BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,591
- 8,826
Mgomo wa wafanyabiashara katika Soko Kuu la Mafinga lililopo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wa kufunga maduka, umeingia siku ya pili leo Agosti 24, 2024 ukisababisha adha kwa wananchi kukosa huduma.
Mwananchi limefika sokoni hapo na kushuhudia milango ya maduka hayo imefungwa huku baadhi ya wananchi waliofika kwa ajili ya kupata huduma wakiduwaa wasijue cha kufanya.
Wafanyabiashara wamedai kuwa hawatafungua maduka hadi malalamiko yao ya kupunguziwa kodi ya Sh80,000 yatakaposikilizwa.
Mwananchi ilimtafuta Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa kuzungumzia hali hiyo lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda baada ya kutafutwa bila mafanikio.
Hata hivyo, Diwani wa Boma, Julias Kisoma lilipo soko hilo, amethibitisha wafanyabiashara hao kufunga maduka kwa madai kodi wanayolipa ni kubwa.
“Wafanyabiashara wanalalamikia kodi wanayolipa ni kubwa ambayo ni ya zaidi ya asilimia 200, lakini mimi kama diwani nitaendelea kuwasemea wafanyabiashara hawa hadi pale nafasi yangu ya uongozi itakapokoma,” amesema diwani huyo.
Wakizungumzia adha hiyo, baadhi ya wananchi wamesema hali hiyo imewasababishia adha kubwa ya kufika sokoni bila kupata mahitaji kutokana na mgomo huo.
“Nimetoka kijijini kwa ajili ya kununua mahitaji ya duka langu lakini nimefika hapa nimekuta maduka yamefungwa, hivyo nimepoteza nauli muda katika suala hilo,” amesema mkazi wa Mtili, Prisca Mlelwa.
Mlelwa ametoa ombi kwa Serikali kukaa meza moja na wafanyabiashara hao ili wafikie mwafaka na kuendelea na biashara zao.
MWANANCHI