Kwa zaidi ya muongo mmoja, Khadija Ali Saleh aliishi na maumivu makali ambayo hatua kwa hatua yaliondoa furaha na ubora wa maisha yake. Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 76, mkazi wa Zanzibar, Tanzania, alisumbuliwa mara kwa mara na vipindi vya kiungulia kikali na maumivu kifuani yaliyosababishwa na ugonjwa wa asidi ya tumbo. Kile kilichoanza kama hali inayoweza kuvumilika kilibadilika taratibu na kuwa hali mbaya zaidi, na kumlazimisha kutegemea dawa ili kuweza kuishi siku hadi siku.
Khadija anasema aliteseka kwa miaka mingi, kwani kila mara baada ya kula, alipata maumivu kifuani, na wakati mwingine alishindwa hata kupumzika vizuri. Kesi yake ilipelekwa Hospitali ya Lumumba, Zanzibar, ambako baada ya vipimo kadhaa, madaktari walimgundua kuwa na tatizo la kupanuka kwa sehemu ya juu ya tumbo (hiatal hernia). Hata hivyo, hospitali hiyo ilikuwa haijawahi kufanya upasuaji wa uvamizi mdogo kutibu hali hiyo.
Wakikabiliwa na changamoto ya kumtibu mgonjwa mzee kwa machaguo machache yaliyopo, madaktari waliigeukia Timu ya 35 ya madaktari wa China huko Zanzibar kwa usaidizi, uamuzi ambao Khadija anasema ulibadili kabisa maisha yake.
Kiongozi wa timu ya madaktari wa China na mtaalamu mwandamizi wa upasuaji, Bao Zengtao, anasema baada ya kupokea ombi hilo, mara moja walianza kuitathmini kesi hiyo, na jibu lilikuwa wazi kwamba dawa haziwezi tena kutatua tatizo hilo, bali upasuaji ndio chaguo pekee lililobaki.
Kutokana na pengo la uwezo wa upasuaji huko, Bao alipanga kupeleka vifaa maalum kutoka China, ikiwemo visu vidogo vya upasuaji na vibanio vinavyotumika wakati wa upasuaji, vifaa ambavyo vilisaidia sana katika kufanya upasuaji huo mgumu.
Siku ya upasuaji, timu ya madaktari wenyeji ilikusanyika katika chumba cha upasuaji. Kwa kutumia ufundi wa mwonekano wazi wa eneo la upasuaji (laparoscope), Bao alifanya upasuaji sahihi na kurekebisha sehemu ya juu ya tumbo, operesheni ambayo ilimaliza kiini cha ugonjwa wa muda mrefu uliomsumbua Khadija.
Upasuaji huo ulikuwa zaidi ya kumtibu mgonjwa mmoja, kwani kupitia mchakato huo, Bao alitoa mwongozo wa moja kwa moja kwa wataalamu wa upasuaji wa Zanzibar, akieleza mifumo muhimu ya tumbo, ufundi wa upasuaji na mikakati ya kudhibiti hatari. Mtaalamu wa upasuaji katika Hospitali ya Lumumba, Haitham Hamudu, anasema hiyo ilikuwa hatua kubwa kwao, kwani ilifungua mlango wa matibabu kwa wagonjwa wengine huko.
Tangu Timu ya 35 ya madaktari wa China kupelekwa Zanzibar, imejumuisha huduma za kliniki na mafunzo ya ujenzi wa uwezo, kwa lengo la kujenga kile wataalamu wanachokiita “timu ya madaktari ambayo kamwe haitaondoka.” Kupitia mafunzo ya kivitendo, ushauri na utambulishaji wa teknolojia mpya, timu hiyo sasa inasaidia kuimarisha mfumo wa huduma ya afya huko katika njia endelevu.
Kwa Khadija, kitu kilichomvutia zaidi ni kwamba uponyaji ulikuwa wa haraka, kwani ndani ya siku chache, dalili zote zilizokuwa zinamsumbua kwa miaka mingi zilipotea, na anasema anahisi kama amepewa maisha mapya. Kwa sasa Khadija anatumia siku zake kupumzika na kufurahi pamoja na familia yake kubwa, na anaishukuru sana timu ya matibabu ya China kwa kumpa fursa nyingine ya maisha.