Kuna wakati huwa nakasirishwa sana na jinsi mambo ambavyo Raisi Samia aliamua kuendesha nchi, ili kuna mahali huwa nakifiri huwa namuonea sana huruma. Amekumbatia wapambe ambao tangu mwanzoni hakutakiwa kabisa kuwarudisha ofisini, kwasababu mbali na kuondolewa na Raisi Magufuli ukweli ni kwamba walikuwa na makandokando makubwa. Katika ngazi ya kiutendaji ndani ya Baraza la Mawaziri, kwenye hili sakata la Bandari Raisi ameachwa peke yake.
Ila kundi baya zaidi ni wale ambao wanamuunga mkono kwa maslahi binafsi, kama fedha, uzanzibari na dini. Bahati mbaya hili ndilo kundi ambalo sauti yake inasikika zaidi kuliko hata lile kundi ambalo linamuunga mkono kutokana na sera za kichama au utendaji wake. Kiufupi, hili kundi ndilo linazidi kumwaga chumvi kwenye kidonda kadiri ya siku zinavyoenda.
Mbinu ambazo hili kundi linazitumia ni zile za Tu QuoQue Fallacy za kusema, kama ninyi mlifanya kwanini Raisi Samia asifanye. AU Kama ninyi mlikosea kwanini Raisi Samia naye asikosee. Kiufupi limemponza sana mama wa watu. Yote tisa, mbali na kufanya mabadiliko makubwa ya kiuongozi inabidi mfumo mzima ufumuliwe. Itakuwa ngumu, lakini kama ana nia njema ya kulisaidia hilo taifa itabidi afanye hivyo.
Kiongozi wa Ufaransa na Baba wa Umoja wa Ulaya, Jean Monnet aliwahi kusema hivi "If you want things to work, you need to people. But if you want things to last then you need institutions".
Uzembe mwingi, rushwa na urasimu mkubwa ambao unaendelea nchini Tanzania, chanzo kikubwa ni kuendelea kutumia mifumo, falsafa na miundo ya kitaasisi ya karne iliyopita ilhali tuko ndani ya karne mpya. Nchi imekuwa kubwa sana ila mifumo haikui wala sera hazibadiliki kuweza kukidhi mahitaji mapya ya kimfumo. Hivyo basi ili mambo yafanikiwe ni lazima:
Mosi, muundo wa muungano uangaliwe upya. Hata kama hatutakuwa na Serikali tatu, basi ni lazima tupunguze nguvu kutoka serikali kuu (Central Government) na kuzipeleka chini kwa serikali za mitaa (Local Government) ambazo zitakuwa huru kwenye baadhi ya mambo. Muhimu ni kwamba watanganyika wanachokitaka ni ile hali ya wao kuwa na maamuzi kwenye baadhi ya rasilimali zao.
Pili, sheria za usimamizi na matumizi ya rasilimali ziwekwe bayana na zianze kusimamiwa kuanzia ngazi za serikali za mitaa na maamuzi mengine yafanyike huko bila kuliachia kila kitu bunge ambalo limejaa wala rushwa wasiokuwa na ufahamu wala uchungu na watu.
Tatu, mawaziri wa wizara nyeti kama Elimu, Nishati, Ulinzi, Mambo ya Nje na Mwanasheria Mkuu lazima wachaguliwe na Raisi na kuidhinishwa na Bunge. Hii tabia ya uswahiba na undugu ndiyo inatuletea hizi changamoto zinazoendelea. Kama Waziri Mkuu anapitishwa na Bunge lote, nini kinazuia mawaziri wengine wasipitishwe na Bunge, ??
Nne, wakuu wa vyombo vya usalama ni lazima nao wapitishwe na bunge na uzoefu wao ndani ya taasisi uwekwe wazi. Wametumikia taasisi husika kwa muda gani na katika nafasi zipi, ni mambo ambayo hayatakiwi kufichwa kabisa. Hata kama hatutazungumzia utendaji wa taasisi kwa undani, basi walau haya mambo ni lazima yawekwe bayana. Tabia ya kufanyia mambo gizani ndiyo yanajenga mazingira ya uzembe, rushwa na uvunjifu mkubwa wa sheria.
NB: Raisi akishafahamu kwamba wateule wake ni lazima watapitishwa na bunge, basi sidhani kama atateua watu kiholele tu. Tena hata ile tengua-tengua isiyo na kichwa wala miguu itapungua. Nafasi za Majaji, Mawaziri na Wakuu wa vyombo vya usalama ni lazima ziangaliwe upya na kurekebishwa ndani ya katiba ili tuondokane na hili jinamizi linaloendelea sasa. Unajiuliza mpaka dude la DP-World linapita hivi hakuna hata mmoja aliyesanua mchongo kweli,?