Mtoto wa Kikwete azua balaa kwa Mwakyembe
Kundi la vijana lapanga kumfanyia vurugu kwenye harambee
na Moses Ng'wat, Mbeya
HARAMBEE ya kuchangisha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wilayani Kyela, mkoani hapa, iliyopangwa kufanyika juzi, imeshindwa kufanyika kutokana na kile kinachodaiwa kuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo, mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani Kikwete, kushindwa kufika.
Habari za uhakika kutoka ndani ya umoja huo wilayani Kyela, zilidai kuwa Ridhiwani ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, akiwakilisha Mkoa wa Pwani, alishindwa kufika kwenye hafla hiyo iliyopangwa kufanyika katika ukumbi wa Kyela Business Center (KDF), kwa madai ya kuwapo kwa kundi la vijana lililopanga kufanya vurugu, kwa sababu za kisiasa.
Vyanzo vyetu vya habari kutoka Kyela, vinadai kuwa kundi hilo la vijana ambalo halijulikani liko upande gani, lina hofu kuwa harambee hiyo ilikuwa na lengo la kumjenga mmoja wa vijana (jina limehifadhiwa), anayedaiwa kutaka kuwania kiti cha ubunge katika jimbo hilo ambalo kwa sasa linashikiliwa na Mbunge machachari bungeni, Dk. Harrison Mwakyembe.
Kwa mujibu wa habari hizo, Ridhiwani alitarajia kufika katika ukumbi huo majira ya saa mbili za usiku juzi, lakini licha ya vijana kuwapo kwa wingi wakimsubiri mgeni huyo rasmi, hakuweza kutokea na hakuna sababu zilizotolewa na kusababisha harambee hiyo ishindwe kufanyika.
Ilipofika majira ya saa nne usiku, minong'ono ilianza kuzagaa ndani ya ukumbi huo kwamba huenda mtoto huyo wa Rais Kikwete, alishindwa kufika kutokana na taarifa za kiusalama kwamba kuna kundi lililoandaa vurugu ili harambee hiyo isifanyike kwa hofu za kisiasa.
Baadhi ya wanachama wa UVCCM, waliozungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotaja majina yao, walisema baada ya kukwama kufanyika kwa harambee hiyo, kuliibuka makundi mawili ndani ya ukumbi huo, moja likifurahia kutofika kwa Ridhiwani, likiamini kuwa limeshinda, huku jingine likihuzunika kwa kutofanyika kwa shughuli hiyo.
Hata hivyo kundi lililokerwa na kushindwa kufika kwa Ridhiwani, lilielekeza lawama zake kwa uongozi wa jumuiya hiyo kwamba haukuwa na uhakika na kitu walichokiandaa na kwamba hiyo ni ishara ya uongozi huo kushindwa kutekeleza majukumu mbalimbali ya umoja huo, ikiwamo kushindwa kuwashawishi vijana kuachana na siasa za makundi katika wilaya hiyo.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa UVCCM, mkoani Mbeya, Reginald Msomba, alikiri kuwapo kwa ziara ya Ridhiwani mkoani mwake kwa ajili ya kuwa mgeni rasmi kwenye harambee hiyo ya kuchangia fedha kwa ajili ya miradi ya vijana wilayani Kyela.
Alisema yeye kama mwenyekiti wa Umoja huo, alipewa taarifa za ziara hiyo kwamba Julai 31, mwaka huu, alitakiwa ampokee mjumbe huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana Taifa kutoka mkoani Pwani ili kwenda naye Kyela kwa ajili ya shughuli hiyo.
Kwa kweli jambo hilo lilikuwapo ndugu mwandishi, lakini mimi nilishangaa kutompokea mgeni huyo ambaye tulikuwa tuongozane naye hadi Kyela, lakini hadi majira ya jioni hakutokea na mimi nilipewa taarifa za kuelekea huko bila maelezo mengine," alisema Msomba bila kufafanua alikokuwa akipata maelekezo hayo.
Alipotakiwa kueleza sababu za kuahilishwa ghafla kwa ziara hiyo wilayani Kyela, alisema yeye hawezi kulizungumzia hilo kwa kuwa liko nje ya uwezo wake, na kuongeza kwamba watu waliopaswa kulizungumzia ni viongozi wa umoja huo Wilaya ya Kyela.
Juhudi za kumpata Mwenyekiti wa UVCCM Kyela, Hanta Mwakifuna, kwa njia ya simu kutoka Kyela zilifanikiwa, lakini hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, hususan sababu za kushindwa kufika kwa mgeni rasmi Ridhiwani Kikwete.
Mimi sidhani kama kuna haja ya suala hili kupelekwa kwenye vyombo vya habari, kwa kuwa hata utaratibu wa kumualika hatukuufanya kupitia vyombo vya habari, naomba unielewe kuwa shughuli haikufanyika na sasa tunaangalia jinsi ya kuandaa upya, sihitaji kukuambia kama alifika au hakufika," alisema.
Alipotakiwa kuelezea iwapo kushindwa kufika kwa Ridhiwani kumekwamisha malengo ya umoja huo wilayani Kyela, mwenyekiti huyo alisema lengo lao halikutimia, na kusisitiza kuwa wanajipanga upya kumwita kwa ajili ya harambee hiyo.
Kuhusu tetesi za kuwapo kwa kundi lililopanga kumfanyia vurugu mgeni huyo kwa sababu za kisiasa, Mwakifuna alikanusha taarifa hizo, kwa madai kuwa si sahihi.
Alisema hafikiri kama kuna vijana waliochochewa kufanya vurugu, kwa kuwa kazi hiyo ililenga kufanikisha uchumi wa miradi ya vijana wa chama hicho.
Taarifa hizo ni za kisiasa tu na hazihusiki kwa namna yoyote na kutofika kwa Ridhiwani," alisema bila kutaja sababu nyingine iliyomfanya Ridhiwani kutofika kwenye harambee hiyo.
Alisisitiza kuwa harambee hiyo itafanyika katika tarehe itakayopangwa upya. Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, UVCCM wilayani Kyela katika harambee hiyo walitarajia kukusanya zaidi ya sh milioni 155, ambapo hadi kufikia juzi, walikuwa wamekusanya sh milioni 21.9, zilizochangwa na watu mbalimbali, wakiwamo vijana wa umoja huo kutoka kata zote 21 za wilaya hiyo.