Kampuni ya Afritainer ilifanikiwa kuchota zaidi ya Shilingi bilioni 12 za EPA kwa kutumia nyaraka zilizosainiwa na watumishi wa kampuni moja maarufu ya Dar es Salaam
(jina tunalo) wakidaiwa kuwa wakurugenzi wa kampuni hiyo kabla ya kufahamika kwamba hawakuwa wakurugenzi halali kisheria.
Kagoda, ambayo ilitumia nyaraka za kughushi, ilichotewa mabilioni hayo ya fedha kabla haijasajiliwa na katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Hadi sasa hakuna taarifa rasmi zinazoonyesha watu waliorejesha fedha za EPA kwa jina la Kagoda pamoja na kuwapo taarifa za uhakika kuhusiana na wafanyabiashara wazito waliorejesha fedha hizo kwa nyakati tofauti kabla ya muda uliowekwa kwisha Oktoba 31, 2008.
Nyaraka zilizotumiwa na Afritainer kuchota mabilioni ya fedha za EPA mwaka 2000 zinaonyesha kwamba kampuni hiyo imetumia n
amba za simu 2861371 na 2861372 ambazo pia ndizo zimetumiwa na Kagoda katika kuchota fedha za EPA mwaka 2005. Namba hizo zinaonekana katika nyaraka za kampuni nyingine yenye uhusiano na wamiliki wa Afritainer.
Nyaraka kutoka Wakala wa Usajili wa Makampuni na Leseni (BRELA) zinaonyesha kwamba
Tabu Omari Masula na Barati A. Goda, walidaiwa kuingizwa kuwa wakurugenzi wa kampuni hiyo Mei 15, 2000 kinyume cha sheria.
Barua ya BRELA ya Februarin 18, 2002, miaka miwili baada ya Tabu na Barati kuchota fedha za EPA, ilieleza kwamba wakurugenzi hao hawakuwa halali kutokana na kutokuwa na hisa katika kampuni ya Afritainer.
Kwa mujibu wa barua hiyo kwenda kwa kampuni ya mawakili ya M.A.Imail, Tabu na Barati walikiuka kifungu cha 50 cha hati ya usajili ya kampuni hiyo kinachomlazimu mkurugenzi kuwa na hisa katika kampuni kwanza ili aweze kuwa na maamuzi.
Waraka wa Afritainer uliowasilishwa BRELA Mei 15, 2000, ulieleza kwamba wakurugenzi pekee na waazilishi wa Afritainer ni
Bahram Abdurasul Chakaar na Gulam Abdurasul Chakaar, wamejiuzulu ukurugenzi na kuwaachia Tabu na Barat.
Hata hivyo, BRELA katika barua ya Februari 18, 2002 iliyoandikwa na Msajili Msaidizi wa wakala huo, L. Kimaro, ilieleza wazi kwamba hadi wakati huo ubadilishaji wa wakurugenzi haukuwa umeidhinishwa kutokana na kutokufuata masharti ya usajili.
Tabu anatajwa kufanya kazi katika kampuni moja ya jijini Dar es Salaam yenye ofisi zake eneo la viwanda barabara ya Nyerere na Upanga.
Kwa mujibu wa habari ambazo Raia Mwema imezipata fedha hizo kiasi cha Sh. Bilioni 13 zilichukuliwa Agosti 2000 kabla ya uchaguzi wa pili wa vyama vingi ambao Benjamin Mkapa aligombea tena urais.