Nimefurahi uwepo wenu humu.
Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa ipo chini ya Wizara, licha ya kuwa na upungufu wa madaktari wa kawaida na bingwa pia ina uhaba wa vifaa tiba. Leo naomba nijikite kwenye mashine ya CT Scan.
Ninaomba Wizara ya Afya mnunue hiyo mashine ya CT Scan kwani ni aibu kwa mkoa wa Iringa kukosa hospitali ya umma yenye mashine hiyo, kwa Manispaa ya Iringa hata hospitali za Binafsi hazina kifaa hicho hivyo kulazimu mgonjwa kusafiri nje ya mkoa kufuata kipimo hicho.
Ukisoma mitandaoni unaona gharama za kununua mashine hizi ni kati ya milioni 400 mpaka bilioni 2, hii ni fedha ya kawaida sana kwa serikali yetu hii. Mwaka juzi 2019, Hans Pope kupitia kundi sogozi la whatsapp aliahidi kufunga mashine hii katika hospitali ya Mkoa, ila wazo halikutekelezwa mpaka sasa, inasemekana alizuiwa kwa sababu za kisiasa (alikuwa anatajwa kugombea ubunge - ununuzi wa hiyo mashine labda ungembeba kisiasa). Sasa naombeni mnunue mashine hiyo, ni aibu kwa karne ya leo kukosa vipimo kama hicho ambavyo ni vya kawaida sana kwa sasa.
Manispaa wamelala usingizi wa pono, badala ya kuwaza kununua vifaa tiba kwa hospitali ya Wilaya ya Frelimo wao wanajenga kwa mapato ya ndani jengo la abiria la stendi isiyotumika ya Igumbilo linalogharimu mabilioni, mawazo yao ni kwenye mapato na sio kuhusu ustawi wa wananchi.
Tunaomba Wizara mtununulie mashine hiyo kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa iliyo chini yenu, hata mashine ya shilingi milioni 500 tu (hata used kama sheria zinaruhusu) mtusaidie wananchi.