A
Anonymous
Guest
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 20(1) inasema, “Kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.”
Hata hivyo, baadhi ya walimu nchini wamelalamika kulazimishwa kujiunga na Chama cha Walimu Tanzania.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 9 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6/2004 Wafanyakazi wanayo haki ya kujiunga na chama chochote cha Wafanyakazi au kuanzisha Chama cha Wafanyakazi kwa kuzingatia matakwa yaliyowekwa katika Kifungu cha 46 na 47 cha Sheria hiyo.
Malalamiko ya walimu
Walimu Wanachama wa Chama cha Kutetea Haki na Maslahi ya Walimu Tanzania (CHAKAMWATA) wamelalamikia kitendo cha baadhi ya Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari wanaohamia kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kuzuiliwa kujiunga na chama hicho ambacho kipo kwa mujibu wa sheria.
Wanao tuhumiwa kuwazuia walimu hao ni wakurugenzi, maofisa utumishi wakuu na maofisa utumishi wasaidizi wa halmashauri nchini.
Walimu hao wanadai kuwa licha ya kujiunga na CHAKAMWATA kwa kufuata hatua zote za kisheria, maofisa hao wanaoingia kwenye mfumo wa mishahara yao (LAWSON) wamekuwa wakikataa kuwaunga CHAKAMWATA walikojiunga na badala yake wanawalazimisha wabaki CWT walikojitoa.
Maofisa hao wanadaiwa kukataa kuondoa makato ya asilimia 2 ya CWT na kuingiza michango ya asilimia 1 ya CHAKAMWATA kwenye mishahara ya walimu wanaojitoa kutoka CWT na kujiunga na CHAKAMWATA.
Uchunguzi umebaini kuwepo kwa walimu wapatao 881 wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya wanamlalamikia Mkurugenzi wao kuwa ameyashikilia majina yao kwa zaidi ya mwaka mmoja na mkurugenzi huyo amewazuia wasiondolewe CWT wala wasiingizwe CHAKAMWATA tangu mwaka 2025 licha ya walimu hao kukamilisha taratibu zote zinazohitajika kisheria.
Wamedai kuwa malalamiko yao yapo kuanzia Machi 2025, muda ambao Mkurugenzi Justice Kijazi amekuwepo ofisini.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, walimu wa shule za msingi na sekondari wanamlalamikia Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Ofisa Utumishi Mkuu pamoja na Afisa Utumishi Mkuu Msaidizi kwa kukataa kutekeleza maelekezo yao ya kuondoa makato ya CWT na kuingiza michango ya CHAKAMWATA kwenye mishahara yao baada ya kukamilisha hatua zote za kisheria.
Mwandishi wetu alifanikiwa kupata barua ya mmoja wa walimu waliokataliwa kuhamishwa kutoka CWT kwenda CHAKAMWATA.
Barua hiyo iliyosainiwa na Fatuma Mabira yenye kumbukumbu namba TDC/PF. 1541/119 ya tarehe 05/11/2025, akimjibu Mwalimu Shabani Ahmadi Napachihi wa Shule ya Msingi Mji Mpya kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, amekataa kumwondoa Mwalimu huyo kutoka CWT alikojitoa na kumpeleka CHAKAMWATA alikojiunga kwa hiari yake na kwamba kwenye Wilaya yake ya Tandahimba Chama halali cha Walimu ni CWT tu.
Barua hiyo yenye kumbukumbu namba J. A. 25/414/02/30 ya tarehe 16 Juni 2025 ilikuwa ikimjibu Mwenyekiti wa CHAKAMWATA wa wilaya hiyo kuwa amekataa kuwaondoa CWT na kufuta makato ya 2% ya CWT kwenye mishahara ya Walimu wote waliohama CWT na kujiunga na CHAKAMWATA na kwamba amekataa kuingiza michango ya asilimia 1 ya CHAKAMWATA kwenye mishahara ya walimu hao.
Madai ya Mkurugenzi huyo kuhusu msimamo wake kwa mujibu wa barua hiyo ya Mwenyekiti wa CHAKAMWATA wa Wilaya ya Tandahimba ni kuwa hayo ni maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi kupitia Waraka namba 1/2022 wa Msajili wenye kumbukumbu namba DA. 76/380/01/67 wa Juni 7, 2022, kuwa CHAKAMWATA hakina sifa za kufanyakazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.
Madai ya Mkurugenzi huyo yanafanana na madai ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Dk Fredrick Sagamiko ambaye kupitia barua yenye kumbukumbu namba HA. 27/294/02/02 ya Mei 19, 2025, akimjibu Mratibu wa CHAKAMWATA Mkoa wa Dodoma.
Katika barua hiyo mkurugenzi huyo alikataa kuondoa makato ya asilimia 2 ya CWT ili kuingiza michango ya asilimia 1 ya CHAKAMWATA kwenye mishahara ya Walimu 78 waliokuwa wamejitoa kutoka CWT na kujiunga CHAKAMWATA.
Mkurugenzi huyo kwenye barua yake anasema hayo ni maagizo kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi nchini kupitia Waraka wa Msajili namba 1/2022.
Taarifa zaidi zinasema kuwa unaodaiwa kuwa ni Waraka wa Msajili namba 1/2022 uliandikwa kwenda kwa Makatibu wakuu wa Vyama vya Wafanyakazi na wala siyo kwenda kwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya.
Hata hivyo, zipo taarifa kuwa waraka huo unaodaiwa kutolewa na Msajili unapingana na Sheria ya vyama vya Wafanyakazi na inadaiwa ulilenga kukibeba CWT dhidi ya CHAKAMWATA.
Soma pia:
Hujuma dhidi ya CHAKAMWATA
Kuna madai kuwa Msajili huyo wa vyama vya Wafanyakazi aliwahi kukipiga marufuku CHAKAMWATA na baadaye akakifuta kutoka kwenye rejista ya yama vya wafanyakazi nchini wakati anajua fika kuwa sheria haiimpi mamlaka ya moja kwa moja kufanya hivyo dhidi ya Vyama vya Wafanyakazi.
Baadaye Msajili alifungua kesi namba 13 ya mwaka 2022 ya kutaka CHAKAMWATA kifutwe ambapo kilifutwa.
CHAKAMWATA ilipingana na uamuzi huo hivyo, ilikata rufaa katika kesi namba 170 ya mwaka 2023 na hatimaye ikashinda na kurejeshewa usajili wake na Mahakama ya Rufani Februari 27, 2025.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro madai yaliyotolewa na walimu waliohamia CHAKAMWATA yanafana na madai ya Halmashauri nyingine ya kuzuiwa kujitoa CWT ambapo walimu 200 wamezuiwa.
Katika halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe walimu waliohamia CHAKAMWATA wamekuwa na malalamiko ya kuzuiwa kutoka CWT Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Abdallah Nandonde alipogigiwa simu kwa lengo la kupata ufafanuzi wa suala hilo, simu iliita bila kupokelewa.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, inadaiwa walimu zaidi ya 250 waliojitoa CWT na kujiunga na CHAKAMWATA wamezuiwa, alipogiwa simu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Erica Yegella ili kuzungumzia suala hilo simu yake iliita mara kadhaa bila ya kupokelewa.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza inadaiwa Walimu zaidi ya 170 wamezuiliwa kujitoa CWT na kujiunga na CHAKAMWATA, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Amon Mkoga, alipopigiwa simu alisema anawaomba viongozi wa CHAKAMWATA waende ofisini kwake wakazungumze.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, kuna walimu zaidi ya 217 waliojitoa CWT tangu 2025, lakini wanadai kuzuiwa kujiunga na CHAKAMWATA kwa madai kuwa hawajafuata utaratibu.
Hata hivyo, walimu hao wamesisitiza kuwa taratibu hizo tayari walishazifuata na walimu hao kama kujaza fomu namba 15 kutoa notisi kwa CWT na kwa mwajiri.
Katika Wilaya ya Singida DC Walimu waliohamia CHAKAMWATA kutoka CWT walilalamikia kuzuiwa na maofisa utumishi kwa madai wanasubiri kupata barua kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida.
Uchunguzi umeonyesha kuwa kuna Halmashauri nyingi ambazo walimu wamezuiwa kuondoka CWT na kujiunga CHAKAMWATA licha ya chama hicho kuwepo kisheria.
Jambo hilo la kuwazuia walimu kutojiunga na chama wanachokitaka limedaiwa kuingiliwa na baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa kuwapinga kujiunga na CHAKAMWATA na chama wanachokitambua ni CWT.
View: https://www.youtube.com/watch?v=n_HQif9bhSg