Rais John Magufuli ameingia kwa kishindo mkoani Mara, aking’aka baada ya kubaini mradi wa maji Bunda, haujakamilika tangu ulipoanzishwa miaka minane iliyopita.
Hilo lilimfanya Rais amkumbuke Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere na kusema, angetokea leo, basi hata yeye angeshangazwa kusikia mradi huo haujakamilika.
Rais Magufuli ambaye alianza ziara yake Mara, akitokea Mwanza, amewataja mawaziri waliosimamia wizara ya maji katika kipindi cha miaka minane iliyopita na kusema:
“Wakati kuna mawaziri walikuwepo tangu wakati huo zaidi ya watatu, Lwenge, Magembe, Kamwelwe na sasa Mbarawa,”alisema.
Aliongeza: “Inashangaza, Nyerere atamshangaa hata huyo mkandarasi, wanabebana si ndiyo, wanabebana si ndio, wataachiana. Nasema wataachiana, naomba hilo mniachie hili nalibeba mimi mwenyewe. Kama mkandarasi mshenzi, mimi mshenzi zaidi, kama ni kufukuza watu wafukuze, kama ni kuwatumbua, watumbue.”
Magufuli aliyasema hayo baada ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Simona Mayaya kumuomba Rais kuingilia kati tatizo la ukosefu wa maji linaloukabili mji huo.
Rais Magufuli alimtaka mkuu wa mkoa kufanya kazi na wakandarasi na ameahidi kumtuma waziri wa maji na katibu mkuu wizara hiyo kusimamia suala hilo.
“Nataka kuahidi maji Bunda lazima mpate. Hamuwezi kunichagua bure, halafu mimi nisiwasaidie,” alisema.
Mradi wa kupeleka maji kwenye mji wa Bunda kutoka ziwa Victoria katika eneo la Nyabeho ulisanifiwa mwaka 2006 na ulikuwa unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha za maendeleo.
Mayaya alipoulizwa ni kampuni gani ya ukandarasi inayohusika na ujenzi wa mradi huo aliomba kusaidiwa na mkuu wa mkoa.
Jibu hilo lilimfanya rais Magufuli amuite Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima ambaye alieleza kufahamu kuhusu sakata hilo na kueleza kuwa hatua zimeanza kuchukuliwa.
Alieleza kuwa hata Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipofika wilayani humo alikuta sintofahamu hiyo na ikaamuliwa kuvunjwa kwa bodi ya Mamlaka ya Maji safi ya Musoma (Muwasa) na aliyekuwa mkurugenzi wake Mhandisi Gantala Said akikamatwa na kuhojiwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Ruswa (Takukuru).
Baada ya kusikia maelezo hayo Rais Magufuli akahoji sababu za mradi huo kutoendelea na kama mkandarasi ana uwezo wa kuukamilisha.
“Kwa hiyo siku zote hizo mnaendelea kuchunguza, kwanini msihakikishe mradi unakamilika na watu wanapata maji. Kwahiyo na wewe mkuu wa mkoa unachunguza? Haya sasa niambie mkandarasi ana uwezo wa kukamilisha mradi huo ndani ya muda gani,”alisema
Aliongeza: “Mkandarasi alikamatwa ila ametolewa nje kwa dhamana na jinsi ninavyomuona hawezi kumaliza mradi huu na fedha zote alishalipwa hivyo tumemuomba waziri tuvunje mkataba.”
Kutokana na maelezo hayo rais Magufuli aliagiza waziri wa maji na katibu mkuu kwenda wilayani humo na kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo ili maji yaweze kupatikana.
Rais Magufuli pia alizungumzia sakata la mwekezaji anayefahamika kwa jina la Magoma anayewataka wakazi wa kijiji Kinyabwiga kuhama kwa kile anachodai ana leseni ya kuchimba madini.
Wakiwa na mabango yanayolalamikia kunyang’anywa ardhi, wananchi hao walidai kuwa hawana pa kwenda baada ya mtu huyo kuwataka kuondoka katika maeneo yao ndani ya siku saba.
“Huyo Magoma agome mwenyewe hakuna wa kumtoa mwananchi kule, RC, DC kama ulimleta wewe mwambieni atoke,”
“Akitaka kuwahamisha awalipe kwa fedha mnazozitaka ninyi hawezi kujiamulia kwas ababu ana leseni kwani hayo madini aliyazaa yeye,”alisema.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kumsimamisha kazi Kamishna wa Ardhi wa kanda, Bunda kwa kushindwa kumrudishia kiwanja anachodai kudhulumiwa, mwanamke mmoja mkazi wa Bunda.
Awali mkazi wa eneo hilo, ambaye hakujitambulisha jina alilalamika mbele ya Rais Magufuli kuwa alikuwa na viwanja viwili na kimoja, kimechukuliwa na tajiri mmoja.
Pamoja na kutoa maagizo hayo, pia Rais alimpa mkazi huyo, Sh 500,000 ili zimsaidie.
Katika hatua nyingine, akiwa eneo la Mwisenge, Musoma, Rais Magufuli alizungumzia mgogoro kati ya wakazi wa eneo hilo na mkandarasi wa kampuni ya Nyakinyang’ari wa kujenga mradi wa maji Bunda.
Rais Magufuli alisema ana taarifa kuwa mtu huyo amevikamata vyombo vya dola ndiyo sababu anafanya mambo yake anavyotaka.
“Nimepata taarifa ni mwana CCM na amevishikilia vyombo vya dola hapa sasa nasema uhalifu hauna chama sheria ichukue mkondo wake, haiwezekani ndani ya miaka minane mradi unasuasua halafu viongozi wangu niliowateua wapo tu wanamuangalia anadunda
“Sasa nitawageukia nyinyi ili wananchi wasiendelee kuteswa kwa kukosa maji, nitawatesa nyinyi,”
“Mliopa nataka mumnyang’anye apewe mwekezaji mwingine na ikiwezekana alipe fedha zote za miaka 10 ambayo amezuia hoteli kufanya kazi. Hivi huyu ni mtu wa aina gani alipewa mradi wa maji Mugumu akashindwa akafukuzwa,”alisema
Awali, mkazi wa eneo hilo, Edwin Wilson alisimama na kumwambia Rais Magufuli kuwa Hoteli ya Musoma ilikuwa inawasaidia kwa mambo mengi ikiwamo ajira lakini mwekezaji mpya aliyeinunua anazuia hata watu kuingia.
“Hoteli ya Musoma ilikuwa inatulisha pamoja na kutoa ajira lakini sasa tunazuiwa hata kuingia ziwani,’’ alisema.
Rais Magufuli alisema mwekezaji alipewa hoteli hii miaka kumi lakini hakuna alichokifanya.
Rais Magufuli pia aligusia suala la mkuu wa wilaya ya Musoma la kuwatishia kuwaweka ndani wanakijiji wa Mwisenge endapo wangebeba mabango wakati wa ziara yake.
Alieleza kuwa wananchi hao walikuwa wakilalamikia kitendo cha mmiliki wa hoteli ya Musoma kuzuia njia ya kwenda ziwani hivyo kuwalazimu kuzunguka umbali mrefu kufikia eneo la ziwa.
“Nina taarifa za tishio la Dc kwa wananchi, yani yeye yupo ndani ya ofisi ina bendera ya nchi sasa anataka kuwaweka wananchi ndani ili wasieleze kero zao, taarifa zote ninazo sitaki watanzanioa wateseke ninachowaambia sasa katizeni hapo hapo kwenye hoteli nendeni mkaogelee ziwani,”
“Ninyi ndio mmeniwezesha kuwa Rais msingenichagua nisingekuwa Rais, nawaagiza watendaji, wakuu wa mikoa, makamanda wa polisi na wakurugenzi kuanzia sasa hawa watu wasizuiwe kwenda ziwani, haiwezekani,” alisema.
Alisema eneo hilo lipo wazi na wananchi wanaweza kufanya shughuli zao hata wakitaka kuifanya fukwe.
Akizungumza katika uwanja wa Mukendo, Musoma, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, kero kubwa mkoani wilayani Musoma ni maji.
Hata hivyo amesema kutokana na utekelezaji wa ilani ya CCM, mradi wa maji wa Mugango utasainiwa katika wiki mbili zijazo.
“Umetupa bilioni 3 tumeboresha vituo vya afya saba wilaya za Tarime, Rorya Bunda, Serengeti na Butiama. Miradi ya Barabara ikimalizika itafungua fursa kiuchumi,”alisema
Alisema kuna mikakati ya kuboresha kilimo cha pamba kutoka kuzalisha tani 6000 hadi tani 60,000 na msimu uliopita mkoa umefanikiwa kuzalisha tani 20000.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Musoma Vijijini, Sospeter Muhongo amemkumbusha Rais kuwa hii ni mara ya pili kwa Rais Magufuli kwenda mkoani humo katika kipindi cha miaka mitatu.
“Umekuja hapa tulipofanya kampeni na Mzee Warioba,” alisema.
Mawaziri wazungumza
Alipoulizwa kuhusu kukosekana kwa maji Bunda, aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge alisema waziri wa maji ndiye anaweza kuzungumzia suala hilo huku akihoji kama waziri anaweza kupeleka maji bila nguvu ya Serikali.
“Mtafute waziri wa maji ndiyo azungumzie hilo. Lakini waziri anawezaje kupeleka maji bila nguvu ya Serikali? Sasa si mtatafuta hata mawaziri waliokufa,” alisema Lwenge ambaye pia ni mbunge wa Wanging’ombe.
Kwa upande wake Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa alieleza kusononeshwa kwake na kusuasua kwa mradi wa maji wa Bunda na kuahidi kuchukua hatua kwa makandarasi wote wasio waaminifu.
“Mkandarasi huyu si mwaminifu na wala hana uungwana amekuwa akichukua fedha halafu hafanyi kazi, kuanzia sasa tutawachukulia hatua na kuhakikisha maji yanapatikana katika mji wa Bunda,”alisema.