Huku Tanzania ikijiandaa kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mnamo Novemba 27, Chadema inaonekana kuingia katika hali ya sintofahamu inayofichua woga wa kushindwa.
Zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la makazi linaendelea kutoka Oktoba 11 hadi 20, lakini matamshi ya viongozi wa Chadema yanaibua maswali kuhusu dhamira yao ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huu.
Leo, Godbless Lema, mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini na mbunge wa zamani wa Arusha Mjini kupitia Chadema, amefanya mkutano na waandishi wa habari, akitoa lugha kali zilizojaa matusi kwa wasimamizi wa uchaguzi.
Lema amemwita mmoja wa wakurugenzi “mshamba na mpuuzi,” akitishia kwamba iwapo uchaguzi huo hautawiana na matarajio yao, “vita ya wenyewe kwa wenyewe itatokea kwani Chadema watalipuka.”
Maneno haya yameonesha kwamba Chadema wanapanda mbegu za hofu na taharuki miongoni mwa wanachama wao, badala ya kujipanga kwa ushindani wa kweli.
Kama inavyojulikana, Chadema wametumia muda mwingi kulalamika kuliko kuhamasisha wanachama wao kujiandikisha na kushiriki kwenye uchaguzi wakati vyama vingine vikiweka mikakati ya kuwafikia wapiga kura, Lema anajikita zaidi katika matusi na malalamiko, ikiashiria kwamba chama chake hakijawa na mipango madhubuti ya ushindani.
Aidha, Lema alilalamika kuhusu uandikishaji wa vijana wa shule za sekondari, akisema, "Kwa nini watoto wa Form 3 wanaandikishwa?" Hii ni ishara ya kutokuwa na uwezo wa kuelewa sheria na taratibu za uchaguzi, kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaruhusu vijana wenye miaka 18 na wale wenye miaka 17 ambao mwakani watakuwa na umri wa kupiga kura.
Badala ya kujiandikisha na kuwajengea vijana uelewa kuhusu umuhimu wa kushiriki kwenye uchaguzi, Lema na Chadema wanaendelea na malalamiko yasiyo na msingi.
Kwa mujibu wa Lema, licha ya baadhi ya wanachama wa Chadema kuonesha nia ya kususia uchaguzi huu, yeye amesisitiza kwamba atashiriki, akijinasibu kuwa "jasiri" asiyeogopa kushindwa.
Hata hivyo, kauli hii imeonesha kujificha nyuma ya ujasiri wa maneno, wakati ukweli ni kwamba Chadema hawana mipango ya kina ya kushinda.
Je, hii inamaanisha kuwa Chadema wanajaribu kuhalalisha hatua yao ya kusitasita, wakitafuta kisingizio cha kushindwa mapema huku wakihamasisha hofu kwa wapiga kura?
Je, ni woga wa ushindani au ni mikakati ya kujitenga na kushindwa?
Muda utaamua, lakini kwa mtindo huu wa kujiandaa, ni dhahiri kwamba Chadema wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kushinda uchaguzi ujao.