Imeripotiwa hapa JF kuwa Mkapa anaona umuhimu wa katiba mpya. Pia imeripotiwa kuwa Jaji Bomani naye amezungumzia umuhimu wa katika mpya.
Kwa upande mmoja ni hali inayoleta faraja, kwa upande mwengine inatia shaka kwa wana CCM kujitokeza hadharani na kukiri kuwa kuna umuhimu wa katiba mpya.
Sina mashaka sana na Jaji Bomani, lakini Napata tabu kuamini kuwa Mkapa anakusudia au anaamini anachokitamka.
Tunazikumbuka kauli zake za ukweli na uwazi au siyo?
Jee alihakikisha kuwa utawala wake kiutendaji unasimama juu ya kauli hiyo?
Watajitokeza wana CCM wengine ambao wataingia katika orodha ya watu wanaotoa kauli kuwa kuna umuhimu wa katiba mpya. Halafu wataishia hapo kwenye kauli.
CCM kama chama na serikali za CCM kama watawala hawana mazoea au utamaduni wa kuwaacha wanachama wake , na kuwaruhusu watendaji wake kutoa mawazo yao kwa uwazi hadharani. Utamaduni wao ni kuzungumzia katika vikao vya ndani vya Chama chao na Vikao vya uongozi wao.
Sasa kunani?
Lakini la kutia wasiwasi zaidi ni kuwa kauli ya Bw. Mkapa imetolewa akiwa nje ya nchi. Kwa mulio karibu naye mpitishieni ujumbe. Kama ni kweli anaamini anayoyasema basi aitishe mkutano na waandishi wa habari ili atowe kauli yake hiyo na watanzania wamsikie na hapo wanahabari watapata nafasi ya kumuuliza masuali kwa vipi anaona hiyo katiba mpya itapatikana na muda ambao anaona iwe tayari kutumika.
Kwa wanahabari au zile taasisi za kuandaa midahalo, majadiliano ni vyema kuandaa mkutano kwa kuanzia japo mmoja wa kuwaweka pamoja, kuwakutanisha hawa wote kwa pamoja ambao ni CCM ili nchi nzima ipate kuwasikia na kujuwa kuwa ndani ya CCM pia wapo wanaotaka , au wanaoona umuhimu wa katiba mpya na tuweze kusikia hoja zao.
Hofu yangu mimi ni kuwa CCM wameanza propaganda ili ionekane kuwa watalishughulikia suala la katiba. Wanajaribu kulihodhi, kuliteka nyara suala la katiba mpya. Wanajaribu ku-preempt wapinzani na wale wote ambao wamekuwa na kilio hiki cha kutaka katiba mpya kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Nitafurahi sana ikitokea kualikwa kwa Jaji Warioba katika mjadala huo, yeye ndiye alishiriki kikamilifu kuiandika hii katiba inayotiwa viraka, kwa hivyo atasaidia, kama hatoweka Uccm mbele, kuonesha mapungufu yaliyomo katika katiba hiyo,( tayari yanajulikana), lakini ataweza kuchangia kwa nini iliandikwa vile ilivyoandikwa. Na kwa nini sasa ni busara kuandika katiba mpya.
Wananchi, wanaharakati, wapinzani , vyama vya kitaaluma na asasi za kiraia zisije zikaingizwa mkenge huu kuona kuwa wanaCCM pia wanaunga mkono katika kudai katiba mpya.
Kwa CCM, linapokuja suala la CCM na Taifa , basi chaguo ni maslahi ya CCM first, baadae ndio maslahi ya taifa.
CCM na serikali zake kupitia waziri wa sheria na katiba wameshatoa msimamo wao kuwa hakuna ulazima wa katiba mpya, ila wataendelea kuweka viraka pale panapohitajika.
Tukiamini kiulaini kauli tunazozisikia basi tuelewe kuwa tunauziwa mbuzi ndani ya gunia.