Nyerere alikuwa binadamu kama binadamu yeyote yule, alikuwa na mapungufu mengi na muda mwingine unaweza ukasema 'aaa hata hili nalo'. Ukimsikia kamara Kasupa, Kamaliza, Bibi Titi na wengineo wengi hasa waliokuwa wapigania uhuru na haki kupitia vyama vya wafanyakazi utaona dhahiri kuwa Nyerere alikuwa na mapungufu na kwa hakika kabisa aliyoyafanya kunyamazisha vyama vya kiraia yana athari katika uhuru binafsi wa mawazo na ushiriki wa wananchi mpaka leo hii. Kipi cha maana katika hayo mapungufu ya Nyerere? La maana ni kuwa misingi aliyoiacha Nyerere inaumiza na kuwanyima haki watu wengine mpaka leo hii aidha kwa kuendelezwa kwa baadhi ya udhalimu aliouacha ama kunyang'anywa haki kulikofanyika kwa watu hao. Sasa sisi yatupasa kutumia hayo kama darasa la kujifunza ili makosa yasije yakarudiwa. Tutajifunza vizuri zaidi kwa kusema ukweli wote, wote kabisa hata kama itaonekana sehemu fulani Nyerere alidanganya kwa kinachosemekana ni maslahi ya taifa kwa wakati huo, tuseme hapa Nyerere alisema uongo, tuutafute ukweli. Hatuwezi kujifunza kwa uongo kwa vile tu ulisemwa au ulisababishwa na Nyerere. Nyerere naye alikuwa binadamu kusema uongo ni sehemu ya ubanadamu huo!