Lema ajue CHADEMA haimiliki siasa za upinzani Tanzania, wanaharakati wana haki ya kumkosoa

Elias Msuya

Platinum Member
Joined
Dec 23, 2011
Posts
267
Reaction score
1,014

Mfumo wa vyama vingi ulirejeshwa Tanzania mwaka 1992 kwa shinikizo la Mwalimu Julius Nyerere, lakini Katiba haikufanyiwa mabadiliko ya kutosha kuhakikisha ushindani wa kisiasa wenye usawa.

Ibara ya 3 ilitambua mfumo huo, lakini mamlaka makubwa ya Rais, usimamizi wa uchaguzi na mazingira ya uendeshaji wa vyama viliendelea kuibua changamoto.

Aidha, wananchi hawaruhusiwi kugombea kama wagombea binafsi, huku vyama vikisimamiwa na Msajili aliye ndani ya mfumo wa Serikali. Hali hii imeendeleza mjadala kuhusu ukiritimba wa kisiasa na umuhimu wa Katiba mpya itakayohakikisha fursa sawa kwa wote.

Ukiritimba unaanza hata ndani ya vyama vya upinzani

Bahati mbaya, hata ndani ya vyama vya siasa, ambako kunapaswa kuwa na nafasi pana ya mijadala na mawazo tofauti, nako kuna dalili za ukiritimba. Baadhi ya viongozi wanajipa mamlaka ya kuamua nani ana haki ya kutoa maoni kuhusu chama na nani anapaswa kunyamaza.

Siku hizi, mtu akikosoa mwenendo au maamuzi ya chama fulani, haraka anapachikwa jina la mwanaharakati, kana kwamba kuwa mwanachama wa chama hicho ndiyo sharti pekee la kuwa na haki ya kukizungumzia.

Nimemsikia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, akiwalalamikia wanaharakati, hasa wale wanaoishi nje ya nchi, akiwatuhumu kuvuruga chama hicho.

Kimsingi, malalamiko yake yanaonekana kumlenga zaidi Mange Kimambi, ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akimkosoa vikali Lema kwa kile anachodai kuwa anashirikiana na upande wa CCM kutafuta maridhiano, kinyume na msimamo wa CHADEMA.

Awali, Lema alipanga kuitisha mkutano na waandishi wa habari mwezi Septemba ili kumjibu Mange na wanaharakati wengine, lakini baada ya kushauriana na viongozi wenzake wa chama aliahirisha mpango huo. Hata hivyo, baada ya shutuma za Mange kuendelea, Lema alijitokeza Novemba 1, 2026 jijini Arusha na kumjibu vikali.

Strategic engagement: Kuna tofauti gani na maridhiano ya Mbowe?

Katika maelezo yake, Lema alizungumzia kile alichokiita strategic engagement (ushirikiano au mawasiliano ya kimkakati) na kutoa mifano ya namna anavyotumia mawasiliano na viongozi wa Serikali kutatua changamoto zinazokikabili chama.

Soma zaidi: Lema: Kufanya vikao vya kimkakati sio usaliti. Watu wamesaidiwa kwa njia hiyo

Alitolea mfano tukio la kusitishwa kwa mkutano wa hadhara wa CHADEMA mkoani Morogoro, akisema alimpigia simu mkuu wa mkoa na kupata ufumbuzi wa suala hilo.

Lema alisisitiza kuwa anachofanya ni sehemu ya mapambano ya kumtetea Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, ambaye amekuwa gerezani kwa muda mrefu kutokana na kesi inayomkabili. Katika kujenga hoja hiyo, alitumia mfano wa magenge ya dawa za kulevya (drug cartels) yanavyoweza kupigania mtu wao anapofungwa.

Hapa ndipo ninapoona kuna maswali ya msingi ambayo Lema anapaswa kuyajibu. Je, anauona utetezi wa Lissu kama suala la kutafuta huruma kutoka kwa CCM au Serikali ili aachiwe huru? Je, anapendekeza mazungumzo hayo yafanyike kwa misingi ya kuomba msamaha au huruma?

Lissu mwenyewe amekuwa akisisitiza kuwa hataki kuonewa huruma. Katika maelezo yake ya mwisho mahakamani, alieleza kuwa kama atapatikana na hatia apewe hukumu inayostahili, lakini kama hana hatia aachiwe huru.

Kwa hiyo, ni aina gani ya huruma ambayo Lema anadhani inahitajika kwa Lissu? Je, ni kuomba Serikali imsamehe au kudai haki yake kupitia mfumo wa sheria?

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, amekuwa akisisitiza kuwa chama hicho hakitapiga magoti mbele ya CCM. Je, Lema huwa hasikii kauli za viongozi wenzake kuhusu msimamo huo?

Lema pia alieleza wasiwasi wake kuhusu Tume ya Jaji Shaaban Lila, akisema CHADEMA inaweza kulaumiwa kwa matukio ya Oktoba 29, 2025 na viongozi pamoja na makada wake kujikuta wakikabiliwa na mashtaka.

Soma zaidi: Lema: Ripoti ya Jaji Lila viongozi wengi wa CHADEMA wataishia Jela

Kwa mtazamo huo, inaonekana Lema anaona strategic engagement kama njia ya kujinasua katika mazingira hayo. Lakini je, kuna tofauti gani ya msingi kati ya anachokifanya sasa na kile alichokuwa akikifanya Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Freeman Mbowe, ambaye Lema alishindana naye katika uchaguzi wa uenyekiti wa Januari 22, 2025?

Mbowe alipotoka gerezani, alikutana na Rais Samia Suluhu Hassan na kuanza mazungumzo ya maridhiano kati ya CCM na CHADEMA, ambayo baadaye yalikwama.

Pamoja na mafanikio ambayo Mbowe amekuwa akiyataja kutokana na mazungumzo hayo, yakiwamo kulipwa kwa malimbikizo ya ruzuku na kuachiliwa kwa baadhi ya makada waliokuwa wanakabiliwa na kesi mbalimbali, matatizo ya msingi ya mfumo wa uchaguzi na kutokuwepo kwa mabadiliko ya Katiba yaliendelea kuwepo.

Ndiyo maana, licha ya maridhiano hayo, katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, CCM ilipata nafasi nyingi huku kukiwa na malalamiko ya vyama vya upinzani kuhusu mwenendo wa uchaguzi. Hali hiyo iliendelea kuwa sehemu ya malalamiko yaliyojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Upinzani hauwezi kuwa mali ya chama kimoja

Lema anajitetea kuwa anachofanya ni kulinda CHADEMA kama taasisi. Anawakosoa wanaharakati, hasa wanaoishi nje ya nchi, akiwatafsiri kama watu wanaoweza kuwa sumu kwa chama hicho na pengine kwa siasa za upinzani kwa ujumla.

Hata hivyo, Lema anapaswa kuelewa kuwa Tanzania imefika hatua ambayo siasa za upinzani haziwezi tena kufungamanishwa na vyama pekee. Wananchi wana uhuru wa kuikosoa CCM na Serikali yake hata kama si wanachama wa CHADEMA au chama kingine chochote cha upinzani.

Ni kweli CHADEMA imepata nguvu kwa sababu ya kusimamia baadhi ya misimamo inayoendana na malalamiko na matarajio ya wananchi. Lakini hilo halimaanishi kuwa chama hicho kina hati miliki ya upinzani nchini.

Ikiwa CHADEMA nayo itaanza kujenga ukiritimba kwa kudhani kuwa ni yenyewe pekee inayopaswa kuongoza mapambano ya kisiasa, wananchi wanaweza kuachana nacho na kuendeleza harakati zao kupitia njia nyingine.

Oktoba 29 ilionyesha kuwa wananchi wanaweza kusimama wenyewe

Tukio la maandamano ya Oktoba 29, 2025, linaweza kutumika kueleza hoja hii. Maandamano hayo hayakuwa mali ya CHADEMA wala chama kingine cha siasa. Wananchi walijitokeza na kuandamana kwa sababu ya malalamiko na madai yao wenyewe.

Wakati huo, viongozi kadhaa wakuu wa CHADEMA walikuwa wamekamatwa, huku kukiwa na hofu kuwa wao ndio wangeongoza maandamano hayo. Hata hivyo, wananchi walijitokeza na kufanya maandamano katika maeneo mbalimbali ya nchi, na yaliyotokea baadaye yanajulikana.

Hii inapaswa kuwa fundisho kwa Lema na viongozi wengine wa vyama vya upinzani kwamba nguvu ya mabadiliko haiwezi kuwekwa ndani ya ofisi za vyama au mikononi mwa viongozi wachache.

Lema anapodhani kuwa CHADEMA ndiyo kila kitu katika siasa za upinzani, anajidanganya. Hii ni dhana inayofanana na ile ya CCM, ambayo nayo wakati mwingine huonekana kuamini kuwa kila kitu katika siasa za Tanzania kinapaswa kupitia vyama vya siasa.

Ndiyo maana CCM imekuwa ikijaribu kuishawishi CHADEMA kuingia katika mazungumzo ya maridhiano, kana kwamba kukubaliana na chama hicho kutamaliza malalamiko yote yaliyopo nchini.

Wanachoshindwa kuelewa ni kwamba chini ya mfumo rasmi wa vyama kuna wananchi wenye malalamiko mengi. Wapo wanaolalamikia kukosekana kwa uhuru wa maoni, hali ngumu ya uchumi, ukosefu wa usalama na matukio ya watu kutekwa, kupotezwa na kuuawa, huku wakidai hakuna uwajibikaji wa kutosha.

Kwa hiyo, hata kama CCM itafanikiwa kufanya maridhiano na CHADEMA, hilo pekee haliwezi kuondoa malalamiko yote ya wananchi.

Wanaharakati ni sehemu ya sauti za wananchi

Wanaharakati walio nje ya nchi, wakiwamo Mange Kimambi, Maria Sarungi na wengine, ni sehemu ya watu wanaotumia majukwaa yao kutoa maoni na kukosoa mwenendo wa Serikali na taasisi mbalimbali.

Ni kweli wanaweza kukosea katika baadhi ya hoja zao, kama ilivyo kwa viongozi wa vyama vya siasa. Lakini hilo haliondoi haki yao ya kutoa maoni, kuhoji maamuzi ya viongozi na hata kukosoa CHADEMA.

Baadhi yao wana majukwaa makubwa ya kuzungumza, lakini hoja wanazozijadili zinagusa pia malalamiko ya wananchi ambao hawana nafasi au majukwaa ya kuyasemea.

Kwa hiyo, Lema anapaswa kutambua kuwa kukosolewa si kuvurugwa kwa chama. Viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa tayari kupokea hoja tofauti, kuzijibu na kujitathmini badala ya kuwashambulia wanaohoji misimamo au maamuzi yao.

Somo la Nabii Eliya: Usidhani umebaki peke yako

Katika mazingira haya, ninapata kumbukumbu ya kisa cha Nabii Eliya kinachopatikana katika kitabu cha 1 Wafalme sura ya 18 na 19.

Ni simulizi la nabii huyo aliyepata ushindi mkubwa dhidi ya manabii wa Baali katika Mlima Karmeli, lakini baadaye akakumbwa na hofu, uchovu na kukata tamaa kiasi cha kumwomba Mungu amuondolee uhai.

Baada ya Eliya kumwomba Mungu, moto ulishuka kutoka mbinguni na kuteketeza sadaka yake, jambo lililowafanya Waisraeli kukiri kuwa Bwana ndiye Mungu wa kweli. Baadaye, kwa agizo lake, manabii wa Baali walikamatwa na kuuawa.

Hata hivyo, ushindi huo haukumaanisha mwisho wa changamoto zake. Malkia Yezebeli, mke wa Mfalme Ahabu, aliposikia yaliyotokea, alituma ujumbe wa kutishia kumuua Eliya.

Nabii huyo aliingiwa na hofu, akakimbilia jangwani na kukaa chini ya mti wa mretemu. Akiwa amechoka na kuvunjika moyo, alimwomba Mungu aondoe uhai wake, akisema amechoka na safari ya maisha.

Alipoambiwa na Mungu aeleze anachofanya hapo, Eliya alijibu kuwa amekuwa na wivu kwa ajili ya Bwana, lakini Waisraeli wameyaacha maagano yake, wamezibomoa madhabahu zake na kuwaua manabii wake. Akaongeza kuwa amebaki yeye peke yake na sasa wanataka kumuua pia.

Lakini Mungu alimfunulia jambo ambalo Eliya hakuliona. Alikuwa amejisazia watu 7,000 katika Israeli ambao hawakuwa wameipigia magoti Baali wala kumbusu.

Katika simulizi hilo, Mungu hakumwambia Eliya kwamba ameshindwa au kazi yake imekwisha. Badala yake, alimpa chakula, mapumziko na nguvu za kuendelea na safari yake.

Lema, mapambano ni makubwa kuliko CHADEMA

Hivyo basi, Lema anapaswa kuelewa kuwa wapo maelfu na mamilioni ya Watanzania wanaoendeleza mapambano ya kudai haki, uwajibikaji, uhuru na mabadiliko ya kisiasa. Wengine ni wanachama wa CHADEMA, wengine ni wanachama wa vyama vingine, na wengine hawana chama kabisa.

Hakuna chama chenye hati miliki ya malalamiko ya wananchi wala haki ya kuamua nani anapaswa kuyazungumza.

Kama kuna jambo la kujifunza kutoka kwa Nabii Eliya, ni kwamba unapokuwa kwenye mapambano, usifikiri kuwa kwa sababu huoni wenzako basi umebaki peke yako.

Na pengine ujumbe muhimu zaidi wa Mungu kwa Eliya ndio unaopaswa kuwa fundisho kwa kila anayehisi amechoka na mapambano: 1 Wafalme 19:7

"Ondoka ule; kwa maana safari hii ni kubwa mno kwako."

Lema ajue kuwa safari ya kudai mabadiliko ya Tanzania ni kubwa kuliko CHADEMA, kubwa kuliko viongozi wake na kubwa kuliko mtu mmoja mmoja. Wanaharakati wana haki ya kukosoa, wananchi wana haki ya kudai mabadiliko, na hakuna chama kinachopaswa kujiona kuwa ndicho pekee chenye mamlaka ya kuongoza sauti za upinzani nchini.
 
Elias, ni kweli wanaharakati au mtu yeyote ana haki kuikosoa Chadema.
Lakini hao wanaharakati hawana haki ya kuleta uzushi dhidi ya Chadema au chama kingine au mtu yeyote.
Siko hapa kumtetea Lema, lakini wewe Elias kama mwandishi wa habari unaona sawa kwa mwanaharakati Mange kuzua habari kwamba Lema na ndugu zake Lissu wamekaa Sea Cliff hotel kwa gharama ya Abdul Hafidh Ameir...habari ambayo imeshathibitishwa kwamba ni uongo?
Lema anaweza kuwa na mapungufu yake,..na pengine alikosea kumjibu mzushi wa hiyo habari Mange....lakini Lema alikuwa sahihi kusema Chadema kama taaaisi kilitakiwa kutoa taarifa kukanusha hiyo habari ya kizushi ya Mange.
Hiyo ni muhimu kwa vile kwa sasa mitandao ya kijamii ina nguvu ya kufikisha taarifa za kweli na uzushi kwa haraka kuliko mikutano ya hadhara, na pia kuna watu wengi wanaamini kila wanachokisema wanaharakati kuwa ni cha kweli. Katika hali hiyo, kushambuliwa kwa Lema kibinafsi,kuna atahari kwa chama kama taasisi kwa vile yeyw ni sehemu ya viongozi wa chama.
Kwa hiyo uongozi wa Chadema ukikuwa na wajibu wa kutolea ufafanuzi madai ya Mange na kuweka hali sawa ili kutopoteza imani ya taasisi yao kwa wananchi.
 
Mange anahaki ya kuongea na huwezi mzuia na huwezi wazuia wanaharakati wengine kuongea

Lema alipeleka malalamiko yake ya mange chamani alijibiwa mange sio mwanachama wa chadema au kiongozi wa chadema chama kinamjibuje

Ukiwa kiongozi sio kila tuhuma unatakiwa ujibu kama unaamini wewe ni msafi
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…