KLHN International
Watumishi wawili wa Benki Kuu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar wakikaribiwa na mashtaka mbalimbali ambayo ni pamoja na kutumia madarka vibaya na kusababishia hasara serikali ya zaidi ya Shilingi Bilioni 220. Watumishi hao Bw. Joachim Liumba ambaye ni Mkuu wa Utawala na Utumishi wa Benki hiyo na Deogratias Kweka ambaye ni Meneja Miradi walitakiwa kuwa na dhamana ya kiasi nusu ya kile kinachodaiwa. Wameshindwa dhamana na sasa wamepelekwa Keko wakisubiri kesi yao kutajwa tena.
Kesi hiyo inayowakabili inahusu ujenzi wa ziada wa majengo ya Minara Pacha ya Benki Kuu ambayo imedaiwa kwa muda mrefu kuwa imetumia kiasi kikubwa cha fedha ambapo ujenzi wa Minara hiyo hadi sasa umegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 300 na kufanya majengo hayo kuwezekana kuwa ni yenye gharama kubwa zaidi katika Afrika ukilinganisha na ukubwa wake na sehemu ya soko.
Mradi wa minara miwili ya Benki Kuu unaigharimu Tanzania Dola 8625 kwa kila mita ya mraba ambapo gharama ya mita kama hiyo sehemu nyingine Tanzania (na Jijini Dar hususan) ni dola 700. Ujenzi wa aina hiyo kwenye majiji ya New York (Marekani) na Tokyo (Japan) haizidi dola 3000 na vyumba hivyo vinakuja vikiwa na samani.
Majengo hayo ambayo yana mita za mraba 40,000 kama yangegharimiwa kwa kutumia viwango vya New York yasingezidi dola milioni 120. Na hapa tunajumlisha gharama za vikolombwezo vyote vikiwemo vifaa vya usalama, teknolojia nyingine, kusimamia dhahabu n.k
Bodi ya Wahandishi wa Tanzania, Bodi ya Wasanifu Majengo, na Bodi ya Wakandarasi zote zilipinga gharama na mchakato mzima wa ujenzi wa majengo hayo lakini serikali ya CCM iliamua kuendelea nayo. Hadi kifo chake Gav. Ballali aliweza kutumia zaidi ya dola milioni 345 katika ujenzi ambao hadi hivi sasa haujakamilika.
Licha ya tuhuma kuwa kuwa Gav. Ballali alipokea rushwa/hongo ya karibu dola milioni 5 serikali haikumchunguza na kumuacha aendelee na mpango huo baada ya kampuni ya Sanska ya Uswedi kuondolewa. Gav. Balali aliendelea kwa kuajili kampuni ya Group 5. Tatizo ni kuwa Group 5 ni kampuni tanzu ya Sanska. Kwa maneno mengine walinyang'anywa kwa mkono huu wakapewa kwa mkono mwingine.
Gharama ya hasara kwa Tanzania ni karibu dola milioni 265 ambazo zinaonekana leo kwenye mashtaka dhidi ya kina Liumba. Mashtaka haya dhidi ya kina Liumba ni wazi ni katika kutekeleza ahadi aliyoitoa Gavana Benno Ndulu karibu miezi mitatu hivi iliyopita ambapo alisema kuwa Benki Kuu imeajiri makampuni ya kimataifa kufanya ukaguzi wa gharama halisi za majengo hayo.
Kampuni ya M/S Mekon ARC ya nchini ilipewa jukumu hilo ikishirikiana na kampuni ya AQE Associates na Bureau for Industries ltd. "Tunataka kujua kama fedha tulizotumia zinalingana na thamani ya majengo haya au la......tuliahidi kuwa tutakagua mahesabu ya ujenzi wa majengo haya na sasa ndiyo tumeanza" Alisema Gavana Ndulu aliyechukua nafasi hiyo kufuatia kifo cha Gavana Ballali.
Mashtaka haya dhidi ya kina Liumba yanatishia watumishi wengine wa serikali ya awamu ya tatu ambao walisimama kutetea ujenzi wa majengo hayo wakiwa Bungeni na ambao bila ya shaka maamuzi yao ndiyo yamechukuliwa kuwa ni baraka za ujenzi huo. Aliyekuwa Waziri wa Fedha Bi. Zakhia Meghji alizungumza wakati wa kufunga mjadala wa Wizara yake mwaka 2006 na kutetea ujenzi wa majengo hayo.
Hata hivyo Waziri Meghji alikumbana na wakati mgumu alipobanwa na Mbunge wa Tabora Mjini Mhe. Siraju Kaboyonga (CCM) ambaye aliuliza "Nafikiri waziri hajajua swali langu, nasema hivi, mtaji wa BoT ni sh bilioni 20, lakini thamani ya majengo yake, haiendani na mtaji huo, fedha hizo za ujenzi zimetoka wapi" Waziri Meghji alionekana kubabaika wazi hadi alipoweza kuokolewa na Naibu Spika Mhe. Anna Makinda.
Hata katika kikao cha bajeti cha 2007 kiongozi wa upinzani Bungeni Mhe. Hamad Rashid Mohamed naye alihoji juu ya ujenzi wa majengo hayo.
Gavana Ballali mwenyewe alijitetea mwaka 2007 Julai na kuelezea kuwa madai ya kutumia fedha zaidi kwenye ujenzi wa majengo ya Benki Kuu ilikuwa ni mwendelezo wa tuhuma dhidi ya magavana wa Benki Kuu na yeye hakuwa wa kwanza. "Gavana Charles Nyirabu (marehemu) alikuwa na mpango wa kupanua jengo la BoT, alikumbwa na kashfa kama ya sasa.
"Alivyokuja Gilman Rutihinda, naye alipanua sehemu ya jengo tunalolitumia sasa, naye aliibuliwa kashfa, akaacha na alipokuja Gavana Idrisa Rashid, akaendeleza ujenzi huo naye alikumbwa na kashfa hiyo hiyo na mimi nilivyoingia mwaka 2000 na baadaye kuanza ujenzi wa ‘Twin Tower', maneno yameibuka tena" alisema Gav. Ballali ambaye baada ya sakata la EPA kuibuka alitoweka nchini kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kufuata matibabu huko Marekani katika hospitali isiyojulikana. Alitangazwa kuwa amefariki dunia muda si mrefu tangu ombi langu la kujiuzulu kukataliwa na Rais. Alifukuzwa kazi na Rais wakati akitangaza kuundwa kwa timu maalumu ya uchunguzi wa EPA .
Wachunguzi wa mambo ya kisheria nchini wanaangalia kama watendaji wajuu wa wizara nao watafikishwa mahakamani kama walivyofikishwa Bw. Basil Mramba na Daniel Yona ambao nao kutokana na nyadhifa zao wanatuhumiwa kuzembea na kufanya maamuzi ambayo yamelisababishia taifa hasara kubwa. Kiasi kinachodaiwa katika suala la majengo pacha ya Benki Kuu ni mara 22 zaidi ya kile kinachodaiwa katika kesi ya kina Mramba na Yona.