SoC04 Mabadiliko yenye tija katika shule za msingi na sekondari

SoC04 Mabadiliko yenye tija katika shule za msingi na sekondari

Tanzania Tuitakayo competition threads

Godwithus

Member
Joined
Jul 22, 2022
Posts
10
Reaction score
6
Tanzania ni moja kati ya nchi zinazopiga hatua katika maendeleo kwenye nyanja mbalimbali barani Afrika. Ni nchi iliyojaliwa raslimali nyingi kama madini, maji, misitu, mbuga za Wanyama na watu kama kiungo katika kuleta maendeleo. Licha ya hayo, bado kasi yake hairidhishi ikilinganishwa na mataifa mengine duniani kama vile Singapore, China, Afrika kusini, Kenya, nk. Hivyo nchi inahitaji mabadiliko makubwa katika elimu ili kuchochea kasi ya maendeleo kwa sababu mfumo wa elimu ulivyo, na utekelezaji wake bado itakuwa ni vigumu kupiga hatua za maendeleo makubwa.

Andiko hili limejikita kutazama madhaifu katika mfumo wa elimu msingi na sekondari na kutoa mapendekezo yatakayoleta mabadiliko makubwa ili kuendana na kasi ya dunia kwani elimu ndio msingi wa maendeleo katika maisha ya mwanadamu, bila mabadiliko katika elimu tutaendelea kuona kizazi cha vijana wasio na ubunifu katika maisha na nyanja zote ikiwemo teknolojoa, uchumi, biashara, ujasiriamali, nk. Pia haipendezi taifa lenye raslimali nyingi kuwa nyuma kimaendeleo, kupitwa na nchi ambazo hazina raslimali nyingi kama zilizopo Tanzania. Kwa hiyo ili mabadiliko yaje lazima mambo yafuatayo yafanyike.

Kuajiri walimu wenye ufaulu wa juu.
Mtu anayetaka kuwa mwalimu lazima awe na ufaulu wa juu kwa kupata daraja la kwanza katika mitihani ya kidato cha nne na sita, hii itasaidia kupata walimu wenye uwezo mkubwa kitaaluma. Mfumo wa sasa mhitimu aliyepata daraja la tatu kidato cha nne na sita anaweza kusomea ualimu. Hadhi ya mwalimu inashuka na kuonekana kama waliofeli mitihani, wanaopata alama za chini ndio wanakimbilia kwenye ualimu na hii imepelekea kupata walimu wenye uwezo wa chini kitaaluma. Sasa ili elimu ikue lazima hadhi ya mwalimu ionekane katika jamii, ikiwa ni Pamoja na uwezo wake kitaaluma kuwa juu ndipo afundishe wanafunzi. Mwalimu ambaye alifaulu vizuri ataheshimika katika jamii, pia atafanya kazi kwa kujiamini na kuipenda, hivyo kulisaidia taifa. Kuna baadhi ya walimu hawataki hata kujitambulisha kama wao ni walimu kwa kuwa hawajiamini kutokana na mfumo wa kuajiri kutokuwa mzuri

Walimu wa shule za msingi wasifundishe masomo yote.
Swala la walimu wa shule za msingi kufundisha masomo yote linaua elimu, ni vema hata shule za msingi walimu wabobee kwenye kufundisha somo moja na lingine la ziada kama sekondari. Kuna baadhi ya shule hazina walimu wa kutosha hivyo waliopo hutakiwa kugawana masomo yote kwakuwa wamaeandaliwa kufundisha masomo yote, lakini kuna walimu hawana uwezo kufundisha baadhi ya masomo na hulazimika kutimiza wajibu huo. Kinachofanyika ni ilimradi tu kazi iende lakini haileti tija katika elimu kwa sababu ni vigumu kwa mwalimu kumudu masomo yote ipasavyo. Mwalimu ili akamilishe ufundishaji anatakiwa kuandalia somo, nukuu, zana nk. Haya yote hayawezi kufanyika katika ubora kama ana masomo mengi.

Vyumba vya mitihani vifungwe kamera (CCTV)
Kumekuwa na udanganyifu wakati wa mitihani kwa ushirikiano baina ya wazazi, wasimamizi wa mitihani, maofisa wa ngazi za juu ambao kimsingi huwa wanatakiwa kuwajibika endapo matokeo katika maeneo wanayoyasimamia yatakuwa mabaya. Pia maandalizi duni yanayotokana na aina ya wanafunzi, uzembe na changamoto mbalimbali katika mazingira hupelekea kutafuta njia mbadala ya kufaulisha. Hivyo kipindi cha mitihani kamera zifungwe nchi nzima ziwe mubashara kwenye kitengo maalumu cha kufuatilia usimamizi na kubaini matukio yanayokwenda kinyume na sheria za mitihani. Itasaidia kupata wasomi wenye sifa watakaolisaidia taifa kwani sasa kuna wasomi wengi wenye vyeti vyenye alama za juu lakini uwezo wao na utendaji ni duni.

Wasimamizi wa mitihani waombe na wapatikane moja kwa moja kutoka balaza la mitihani.
Mfumo uliopo wasimamizi wa mitihani kuteuliwa, na wanaosimamia zoezi hilo huwa ni maafisa elimu kwa kushirikiana na walimu wakuu, wakuu wa shule ili kuwapata walimu wa kusimamia mitihani. kumekuwa na malalamiko ya zoezi hili kuambatana na rushwa na upendeleo. Kuna baadhi ya shule huwa zinapelekewa wasimamizi walewale kila mwaka, wasimamizi hao hutoa ushirikiano kwa jambo lolote ikiwemo udanganyifu na wasipotoa ushirikiano hawatateuliwa tena miaka inayofuata. Haya yanafanyika kwa sababu wanaotakiwa kuwajibika endapo matokeo yatakuwa mabaya ndio wanaosimamia uteuzi huo, hivyo ni lazima watatengeneza mazingira ya kulinda nafasi zao kwa kufanya matokeo yawe mazuri, hatimaye taifa linapata wasomi wasio na uwezo kuleta maendeleo, hivyo ni vema wasimamizi wa mitihani waombe halafu wachaguliwe na balaza la mitihani.

Sekta ya elimu isisimamiwe na wanasiasa.
Elimu ndio msingi wa maendeleo na mabadiliko katika jamii, ni vema kukaundwa chombo huru kisichofungamana na maswala ya siasa. Kuna Waziri wa elimu, Waziri wa TAMISEMI, hawa wote ni wanasiasa. Madhara yanakuwa mabaya kwani wanasiasa hao kutokana na mfumo wa utawala, wanateuliwa na rais ambaye naye ni mwanasiasa, viongozi hawa kwa kuwa wanatakiwa kuwajibika kwenye mamlaka ya uteuzi hawawezi kukosoa waziwazi mifumo mibovu ambayo kimsingi ipo katika elimu na imesababishwa na serikali yenyewe ambayo nao wamo. Kwa mfano ni vigumu kwa mawaziri kuonesha, kukosoa au kusemea changamoto katika elimu ikiwemo nyumba za miti wanazoishi walimu, walimu kukosa makazi na kuishi madarasani, wanafunzi kusomea chini ya miti, wanafunzi kujisaidia porini kutokana na uhaba wa vyoo, nk. Wakiyasema haya ikiwa yanaiaibisha serikali, nao nafasi zao zinaweza kuwa hatarini kutenguliwa hivyo watakaa kimya mambo haya yaibuliwe na jamii au makundi mengine ya watu ikiwemo mitandao ya kijamii na wanahabari.

Wanafunzi waruhusiwe kutumia simu shuleni.
Ulimwengu wa sayansi na teknolojia inayokua kwa kasi simu hasa simu janja ni kifaa muhimu katika kurahisisha kazi, chaweza kutumika kupakua au kutazama maudhui yanayohusiana na masomo badala ya Kwenda maktaba au kutafuta vitabu. Pia licha ya mawasiliano simu huibua vipaji na ubunifu. Kwa mfano mwanafunzi anaweza kujifunza, kuchora, kusuka, kupika, kupamba, muziki, ubunifu wa mavazi nk. Hivyo ni vema serikali ikaachana na dhana potofu ya kuwazuia wanafunzi kumiliki simu kwa kigezo cha kuharibika kimaadili kutokana na matumizi mabaya ya simu. Jambo la kufanya ni kuruhusu na elimu itolewe jinsi na namna bora ya kutumia simu. Kwa kufanya hivyo elimu itakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo

Hitimisho
Serikali ikubali kufanya mabadiliko ili elimu iwe na tija, sio kuwa na mlundikano wa wasomi ambao elimu haiwasaidii kupambana na changamoto za mazingira kama kujiajiri, ubunifu, sayansi, teknolojia, biashara nk. Pia serikali iboreshe mazingira na kipato cha mwalimu ili afanye kazi kwa moyo aipende kazi yake. Walimu wana changamoto nyingi ikiwepo madeni wanayoidai serikali, makazi duni, uhaba wa miundombinu mahala pa kazi nk. Maboresho yakifanyika kutakuwa na mabadiliko elimu itakuwa na tija kwa taifa.
 
Upvote 3
Back
Top Bottom