Na Saed Kubenea
MwanaHALISI~Maslahi ya Taifa Mbele
MBUNGE wa Mtera, mkoani Dodoma, makamu mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu (CC), John Samwel Malecela ameibuka na kusema chama chake hakitishiwi na kundi la viongozi wa chama hicho wanaotaka kujimega.
Amesema, Wanaotaka kumeguka waondoke haraka. Wasitutishe. Amesema CCM ni imara, hakiwezi kuyumbishwa na kundi la watu wachache na kwamba kamwe chama hakitakabidhiwa kwa matajiri kwa kuwa chama hicho ni cha wanyonge.
Hiyo ilikuwa wiki iliyopita alipoongea na waandishi wa habari Dar es Salaam.
Hiki ni chama cha wanyonge. Ni chama cha wakulima na wafanyakazi na kitaendelea kubaki hivyo, alisema.
Alitishia kwa kutoa mfano kuwa CCM ilishawahi kufukuza viongozi wake mbalimbali na bado ikabaki imara.
Alisema akina Wilfred Mwakitwange, Chogga na Fotunatus Masha walifukuzwa wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere lakini chama kilibaki imara.
Malecela alisema wanaotishia kuondoka CCM wanatumia kauli ya Baba wa Taifa, kwamba upinzani imara utatokana na kumeguka kwa CCM.
Huwezi kusema baba wa taifa (Nyerere) alitaka CCM imeguke ili kuleta upinzani imara. Mbona kuna mengi ambayo Mwalimu aliyasema lakini hayajachukuliwi kama kigezo? alihoji.
Malecela hakutaja aliowalenga. Lakini kauli yake ililenga kurudisha moyo kwa wale waliokuwa wakidhani chama kinameguka kutokana na malumbano miongoni mwa wabunge na viongozi wengine ndani ya chama.
Katika siku za karibuni, CCM kimekuwa kikikabiliwa na tuhuma lukuki, ikiwamo chama kukabidhiwa matajiri hasa wale wenye tuhuma za kushiriki katika vitendo vya ufisadi.
Kumekuwa na madai kuwa uongozi ndani ya CCM hautokani na sifa za mwanachama katika kukitumikia chama, uadilifu na uaminifu wake katika jamii, bali unatokana na jinsi anavyotoa fedha na kiwango kinachotolewa.
Uchaguzi mkuu ndani ya chama hicho uliokamilika mwaka jana, ulilalamikiwa kwa matumizi ya fedha kuanzia ngazi ya nchini ya uongozi hadi ya juu.
Ndani na nje ya CCM si siri tena kusikia kuwa uaminifu na uadilifu vimetoweka. Vigezo vya iwapo mtu alikuwa mwanamtandao au mpinzani wa mtandao, navyo vimekidhoofisha chama kwa kuleta mgawanyiko.
Sasa swali kubwa ambalo baadhi ya wananchi wanajiuliza ni: Je, Malecela ametumwa na nani kusema haya aliyoyasema?
Hii haina maana kwamba Malecela hana uwezo wa kutoa kauli za aina hiyo. Wala hahitaji msaada ili afikiri na kusema hivyo. Lakini kwa muda aliposemea na kumbushio la historia ya kilichowahi kutokea ndani ya chama, inaonekana kuna uzito nyuma ya kauli yake.
Kitu kingine ni kwamba Malecela, na siyo Kingunge Ngombale-Mwiru, ndiye anaonya dhidi ya wenye fedha kumiliki chama. Hili nalo linaleta nuru mpya katika mazingira ya sasa.
Kwa kuzingatia ambayo yamekuwa yakitendeka, kauli ya Malecela inaleta sura mpya: Je, CCM imo mbioni kuzaliwa upya? Hapa ndipo wengi wanajiuliza iwapo Malecela amesimama peke yake katika hili au yuko sambamba na Kikwete.
Rais Kikwete amekuwa mkimya mno kuhusu kinachoendelea ndani ya serikali na ndani ya chama. Inadhihirika sasa kuwa anatumia mtindo wa Acha wanyukane kwanza, nitawaamua baadaye.
Wachunguzi wa mambo wanasema ukimya wa Kikwete unalenga kumpa muda wa kuona nani yuko upande wake na nani mpinzani wake. Lakini ni ukimya huu unaoweza kukifikisha chama katika kumeguka huku viongozi wakichelea kutoa maamuzi.
Kujitokeza kwa Malecela, kutishia wanaotishia kuhama chama na hata matajiri ambao kwa muda sasa wamekuwa wakisema wamekiweka chama kiganjani, haliwezi kuwa tukio la kawaida tu.
Ni kweli, Malecela amekuwa Tingatinga la CCM kwa miaka mingi; akikata mbuga kurejesha majimbo ya chama chake yaliyochukuliwa na upinzani.
Pale ambapo tingatinga halikufika, hasa katika uchaguzi mdogo, CCM ama ilipata wakati mgumu kushinda au ilishindwa. Lakini katika miaka miwili ya utawala wa Kikwete, naye amekuwa mkimya.
Wengi wanasema hataki kuonekana ana uchu wa kurejea kwenye ulingo mkuu wa siasa. Hili nalo linaweza kuwa kweli, ingawa ni yeye anayesema mara kwa mara kuwa ubunge wake wa Mtera, Dodoma unatosha.
Kama hivyo ndivyo, uchungu wa kutoa kauli kama aliyotoa wiki iliyopita, unatoka wapi? Ni hapa kauli yake inahusishwa na Kikwete na ikiwa maandalizi tu ya kitakachofuata.
Malecela anaonekana kutolea macho wale wanaoitwa mabingwa wa mizengwe. Wale wanaohusishwa na tuhuma mbalimbali; wanaolalamika kuwa Kikwete ametutosa.
Kiongozi huyo wa muda mrefu atakuwa anawatunga kidole jichoni wale wanaotuhumiwa kutaka kumzuia Kikwete katika uchaguzi ujao na wale wanaopanga kumhusisha na kashifa za ufisadi.
Kwa mfano, ni kauli ya Malecela kwamba, anayetaka kumpinga Kikwete 2010 anajisumbua na kwamba CCM hakiwezi kukabidhiwa kwa watu wenye fedha.
Kulenga au kutolenga mtu, kauli ya Maleclela inastahili pia kupimwa kwa mujibu wa wakati.
Anaposema kuna baadhi ya wanachama waliwahi kufukuzwa na chama hakikutetereka, hakika ni miaka mingi iliyopita.
Ni wakati Nyerere akiwa usukani. Wakati huo kulikuwa na ubishi wa chinichini na wachache walidiriki kutoa kauli waziwazi.
Hizo zilikuwa nyakati za mfumo wa chama kimoja. Zilikuwa pia nyakati za zidumu fikra za mwenyekiti. Uhuru wa kujieleza ndani ya chama kimoja ulikuwa finyu isipokuwa ulipokuwa na hoja kusimamia au kuboresha hoja kuu ya chama.
Aidha, hakukuwa na mahali pa kukimbilia. Nani ambaye hajasikia viongozi wa serikali na CCM wakisema kwamba walifanya makosa kumpoteza Dk. Willibrod Slaa alipokuwa anataka kugombea CCM na hivyo akaamua kuhamia upinzani.
Wale ambao ni woga wa hoja wanasema wangekuwa naye katika chama chao huenda asingekuwa anaibua hoja kali na ushahidi usiopingika dhidi ya CCM.
Lakini sasa Malecela anatishia wale ambao wanadai wanataka kuhama na wale ambao wanataka kuzuia Kikwete kugombea mwaka 2010. Hata hivyo, bado wana mahali pa kukimbilia.
Bali ujumbe umetumwa na umefika. Katika kauli yake, Malecela amesimama na Kikwete; liwake jua au inyeshe mvua.
Kauli ya Malecela inalenga kuonyesha kuwa karibu Kikwete atakunjua makucha. Nani asiyesubiri wakati huo? Yawezekana Kikwete sasa ameamua kufumba macho na kusema liwalo na liwe na Malecela ni ngazi.