ALHAJ Ali Hassan Mwinyi, ametokeza na kumlaumu January Makamba, kutumia picha yao ya zamani wakicheka pamoja kwenye 'twiti' ya kuridhia kutenguliwa Uwaziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Mwinyi amehoji, kwa nini picha hiyo itumike kipindi mambo yamekoregeka? Ukimwelewa Mwinyi, ni kama anashawishika kuamini kwamba picha imetumika vibaya na inatoa tafsiri kwamba yeye na January wanachekelea uamuzi wa Rais Magufuli kutengua uteuzi wa January Baraza la Mawaziri.
Maneno ya 'twiti' ya January akisema, amepokea mabadiliko yaliyofanyika kwa moyo mweupe kabisa, akiambatanisha 'emoji' ya cheko la upendo, kisha picha kuwaonesha January na Mzee Mwinyi wakichekelea, hapo ndipo mwanzo wa nongwa.
Ni hofu tu! Inawezekana Mzee Mwinyi alielewa vibaya au kuna watu walimshawishi kuelewa tofauti. Hofu ingeondoka, picha hiyo ina thamani kubwa kwa Mwinyi. Na Mwinyi angeona raha namna anavyokuwa hamasa kwa vijana viongozi wa kizazi cha sasa.
Ipo hivi; mwaka 1974, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Shinyanga, Michael Mabawa, alitumia askari wa Jeshi la Polisi, kufanya oparesheni ya kusaka wachawi, wananchi wasio na hatia walipigwa na kudhalilishwa mno kwa tuhuma za kujihusisha na ushirikina.
Kwa kitendo hicho, Mwinyi akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, bila kupoteza muda, alimwandikia barua ya kujiuzulu, Mwalimu Nyerere, kwa sababu polisi ambao walikuwa chini ya wizara aliyoiongoza, walipiga na kutesa raia.
Mwaka 1984, miaka 10 baada ya tukio hilo, kikao cha Halmashauri Kuu CCM kilimvua Urais wa Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe kisha Mwinyi akapitishwa kuwa Rais wa visiwa hivyo. Mwaka 1985, Mwinyi akawa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akamrithi Mwalimu Nyerere.
Hivyo, Mwinyi ni alama yenye kutoa hamasa kwa viongozi hasa vijana, kutambua kuwa zipo nyakati za kuteleza na kuanguka, lakini muhimu ni kujikusanya, kunyanyuka na kuendelea na mwendo. January katika picha yake na Mwinyi, bila shaka alikusudia tafsiri kuwa aliyopata ni ajali kama ya Mwinyi, hivyo atanyanyuka kama alivyonyanyuka Mwinyi. Hapo kuna ubaya gani?
Muhimu ni kwamba January ana ndoto za kuwa Rais. Mwinyi alikuwa Rais baada ya ajali ya kujiuzulu. Ni kosa January kujipa moyo kuwa ipo siku atakuwa Rais baada ya ajali ya kutenguliwa? Tatizo siku hizi hofu inafubaza uwezo wa kufikiri. Uoga umetamalaki!
Ndimi Luqman MALOTO