Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
DESEMBA 21, mwaka 2009, Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne Tanzania anatimiza miaka minne ya kukaa madarakani, tangu alipoapishwa kuwa Rais Desemba 21, 2005.
Kazi ya urais si nyepesi kama wengi wanavyodhani, kama muasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alivyohoji, wapinzani wanakimbilia Ikulu kuna nini?
Kazi ya kuongoza watu ni nzito aliyotwishwa na Watanzania tangu kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Tanzania Desemba 14, 2005.
Mtihani wa kwanza mkubwa alipoingia Ikulu ya Magogoni, ilikuwa kushinda shinikizo kubwa la wanasiasa waliotaka kulipwa fadhila kwa kupewa vyeo eti kwa sababu kaingia Ikulu.
Katika kundi la mamba hata kenge wamo, wapo waliotaka kupewa fadhila hizo kwa sababu za kibiashara na shughuli nyingine ili kuzifanya zipite kiulaini.
Rais akafanya uteuzi wa Baraza la Mawaziri 60, wananchi wengi wakahoji juu ya ukubwa wa baraza hilo ingawa Rais Kikwete mwenyewe alisema amefanya hivyo ili kusukuma mambo ya maendeleo kwa kasi kubwa aliyoitazamia.
Kuunda Baraza la Mawaziri, Mawaziri kamili 30 na Naibu Mawaziri zaidi ya 30 kutokana na miongoni mwa wizara kuwa na manaibu wawili, si jambo la kawaida.
Hilo lilikuwa baraza kubwa kwa serikali na walipa kodi wake. Hata hivyo pamoja na nia nzuri ya Rais kuwateua wasaidizi wake, kilichotokea ni baadhi ya mawaziri kutotimiza wajibu wao ipasavyo hatua iliyomfanya Rais Kikwete kupanga upya safu ya Baraza lake na kupunguza ukubwa wake.
Kuhusu rushwa, Rais Kikwete amejitahidi sana kuijengea uwezo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Si siri kwamba chombo hicho hivi sasa kina nyenzo za kufanya kazi vizuri kuliko ilivyokuwa enzi za utawala wa serikali zilizopita.
Lakini kukipa nyenzo chombo hicho pekee yake hakutoshi, wananchi wanaona bado tuhuma za vigogo kujihusisha na rushwa bado zinakaliwa.
Katika hotuba zake nyingi hasa anapozungumza na Watanzania, Rais Kikwete hutamka maneno mazito dhidi ya namna atakavyopambana na rushwa, lakini baadhi ya watendaji katika vyombo husika hajawashawishi Watanzania wakaridhika na kasi yake ya uchukuaji wa hatua kwa vigogo wanaotajwa kuhusika na vitendo vya rushwa.
Penye ufisadi, hakuna haki. Pasipo na haki, hakuna amani. Na pasipo na amani, hakuna maendeleo, hivyo kwa kushughulikia polepole masuala ya mafisadi ni sawa na kuendelea kufuga ufisadi serikalini ambao ni maadui wakubwa wa taifa hili.
Kwa mfano, baadhi ya mawaziri mpaka sasa, bado wanaandamwa na tuhuma nzito za ufisadi, na wengine wametajwa kwa majina hadharani, lakini vyombo vinavyohusika ikiwemo Takukuru vimekuwa na kasi ndogo ya kuchukua hatua.
Mbali ya ufisadi kufunika anga la siasa nchini, upande mwingine mambo mengine yakiwamo ya kilimo, yanakwenda vizuri.
Rais Kikwete ameingia na kasi ya Kilimo Kwanza. Ukweli katika ngazi ya rais, kilimo kwanza kimekwenda vizuri, kilichobaki ni utekelezaji katika halmashauri na wilaya.
Kuimarika kwa mikakati ya kilimo, kumemfanya Rais Kikwete sasa aanze kuelekeza nguvu kwenye sekta ya mifugo.
Sekta hiyo ambayo iliipa uzito wa aina yake kwa kuiundia Wizara (Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) imekuza kwa kiasi kikubwa ufugaji na uvuvi.
Katika kuhimiza sekta ya mifugo, ambayo yeye mwenyewe ni mdau kama mfugaji kule Bagamoyo, amepita kukagua mashamba mbalimbali ya mifugo mkoani Iringa na kuona mafanikio na changamoto zilizopo.
Kilimo Kwanza, kimeanza pamoja na kampeni za kuhakikisha halmashauri zinakuwa na matrekta ya kukodisha wakulima wadogo ili waachane na jembe la mkono, lakini pia ameimarisha mfumo wa upatikanaji pembejeo kwa kuanza kutumia vocha na stakabadhi ghalani ili kutowanyosha wakulima jasho lao.
Jitihada zinafanyika hata kama kasi katika baadhi ya maeneo ni ndogo. Kuhusu elimu, Rais Kikwete amezoa sifa tele, kuanzia kwenye shule za awali hadi ujenzi wa Chuo Kikuu Dodoma (Udom) ambacho kitakuwa kikubwa zaidi Afrika Mashariki.
Watanzania wanakubaliana na kasi hiyo, wanajua matunda yake si ya mwaka kesho au keshokutwa, ya karne.
Mbegu anayoipanda itachelewa kutoa matunda katika elimu, lakini ipo siku itatoa matunda yatakayokuwa kumbukumbu ya karne.
Katika sekta hiyo kilio cha wananchi kimebaki kwenye miundombinu ya kuboresha elimu hiyo, hasa uhaba wa walimu, nyumba za walimu, vifaa vya maabara na zana nyingine muhimu katika kutoa elimu bora wala si bora elimu.
Kampeni ya Rais imeelekezwa katika kujenga zahanati katika kila kijiji kilicho umbali wa kilometa tano kutoka ilipo nyingine, lakini pia kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya, wilaya inakuwa na hospitali na mkoa unakuwa na hospitali ya rufaa.
Hospitali za kanda za rufaa za kanda na taifa zifanya kazi hiyo si kutibu mafua. Upande mwingine ambao umeonekana katika kipindi cha miaka minne ni kuhusu vyama vya akiba na mikopo.
Kikwete ameimarisha Saccos, kwanza alianza kwa kasi ya kuingiza mabilioni, yaliyojulikana, Mabilioni ya Kikwete.
Pamoja na nia nzuri ya kuwajaza mapesa Watanzania, bado kuliingia urasimu wa ajabu kuanzia kwenye benki hadi kwa wale waliopewa dhamana ya kuchagua wakopaji mikopo hiyo.
Walijipendelea, wakajikopesha na kujinufaisha, hivyo walio wengi wakabaki na kiu ya mapesa na umaskini ukazidi kuwakaba.
Wakati anaingia madarakani miaka minne iliyopota, ilikadiriwa kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitano, kutakuwa na maambukizi mapya ya Ukimwi kwa zaidi ya watu 1,000,000 na vifo 500,000, lakini kwa kazi ambayo serikali yake imefanya katika kipindi cha miaka minne tu takwimu hizo zitashuka.
Lakini mafanikio makubwa ambayo Rais Kikwete ameyapata katika kipindi cha miaka minne ni namna alivyoiendesha kampeni dhidi ya Ukimwi.
Ukimwi ni tatizo kubwa katika nchi yetu na Rais ameonesha kutambua hilo. Hatua ya Rais Kikwete kuanzisha kampeni ya kitaifa ya kupima Ukimwi kwa hiari na yeye na mkewe Salma kuwa watu wa kwanza kupima Ukimwi hadharani, ilikuwa ni changamoto chanya.
Hata hivyo hali ya kipato cha wananchi bado ipo chini, umasikini unatesa mamilioni ya Watanzania. Zaidi ya asilimia 54 ya Watanzania ni masikini, na kati yao asilimia 18.7 ni masikini wa kutupwa ambao hawana hakika hata ya mlo mmoja kwa siku.
Hali hiyo inabaki kuwa changamoto katika kipindi kinachobaki. Mkakati wa serikali wa kuhifadhi mazingira na kutunza vyanzo vya maji, ilioutangaza Aprili mosi, mwaka 2006, kwa hakika, umeleta matunda mazuri.
Ardhioevu ya Ihefu, Mbarali na unakoanzia mto mkuu wa Ruaha kwenye mpango wa milima Livingstone, na mahali pengine nchini, imejirudia hali yake ya zamani kwa kasi, maji yameongezeka na uoto wa asili umetanda kila mahali.
Rais Kikwete anapenda michezo, hatasahauliwa katika kuimarisha, kudumisha na kuendeleza michezo, licha ya kumtafuta kocha wa kuinoa timu ya Taifa (Taifa Stars) Marcio Maximo, lakini pia amekuwa akimlipia kocha kwa muda wote. Wakati mwingine amekuwa akikemea vitendo vinavyoharibu sura ya nchi katika michezo. Mikakati hiyo
ya maendeleo inayosimamiwa na Rais Kikwete imeleta matokeo mazuri baada ya Taasisi ya Utafiti wa Demokrasia Tanzania (REDET) kuonesha kwamba, licha ya kasoro za hapa na pale zinazoiandama serikali ya awamu ya nne,
lakini bado Watanzania wana imani na Rais Kikwete ingawa hawana imani na serikali yake. Sekta na idara zilizotajwa hapo juu ni chache kati ya nyingi ambazo amezifanya vizuri katika utendaji wake hata kama kumekuwa na dosari ndogo ndogo, serikali ya awamu ya nne inayo ya kujivunia.
Hayo ni miongoni mwa mambo mengi ya kujivunia ya Rais Kikwete, ambaye leo ametimiza miaka minne akiwa Ikulu.
Ni ukweli kwamba machoni mwa Watanzania Rais Kikwete anaaminika, taasisi za kimataifa zinamuheshimu, kazi kwao watendaji wake ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taifa la Tanzania.
http://www.habarileo.co.tz/makala/?n=4931