Naomba kutoa maoni yangu.
Kama katika maisha yako huna mipango ya maendeleo ya muda mfupi na muda mrefu, hutaweza kufanikiwa. Upeo wa kuona zaidi ya leo na kesho ni tatizo kubwa sana kwa maendeleo ya nchi zetu za Afrika.
Naomba kutoa mfano hai. Ninaishi Marekani (miaka 25 sasa). Nimeona jinsi wanavyopanga mipango ya muda mfupi na muda mrefu. Nitoe mfano wa mchezo wa mpira wa kikapu (Basketball), ambao Marekani ameutawala kwa muda mrefu. Kuna viwanja vya kikapu (Basketball playgrounds) kila sehemu. Kila shule za awali (pre-school), shule za msingi na sekondari (grade and high schools), na vyuoni, pamoja na sehemu zilizotengewa kama za wazi zimesheheni viwanja vya nje na ndani. Kwahio watoto kuanzia umri mdogo wanacheza na kufundishwa kuucheza mchezo huo. Kuanzia shule za msingi na sekondari mpaka vyuoni, kila shule ina makocha wa karibu kila mchezo aliyeajiriwa na shule. Sehemu ya kodi unayolipia sehemu unayoishi (kitongoji, mji, nk.) inalipia mishahara ya makocha na gharama nyingi za shule ikiwemo viwanja vya michezo. Kuanzia shule za msingi, kuna mashindano ya kitongoji (wilaya) mpaka jimbo zima. Kwahio, toka udogoni, unapata vikundi vya vijana ambao wanafundishwa jinsi ya kucheza pamoja na kuwa mwanamichezo (namna ya kufanya mazoezi, kula, kuongea na waandishi wa habari, nk).
Ukienda vyuoni, kuna chama kinachoongoza michezo (NCAA). Kinashirikisha vyuo vyote kulingana na madaraja (division 1, 2, etc). Wachezaji karibu wote mashuhuri wa kikapu waliopata na wanaocheza sasa katika ligi kubwa na maarufu ya kikapu duniani (NBA) kama Michael Jordan, Magic Johnson, Shaquille O'Neal, Hakeem Olajuwon, Tim Duncan, etc. wametokea katika mfumo huo. Mpaka wamefika kucheza vyuoni (NCAA), wameshapikwa kutoka mfumo wa chini (msingi na sekondari). Haya mashindano yanadhaminiwa na makampuni yote makubwa duniani kama Nike, Adidas, Coca Cola, nk. Hii ndio sababu Marekani wanatamba zaidi katika mchezo waliowekeza zaidi.
Kutokana na uwekezaji mkubwa na faida kubwa makampuni yaliyowekeza wanayopata, sekta ya michezo imefungua na kukuza sana michezo. Zaidi ya kuwafanya wachezaji wa kikapu kuwa matajiri sana, imefungua uchumi wa nchi na kuwajumuisha madaktari wa michezo, hospitali zenye vitengo vya kutibu wana michezo, wahasibu wa wachezaji, mawakala wa wachezaji, sports trainers, wasemaji wa wana michezo, etc. Imefanikisha kufanya vyuo kuanzisha degrees za michezo. Kwahio sekta ya michezo imekuwa muhimu sana katika kukuza uchumi wa Marekani.
Hata tulipowekeza kwa kiasi kidogo, mafanikio na maendeleo yaliwahi kuonekana. Mimi nilisoma shule ya msingi ya Upanga miaka ya themanini. Kulikuwa na mashindano ya mpira wa miguu kati yetu na Zanaki, Muhimbili, Olympio, nk. Wakati nasoma sekondari shule ya Azania (nikiwa nacheza kikapu), tulikuwa tunashiriki mashindano ya mkoa. Nimeshiriki Umisseta mara mbili (1990 na 1991). Timu yetu yote ya kanda ya Mashariki ndio iliyokuja kuunda vikosi vya kwanza vya Pazi na Vijana, ambazo ndio zilizokuwa zinatamba kwenye kikapu Tanzania. Nilienda Umisseta na wachezaji kadhaa ambao walikuwa kucheza Simba, Yanga, na timu zingine kwenye soka pia.
Ninachotaka kusema ni hichi. Katika orodha ya nchi zinazotamba katika michezo (kwa mfano mpira wa miguu), asilimia kubwa zaidi ni nchi zilizowekeza zaidi kuliko wengine. Zinakuwa zinashindana wenyewe kwa wenyewe. Hakuna suala la njia ya mkato au bahati. Ni mipango thabiti ya kuinua vipaji toka utotoni ndio njia pekee ya kupata vipaji na kuvikuza katika misingi mizuri. Kama unajua mwanao atakuwa anakwenda chuoni miaka mitatu ijayo na hujaanza kujipanga kupata fedha za ada na za kujikimu toka sasa, usilaumu mtu yoyote utakaposhindwa kumpeleka.
Michezo inahitaji uwekezaji kama vile tunavyowekeza kwenye sekta zingine. Lakini tukichukua michezo kama njia ya vijana kutoka jasho na kufanya mazoezi tu, hatutafika popote.
My 2 cents.