Hii ndiyo Tarjama, tafsiri ya kwanza kabisa ya Qur’an kwa lugha ya Kiswahili. Ilifanywa na Askofu Godfrey Dale akiwa Mmisionari Zanzibar mwaka 1923.
View attachment 3399727
Kwa bahati mbaya hatuna sokoni tafsiri hii, kwani Waislamu hasa wa Kisunni walizinunua na kuziteketeza.
Shirika la Kimisionari la CMS alilohudumu nalo Padre Dale bado lina nakala mama kule Uingereza, ila toleo hilo halipo sokoni tena.
Dale alikuwa mwanazuoni aliyebobea katika Kiarabu, Kiebrania, Kigiriki, na akajitolea kujifunza Kiswahili kwa muda wa utumishi wake Afrika Mashariki. Inasikitisha kuona kwamba hatuna tena toleo hilo.
Waislamu walipoiona tafsiri hiyo ya kisomi, alijitokeza Sheikh Mbarak Ahmed wa madhehebu ya Ahmadiyya naye akafanya Tarjama ya pili ya Kiswahili, akiifasiri kwa mtazamo wa madhehebu yake.
Toleo lake la kwanza lilichapishwa mwaka 1953. Katika toleo hilo mara nyingi alimzungumzia Padre Dale na kutafuta kumkosoa.
Baada ya toleo hilo, ndipo Waislamu wa Kisunni walipozinduka. Akasimama Sheikh Saleh Abdallah Farsy, aliyekuwa Kadhi Mkuu Zanzibar na baadaye Kadhi Mkuu Kenya. Huyu naye alifanya Tarjama ya tatu ya Kiswahili kwa mtazamo wa madhehebu ya Kisunni.
Kwenye toleo lake aliongeza maelezo mengi ya kumkosoa Sheikh Mbarak Ahmed, ambaye alimwita Qadiani, kwa kuwa Waislamu wa Ahmadiyya wanaamini kwamba Yesu aliwekwa msalabani (japo hakufia pale), ila aliokolewa na kukimbilia India ambako alioa na kupata kizazi. Alikufa Nabii Isa akiwa na umri wa miaka 120 kutokana na ugonjwa wa kipindupindu (cholera). Katika kizazi cha huyu Yesu alizaliwa Mirza Ghulam Ahmad, ambaye ndiye Masihi mtarajiwa yaani Yesu aliyerudi mara ya pili.
Farsy alimkosoa vikali katika sehemu nyingi za tafsiri yake.
Katika miaka ya mwisho wa uhai wake, Sheikh Farsy alibadili misimamo yake na kuegemea madhehebu ya Kiwahabi, akipinga Maulid na ibada za makaburini ambazo Wasunni wengi wa madhehebu ya Kitweliqa (yaani Masufi) wanashiriki.
Baadaye, katika miaka ya 1970, alijitokeza Sheikh Ali Barwani kutoka Zanzibar. Baada ya misukosuko mingi dhidi ya serikali ya CCM na utawala wa Zanzibar, alikimbilia Oman na kutoa toleo la Tarjama ya Kiswahili ambalo leo ndilo linalotumika zaidi kwenye mitandao. Hii ikiwa Tarjama ya nne ya Kiswahili iliyochapishwa Kuwait.
Mapema mwaka wa 2000, Waislamu wa madhehebu ya Kishia nao wakatoa nakala yao ya kwanza ya Kiswahili iliyotolewa na mwanazuoni wao Sheikh Jumaa Ali Mayunga. Hii ni tafsiri ya tano ya Qur’an kwa Kiswahili.
Kwa bahati mbaya, wenzao wa Kisunni walinunua nakala hizi kwa wingi na kuzichoma; zingine zilitupwa baharini Hindi. Leo, japo Mzee Ali Mayunga bado yuko hai, kuzipata nakala za toleo la kwanza ni sawa na kutafuta maziwa ya kuku.
Katika toleo hilo, Sheikh Mayunga aliikosoa misimamo ya madhehebu ya Kisunni, akinukuu baadhi ya hadithi ambazo kabla yake hazikuwahi kutafsiriwa. Kwa sababu hii, alichukiwa mno na tafsiri yake ikaandamwa; leo hii ni vigumu sana kuipata sokoni.
Mnamo 2004–2005, alijitokeza mwanazuoni wa madhehebu ya Kiibadhi kutoka Zanzibar na Oman naye akachapisha tafsiri yake ya Qur’an kwa Kiswahili, akiita Asili ya Uwongofu. Hata hivyo, hii ilichukua mwelekeo wa tafsiri zaidi kuliko tarjama, na aliichapisha kwa juzuu ishirini.
Hii ni Tarjama ya sita ya Kiswahili, japo haikupata umaarufu mkubwa.
Mwaka 2023, Waislamu wa madhehebu ya Sarafu (yaani Mawahabi) nao wamefanikiwa kutoa toleo lao la Qur’an ya Kiswahili, iliyotarjumiwa na jopo la wanazuoni wa Kiwahabi wa Afrika Mashariki. Tafsiri hii inaelekezwa kufanana na toleo la Kiingereza la King Fahd wa Saudia Arabia. Hii ni Qur’an ya saba ya Kiswahili.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na tafsiri/ tarjama nyingi. Hata hivyo, tafsiri za Sheikh Farsy na ile ya Sheikh Ali Barwani ndizo zinazoongoza kwa matumizi miongoni mwa watu wa Afrika Mashariki.
Zipo pia tarjama kama za Sheikh Hassan Mwalupa, Sheikh Abubakar, ambazo hazina umaarufu mkubwa.
Tarjama ya Sheikh Ali Mazrui wa Mombasa haikukamilika kwani alifariki kabla ya kuihitimisha.
Kitendo cha kuchoma au kuharibu tafsiri mbadala za Qur’an hakionyeshi nguvu ya hoja, bali ni alama ya woga na ukosefu wa ujasiri wa kukabiliana na ukweli katika mjadala wa wazi. Badala ya kujadili tofauti za kiitikadi kwa hoja na maarifa, baadhi huchagua kutumia moto kufunika kile ambacho hawawezi kukipinga kwa mantiki. Kwa kufanya hivyo, wanafunga milango ya elimu, kudhibiti fikra huru, na hatimaye kupotosha historia ya namna Uislamu ulivyoeleweka na kutafsiriwa na wasomi wa madhehebu mbalimbali.
Kwani, ikiwa kweli tafsiri nyingine ni potofu mbona zisiwe fursa ya kujenga hoja madhubuti dhidi yake? Moto hauwezi kuzima hoja; huacha tu majivu ya uoga na mabaki ya fikra zilizozuiliwa.