Mara nyingi matatizo katika kujieleza yanaonesha matatizo katika kufikiri.
Hususan, kukosa uwezo wa kufikiri kwa kina, au kutojali habari za kufikiri kwa kina.
Sifikiri kwamba hatuna uwezo wa kufikiri kwa kina. Hakuna sababu ya kunifanya nikubali hilo. Naona kama tumekubali utamaduni wa kutofikiri kwa kina.
Wengi tunatakiwa kubadilika kwa angalau haya.
1. Kufikiri kabla ya kusema. Ni rahisi kuharibu kujieleza kama tunasema sana bila kufikiri.
2. Kujali wengine sana. Ukijali wengine, utaweza kufikiri sana jinsi ya kujieleza mpaka wakuelewe vizuri. Kwa mfano, ukiongea na mtoto, ukimjali, utataka kuongea kwa njia ambayo mtoto atakuelewa. Ukimuelezea mtoto kwa lugha ambayo imekaa kikubwa utamchanganya. Mara nyingi makosa katika kujieleza yanaonesha mtu anayejieleza kutojali wanaomsikiliza.
3.Kujifunza kujieleza kutoka kwa watu maarufu waliofanikiwa kuweza kujieleza kwa umakini. Kuna watu wana kipaji hiki. Ni muhimu kuwasoma.
4. Kusoma vitabu. Kusoma kunajenga mawazo na kupanua wigo. Kunatupa kanuni za msingi za kufuatilia na jinsi ya kuzihakiki.
5. Kutotaka kutafsiriwa vibaya. Ukiwa hutaki kutafsiriwa vibaya utaweka juhudi zaidi kujieleza vizuri. Kwa mfano, hata ukisema kitu, halafu ukagundua hakijamalizika au kina utata, utarudia ili kufanya masahihisho au maongezo. Hiki ni kitu ambacho wengi wetu hatufanyi.
6. Kumalizia sentensi. Jaribu kumalizia kila sentensi na wazo. Usidhani tu kila mtu anaelewa unachosema na anaweza kumalizia.
7. Kuelezea mambo kutoka mwanzo mpaka mwisho. Tuepuke kuanza kuelezea habari kutoka kati au bila hitimisho.
8. Kuuliza kama umeeleweka au kama kuna maswali. Mara nyingi mawasiliano ni kitu chenye utata, kwa sababu, hujui mwingine unayewasiliana naye ana uwezo gani, kaelewa nini, hajaelewa nini n.k. Hivyo, ni muhimu kumuachia nafasi na yeye ajieleze, kumpa muda wa kuuliza maswali na kuweza kuhakiki kwamba wote mnaelewana. Kuna watu wakianza kuongea wanataka kuongea wao tu bila kuwapa nafasi wengine.
9. Kuangalia "non verbal communication". Mambo mengine hayasemwi, unaweza kuona mtu anaangalia saa yake wakati mna maongezi ukajua labda unamchelewesha. Hapo unaweza kumpa nafasi ya kuaga kwa kumuuliza "Una miadi sehemu nini?"
10. Kusikiliza si tu kinachosemwa, bali hata ya kilichoachwa kusemwa. Ukimuuliza mtu swali moja, halafu asijibu hilo swali na kujibu lingine, unatakiwa kujua ama hajaelewa swali au anataka kuficha na kutojibu. Unaweza kuamua kuuliza swali tena ili kumpa nafasi ajibu, hususan kama unaona hajaelewa, au kuacha kuuliza kwa kuona anakwepa kujibu.