana na mke wangu bila lawama. Namkumbatia kwa huba na mapenzi kama nilivyokuwa najisikia nilipokuwa ndani na nje ya jela tangu nilipokutana naye.
Mabibi na mabwana, mtakubaliana nami kwa maumivu niliyokuwa nayo na huu ndio mwisho mahojiano yangu na ninyi"...Mzee Mandela akasimama kwa huzuni na kuondoka.
Hapa ndio ukawa mwisho wa mahusino ya Mzee Mandela na Winnie mkewe wa zaidi ya miaka 27 akiwa gerezani na nje ya gereza.
Hata katika wosia wa urithi wa mali na pesa aliouandika Mandela wakati akiwa hai, hakuna mahali ambapo amemtaja Winnie kama sehemu ya watu wataopata urithi wa mali zake. Amekuja kuandika Graca Machel ambaye wameona baada ya kumtaliki Winnie.
Watatezi wa mfumo jike(Feminist) wanamtetea Winnie nakuona kama hakutendewa haki. Miaka 27 ya kuisi mbali na mumewe isingeweza kumuacha salama,wanaamini Winnie hakustahili kile alichofanyiwa na Mzee Mandela.
John Curlie anamnukuu Winnie akisema:
“I have never lived with Mandela,” she said. “I have never known what it was to have a close family where you sat around the table with husband and children. I have no such dear memories. When I gave birth to my children he was never there, even though he was not in jail at the time.”
Kwa tafsiri isiyo rasmi Winnie anasema "Sijawahi kuishi na Mandela. Sikuwahi kujua kile kinachoitwa kuwa karibu na familia ambapo unakaa kwenye meza moja wewe, mume na watoto. Sina kumbukumbu nzuri kama hizo. Nilipojifungua watoto wangu wawili (Mandela) hakuwepo,japokuwa kwa wakati ule hakuwa jela"
Kauli hii ya Winnie inaonyesha kuwa hata Mandela naye alikuwa bize sana na harakati za kumkomboa mtu mweusi, kiasi hata wakati akiwa hajaenda jela,hakuweza kuwa na muda wa kukaaa nafamilia yake.
Mjadala ni mrefu sana kuhusu hili la Mandela na Winnie, unaweza pia kutafuta kitabu cha John Curlie ujisomee namna Mandela alivyompata Graca Machel, alivyomtongoza na hatimaye kumuoa. Graca Machel mwanamke mwenye ngekewa ya kuwa mke wa marais wa nchi mbili tofauti.
Kama ni mpenda kusoma vitabu,tafuta kitabu cha "KNOWING NELSON MANDELA", kipo Amazon, kinunue upate simulizi za kusimumua za Winnie na Mandela!