Kwa ujumla dondoo nyingi kwenye uzi huu ni sahihi. Kujazia tu nitataja za ziada zifuatazo.
Dr Kleruu alikuwa Mkristu, msomi wa Kichaga mwenye PhD aliyefanywa kuwa Mkuu wa Mkoa Iringa mwezi Januari 1971 akihamishwa kutoka Mtwara. Alikuwa mpenzi wa siasa ya Ujamaa iliyokuwa ikihamasisha vijiji vya Ujamaa. Siku ya tukio ilikuwa Krismas, tarehe 25 Desemba 1971. Mwamwindi alikuwa Mwislamu ambaye siku hiyo alikuwa akilima shambani kwake kwa trekta.
Hapo shambani kulikuwa na makaburi ya wahenga wa Mwamwindi ambayo ni mojawapo ya sababu iliyomfanya Mwamwindi aendelee kulihifadhi shamba hilo. Katika majibizano, Dr Kleruu alidiriki kuyakashifu makaburi hayo, kitu ambacho kilimuudhi sana Mwamwindi na kuamua kumuulia mbali Mkuu huyo wa Mkoa.
Baadhi ya vitu vilivyojitokeza upande wa utetezi katika kesi hiyo ya mauaji ni vifuatavyo:
1. Dr Kleruu, Mchaga ambaye hakufuata 'mila' za kabila lake za kwenda 'kuhiji' nyumbani kwao wakati wa Krismas.
2. Dr Kleruu, Mkristu ambaye anachagua kufanya kazi siku ya Krismas, kuhimiza utekelezaji wa zoezi la vijiji vya Ujamaa.
3. Mkuu wa Mkoa anaendesha gari yeye mwenyewe peke yake umbali wa takriban km 40 kwenda shambani kwa Mwamwindi.
4. Dr Kleruu kukashifu makaburi ya wahenga. Wazee kadhaa wa kabila la Mwamwindi waliitwa na kuthibitisha kuthamini huko kwa makaburi.
5. Kwa kuwa Mwamwindi alikuwa Mwislamu, haikuwa ajabu kwake kuwa analima siku ya Krismas.
Baada ya kumuua, aliuweka mwili kwenye buti la gari alilokuja nalo Mkuu wa Mkoa na kuendesha hadi kituo cha Polisi mjini Iringa. Hapo akawaambia polisi waende wakachukue 'mbwa wao' kwenye buti. Mwamwindi akashikiliwa kwa uchunguzi na kesi ikaanza kusikilizwa. Ilidumu miezi kumi tu Mwamwindi akapatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia. Akahukumiwa kunyongwa na hukumu hiyo ikatekelezwa.