Kwanza tuweke mambo sawa tozo ni aina ya kodi. Hivyo tusiongelee tozo kama vile sio kodi.
Mimi binafsi sijaona ubaya wowote wa serikali kuweka tozo na nina fikiri hakuna njia nyingine kwa wakati huu zaidi ya tozo na nitajaribu kuweka hoja hapa vizuri. Tanzania kama nchi inayoendelea inahitaji pesa ili iweze kuwekeza kwenye miradi mingi sana kuanzia elimu, maji, barabara, umeme, kilimo, ulinzi.......n.k
Sasa vyanzo vya mapato ni hivi
- Missada kutoka nje
- kodi na tozo
- mikopo
Tanzania tumeshakopa na bado tutaendelea kukopa kama tutapata mikopo nafuu lakini vilevile tunakusanya kodi mbalimbali. Lakini ukiangalia vizuri budget zetu pesa ya kodi ambayo haitoshi hata kwenye budget bado inaenda kwenye shughuli ambazo sizo za kimaendeleo hivyo sio uwekezaji wa nchi bali ni matumizi. Kuna miradi tunalipia kwenye kodi kama ya maji na umeme lakini wakati wa Kikwete pesa karibu yote ilikuwa ni kulipa mishahara na matumizi ya serikali.
Sasa kama nchi tuko kwenye kipindi cha uwekezaji kwa mara ya kwanza tunaanza kuona barabara za kisasa, shule bora, hospitali na umeme hasa vijijini. Sasa tumefikaje hapa ? Ni kuwekeza kwa kodi mpya na tozo. Umeme mfano wa vijijini umepelekwa na tozo maalamu kwenye luku za nyumbani na barabara za vijijini nyingi zinatengenezwa na tozo kwenye mafuta. Lakini ili kama nchi tuweze kuwekeza na kuongeza walipa kodi ni lazima tuwekeze kwenye kilimo. Kilimo kitaongeza mapato kwenye kodi lakini tatizo hatuna mfumo mzuri wa kilimo kuwa na uazalishaji wa uhakika. Bashe amekuja na mpango mzuri wa kuongeza uzalishaji kwa kufanya yafuatayo (1) Serikali itatoa ruzuku kwenye mbolea (2) Serikali itawekeza kwenye umwagiliaji (3) watatoa mbegu (4) watafuta wawekezaji wa viwanda (5) kutafuta masoko. Hii ndiyo mojawapo kubwa ya kuongeza ajira na kodi lakini mtaji wa yote haya ni karibu Trillion moja sasa mtaji unatoka wapi? Hii ndiyo sababu imeenda kwenye tozo hivyo tozo ni muhimu kwasababu ni mtaji wa uhakika wa kuongeza kodi kwa miaka ijayo. Lakini ni tukiangalia vizuri tatizo letu ni utamaduni mbovu watu wengi walizoea kukaa bila kulipa kodi wala tozo
Mimi ni diaspora wa muda mrefu sana na naishi na kutafuta maslahi yangu jimbo la Texas. Hili jimbo letu linajulikana kwa kuwa na kodi ndogo lakini ngoja niwape data kidogo ili mgundue tonavyolipa kodi.
- Nyumba kila mwaka nalipa 3% ya thamani ya nyumba. Hivyo kwa mfano kama nyumba pale Tanzania yenye thamani ya Tsh 100,000,000 basi unatakiwa kulipa kila mwaka Tsh 3,000,000. Hakuna mjadala kwenye hili na usikolipa unapekwa mahakamani na nyumba inapigwa mnada
- Jumuia na majiradi vilevile wana kitu kinaitwa HOA-Housing Owners Association hii ni jumuia ya makazi yako na majirani kila nyumba inalipa $350-$1000 kwa mwaka kwa usafi wa jumla kama kukata majani na kusafisha mitaro. Hii ni nje ya nyumba yako hii nayo ni lazima na kisheria wanaweza kwenda na utaratibu mpaka wakapiga mnada nyumba
- Tuna tozo za maji na kuchukuwa taka. Kila wiki wanapita kuchukuwa taka kwenye magaloni maalumu. Hii inafanywa na manispaa huwezi kuchoma matakataka ovyo ovyo. Maji unalipa kutokana ma matumizi lakini taka utalipia unataka au hautaki jumla sio chini ya $100 kila mwezi. Ukitupa uchafu ovyo ni faini, usipoweka uchafu vizuri kwenye mifuko ni faini....
- Barabara nyingi zinajegwa kwa mikopo inayoitwa goverment bonds hivyo ni lazima ilipwe. Kila nikienda kazini kwa mfano ni lazima nipitie kwenye barabara za kulipia "toll roads" na natumia sio chini ya $5-$7 kwenda kwa siku moja na kurudi. Tena hii ni rahisi New York wanatumia $12-$15.
- Ukienda kwenye hotel na kokodi chumba karibu 35% ni kodi na tozo, kwenye simu, cable za TV au Dish hivyohivyo
- Kwenye super market kila ukinunua kitu kuna 5% ya tozo inaenda kusaidia “Metro" ambayo ni kama mwendo kasi yetu.
- Lakini hapa kuna bima ya karibu kila kitu nyumba ni lazima uwe na bima na kwenye hizi bima kuna pesa zinaenda kusaidia idara kama Zimamotto... na ambulance
Hapa sijaongelea tozo na kodi za mishahara. Lakini mjue hapa bado tuna nafuu sana kulinganisha na nchi za Ulaya au Canada ambako Tozo na kodi zipo juu sana. Familia yangu ina bahati tuna nyumba Uninio sehemu ambayo ina thamani sana lakini kodi zetu pale hazifiki hata 1% ya thamani wakati bodaboda wanalipa kodi kwenye mafuta. Hivyo kuna sehemu kiukweli wanaonufaika ni matajiri tu kusema ukweli.
Kuna ambao watasema huko Ulaya na US pesa inaonekana ni kweli tuna shule kwenye kila mtaa za watoto zina mabasi na ni bure lakini tunalipa 3% kwenye thamani ya nyumba na pesa inaenda huko. Hivyo hoja ni yaanze mayai au kuku lakini kodi ni muhimu na maendeleo ni muhimu. Ndiyo maana hoja yangu ni kwamba tozo ni muhimu kwasababu ni mtaji na utaratibu mpya wa kuongeza wigo la walipa kodi na kuweka mifumo ya kimaendeleo. Tatizo kubwa ni mazoea ya watu wengi walikuwa wamezoea kukaa bila shughuli na kubangaiza lakini kama tunataka umeme vijijini, barabara za lami na hospitali ni lazima zitengenezwe, kuwe na pesa za matengenezo kila mara na pesa za wahudumu. Ni lazima kuwe na mfumo wa mapato na wananchi ni lazima wazalishe ili waweze kuwa na mifumo hii. Huwezi kukaa kijijini hulipi kodi yeyote, huzalishi chochote halafu unahitaji barabara, maji, umeme ... pesa inatoka wapi? Ni lazima serikali iwekeze kwenye kilimo ili wewe mwanakijiji uweze kuchangia kodi na maendeleo na ndicho kinacho fanyika kwa sasa
Mkuu, naona umeongea mambo mengi lakini umeshindwa kufafanua uzuri kuhusu hizi kodi na tozo.
Ni kweli kuna kodi na ushuru na hizi zipo kisheria na zatambulika, kisha kuna tozo ambazo uingizaji wake katika mfumo wa kodi hakueleweki na kwahitaji ufafanuzi.
1. Kuna kodi ya maendeleo yaani PAYE, kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT, kodi ya kiwanja yaani ambayo ni kwa maendeleo ya eneo unoishi, kodi ya uingizaji magari nchini, kodi ya uuzaji mali kama nyumba yaani "stamp duty", kodi za uingizaji bidhaa ndogondogo nchini, kodi kwenye usafirishaji bidhaa nje ya nchi na kodi zingine, ila hizi ni kodi na zimewekwa kisheria na zatambulika.
2. Kuna ushuru ambao pia watambulika kama ushuru kwenye mizani, ushuru wa gharama ya ujenzi wa reli, ushuru kwenye kupata leseni ya udereva na ushuru kwenye shughuli za mitandao (sifahamu kama zimeondolewa) na ushuru wa kusafirisha bidhaa zitokanazo na miti, ushuru wa vivuko ushuru mwingine.
3. Kuna tozo ambazo ndizo tatizo na serikali imezi-introduce kwa wananchi kinyemela, tozo ya miamala katika simu za mkononi, miamala kwenye mabenki, tozo katika majengo ambayo mpangaji ahusika. Tozo hizi ni zile ambazo zakatwa mara mbili yaani double Taxation baada ya mtu kukatwa mapato ya PAYE na VAT pamoja na kukatwa katika simu ya mkononi na kukatwa na mabenki ambayo nayo hukata fedha ambazo huziita "account maintenance".
Sasa mimi pia nimeishi huko Marekani na pia nimepata bahati ya kuishi katika nchi zingine lakini ni pale Uingereza ambako nilikaa kwa muda na niliona aina za kodi wanozitoza kwa wananchi wake na mimi kuwa ni mmoja wa watozwa kodi kwa miaka kama mitatu hivi.
Uingereza pale wana kodi ya PAYE, wana kodi ya maendeleo ambayo huiita "council Tax" ambayo kiufundi ni kodi ya majengo au kodi ya kichwa kwani hata mtoto akifika umri wa miaka 18 kama akianza kazi rasmi basi hutakiwa kulipa kodi hiyo.
Hii ndo sababu kubwa pale nchini Uingereza mtoto akifika umri wa miaka 18 huweza hata kufukuzwa ndani ya nyumba ili aende akajitegemee na ajitafutie maisha isipokuwa kama yupo bado asoma.
Hizi kodi mbili yaani kodi ya PAYE huenda serikalini moja kwa moja, lakini ile ya majengo hutozwa na manispaa husika ambayo hutathmini kodi hiyo kila mwaka.
Kodi hii ya manispaa ndiyo huenda kutoa huduma katika manispaa hiyo kama uzoaji taka, ujenzi au uboreshaji wa miundombinu, malipo ya huduma za wazima moto na polisi na shughuli zingine kama ujenzi wa nyumba za kijamii au "social housing", mashule, huduma kwa wazee na wasojiweza pamoja na usimamizi wa maeneo ya kujipumzisha au "recreation parks".
Sasa baada ya mazagazaga hayo ya hizi kodi ndio kuna tozo za kawaida ambazo ni hitaji la lazima kwa kila mwananchi kama tozo ya huduma ya Runinga au TV Lisence, kwamba ni lazima ulipie leseni ya Runinga kuangalia, na hiyo itakuwezesha kuangalia channels zote za bure nchini humo isipokuwa zile channels kali kama za mpira ambazo ni lazima ulipie gaharama za ziada kupitia ankara au bills za kila mwezi. Kwa mfano weye walipia Runinga kiasi kama pauni 245 kwa mwaka, basi hiyo ni mbali na gharama za kuangalia huduma kama za Sky ambazo hutoza kama pauni 60 hivi kwa mwezi na pia zipi huduma zingine kama virgin media na kadhalika.
Kisha kuna tozo ya huduma za simu ya mkononi yaani na ile simu ya ndani telephone bills pamoja na internet ambayo huja kwa vifurushi tofauti. Kuna tozo ya huduma ya maji, umeme, gesi na hizi ni huduma za lazima kwa kila nyumba nchini humo.
Hivyo wakati huu nchini humo wananchi wanalalamika gharama za maisha kupanda, mfumuko wa bei kuwa juu na gharama za mafuta na gesi kutabiriwa kuwa juu zaidi ifikapo mwezi Disemba na January. Lakini viongozi wa nchi hiyo mida hii wana wkati mgumu kuhakikisha kila mwananchi hawapati shida na wanatumia muda mwingi kueleza namna watavyolitatua tatizo hilo ambalo pamoja na kuathiri dunia nzima lakini kila mtu ataubeba msalaba wake.
Sasa nimekuelezea tofauti ya Kodi, Ushuru na tozo na kinachowaudhi watanzania wengi ni tozo ziloibuka bila maelezo na sababu za msingi na pia kuonekana wazi kwenye macho ya watanzania kwamba kitendo hicho ni "double taxation" ambayo yawamiza zaidi watanzania wa kawaida kabisa.
Kwenye hili hakuhitaji ushabiki wala ufuasi wa chama bali umakini na mjadala pevu kwa maslahi ya watanzania wote.
Mjadala huu wa kuhusu Tozo ni "genuine" yaani ni wa kweli na serikali wana budi kuketi na kutafakari namna ya kurekebisha tozo hizi kuendana na hali halisi ya nchi yetu kiuchumi kwa kubuni tozo rafiki zenye unafuu badala ya kutumia mabavu, maneno ya vitisho na kebehi kwamba wanouliza wahamie Burundi.