No reform no election ni ajenda ya Chama cha demokrasia na maendeleo yenye lengo la kuhamasisha mabadiliko kabla ya kufanya uchaguzi mkuu 2025. Ajenda hiyo imekuwa na mapendekezo mbalimbali yanayopaswa kufanyika ili kuwe na uchaguzi huru na wazi.
Machi 02, 2025
CHADEMA chini ya mwenyekiti wake
Tundu Lissu ilifanya
mkutano na Jukwaa la wahariri Tanzania (
TEF) chini ya mwenyekiti wao Deodatus Balile, ajenda ya mkutano huo ikiwa ni kujadili suala ama ajenda ya No reform no election ya CHADEMA.
Madai
Kumekuwepo na grafiki zinazonesha picha ya mwenyekiti wa CHADEMA, Lissu ikiambatana na maneno
‘TUMESITISHA RASMI MSIMAMO WETU WA ‘NO REFORM NO ELECTION’, tazama hapa, nyingine ikiwa imeandikwa
“LISSU: MSIMAMO WA ‘NO REFORM NO ELECTION’ UMEFELI HIVYO TUMEAMUA KUACHANA NAO KWA SASA”
Uhalisia wa madai hayo
JamiiCheck imefuatilia madai hayo kwa njia ya mtandao ikiwemo kufuatilia mjadala mzima uliokuwa ukirushwa na chaneli mbalimbali za
youtube na kubaini kuwa
si ya kweli, Lissu hakusema maneno hayo.
Katika mkutano huo Lissu alieleza kuwa ni lazima mabadiliko yafanyike kabla ya kuendelea na uchaguzi na akasema kuwa atahakikisha kama mabadiliko hayatofanyika basi watazuia uchaguzi. Lissu alisema kua;
"Mheshimiwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, lugha yangu ilikuwa bayana kabisa, tumesema siyo hatutasusia uchaguzi, tutazuia uchaguzi, lugha siyo kususia uchaguzi lugha ni kuzuia uchaguzi, na tumesema tutazuia uchaguzi kwa nguvu ya umma, tutawaalika Watanzania wahakikishe uchaguzi huu haufanyiki. Bila mabadiliko hakuna uchaguzi na siyo bila mabadiliko hatutashiriki uchaguzi, hiyo siyo lugha yetu, lugha yetu ni bila mabadiliko uchaguzi hautafanyika, ndiyo lengo letu"- Lissu.
Aidha grafiki zinazoonekana kutumika moja ikionekana ya MillardAyo na nyingine Jambo Tv ni za kuhaririwa na taarifa hizo hazijachapishwa na kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya vyombo hivyo.