Tundu Lissu ni mwenyekiti wa Chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) ambaye kwa sasa anakabiliwa na makosa ya uhaini na uchochezi. Tarehe 09 Aprili, 2025 Lissu
alikamatwa na jeshi la polisi mara baada ya mkutano wa hadhara alioufanya Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma na kusafirishwa hadi Dar es Salaam.
Kuelekea uchaguzi mkuu wa CHADEMA uliofanyika mwezi Januari 21, 2025 alipokuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti, Lissu alihojiwa kupitia kipindi cha 'One on one With Charles William' cha Wasafi TV ambapo mahojiano hayo yalichapishwa katika mtandao wa
YouTube mnamo Januari 13, 2025. Pamoja na mambo mengine Lissu alitumia nafasi hiyo kueleza kwanini alifikiri anastahili kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho.
Katika mtandao wa
TikTok ipo video inayosambazwa ikimuonesha Lissu akiulizwa swali
"Wenzako wanasema unataka uanzishe maandamano yatakayozua vurugu badae ukimbilie nje ya nchi kwa sababu hata familia yako umeiacha huko hapa ni kama upo na begi lako tu tayari kwa kuondoka kama hali ikichafuka?" ambapo anaonekana Lissu akijibu kwa kusema
"Wanangu wako marekani, wanasoma, wanakula bata mimi niko hapa twendeni kwenye mapambano, watu wapigane ngumi (anaulizwa na mtangazaji, '
ndivyo unavyomaanisha?'), anajibu,
na hiyo ni dhambi kiasi gani?"
Je, ni kweli Lissu alitoa majibu hayo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia utafutaji wa maneno muhimu, pamoja na marejeo ya video, umejiridhisha kuwa video hiyo imepotoshwa uhalisia wake kwa kukata na kuunganisha vipande visivyohusiana kutoka kwenye Video ya mahojiano ya Tundu Lissu na Charles William.
Katika
video halisi alipoulizwa kuhusu maandamano na uwepo wa familia yake nje ya nchi Lissu, alisema mke wake na watoto wake waliopo nchini Marekani wamekataa kurudi Tanzania kutokana na tukio la kushambuliwa lililomtokea.
"Hapa ni nyumbani kwangu, nimekaa hapa miaka 27, huu ni mwaka wa 28, nilienda nje nikiwa nusu mfu. Nilipoondoka mara ya pili, watu wanajisahaulisha tu kwamba ilishatoka amri ya Magufuli nishughulikiwe. Ukifa safari yako ya duniani imeisha, kama ulikuwa ulikuwa unapambana mwisho wa mapambano yako ndiyo huo.
"Ukiishi unaweza kupambana siku ya pili. Mke wangu anasema hivi, 'baada ya risasi zote zilizokupiga wewe, mimi sina amani tena na hio nchi' Nani anaeweza kumlaumu huyu mama. Wanangu wanasema hivi, 'Baba tupokuja hospitali Nairobi ulikuwa na sura ya maiti' nani anaeweza kuwalaumu hawa watoto. Nani ambae amepitishwa walikopitishwa wao, anaeweza kuwalaumu kwamba wanakula bata ulaya na Marekani, wanangu wako Marekani wanasoma"
Rejea hapa kuanzia
dakika ya 39
View: https://youtu.be/6DfBsIaGJlA?si=qffJxpLCa1bOr8De&t=2368