Date::9/9/2008
Marekani yasubiri majina ya mafisadi toka serikali ya Tanzania
Na Kizitto Noya
Mwananchi
MAREKANI imesema inasubiri orodha ya mafisadi kutoka serikali ya Tanzania ili iwaingize kwenye orodha ya watu wanaotakiwa kuzuiwa kuingia ndani ya taifa hilo la Amerika Kaskazini.
Marekani, ambayo inasifika kama kinara wa demokrasia duniani na ambayo imekuwa mstari wa mbele kupiga vita ufisadi, juzi ilitangaza kuwa watu wote wanaojipatia fedha isivyo halali kwenye nchi zao, hawataruhusiwa kuingia nchini humo kwa shughuli za kibiashara, matembezi au kutafuna fedha hizo haramu.
Jana, msemaji wa ubalozi wa Marekani nchini, Jaffery Salaiz aliliambia gazeti hili kuwa kwa sasa nchi hiyo haina orodha ya mafisadi wa Tanzania na hivyo haiwezi kuwaingiza kwenye mpango huo mpya, lakini macho yake yanaelekezwa kwa watuhumiwa wa ufisadi wa EPA, Richmond na Rada.
Salaiz alisema hayo alipoulizwa na gazeti hili endapo Marekani imeshapata orodha ya mafisadi inaokusudia kuwazuia kuingia nchini humo kama sehemu ya utekelezaji wa tangazo namba PP7750 la Rais George W. Bush.
Alisema watuhumiwa wa ufisadi wa wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), utoaji wa zabuni kwa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond na ununuzi wa Rada wataingizwa katika orodha hiyo baada ya kuthibitika kuwa walishiriki katika vitendo vya ufisadi unaoathiri maslahi ya Marekani.
"Sasa hatuna orodha yao na hao wanaotuhumiwa kwa ufisadi wa EPA, Richmond na Rada wataingia kwenye orodha yetu baada ya mchakato unaoendelea sasa na kuthibitika kuwa walishiriki matendo ya ufisadi," alisema Salaiz.
Katika tangazo hilo la rais namba PP7750 Marekani pia imekusudia kuwafukuza maafisa wa serikali wanaotuhumiwa kwa ufisadi na ambao tayari wamewekeza nchini humo au kusafiri kwa ajili ya matumizi ya mali walizopata kinyume cha taratibu.
Marekani imekuwa ikionekana kama kiota cha mafisadi ambao hujichotea mamilioni ya fedha kwenye serikali za nchi changa na kutowekea kwenye taifa hilo kwa lengo la kuwekeza, kutembea au kuanza maisha mapya.
Balozi wa Marekani nchini, Mark Green alisema katika taarifa yake kuwa mafisadi wanaoomba na kupokea rushwa na hata wanaotumia madaraka yao vibaya, pamoja na ndugu, jamaa na marafiki zao wanaofaidika na ufisadi huo, hawataruhusiwa kuingia Marekani.
Green alisema uamuzi huo ni tangazo jipya la rais na linawahusu maafisa wa umma na viongozi wa serikali wenye tabia ya kuomba na kupokea rushwa au kutumia madaraka yao vibaya kwa faida binafsi.
Kwa mujibu wa Balozi Green, marufuku hiyo ya kuingia Marekani pia inawahusu wachumba, watoto na wategemezi wa wafanyakazi wa sekta binafsi wenye tabia ya kuwahonga watendaji wa serikali na maafisa wa umma ili wafanye mambo kwa maslahi yao badala ya umma wanaoutumikia.
Alisema Marekani haitakubali kuwa kiota salama cha mafisadi na walarushwa na mpango huo mpya wa kuwazuia mafisadi kuingia nchini humo, umelenga kuieleza dunia kwamba Marekani iko makini katika suala hilo.
"Uwazi na vita dhidi ya ufisadi ni tunu za Marekani. Tunaendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania ili kung'oa mizizi ya ufisadi na kumpeleka mbele ya sheria mtu yoyote anayetuhumiwa na kubainika kushiriki matendo ya kifisadi," alisema Green katika taarifa yake.
Alisema mpango huo unawalenga watumishi walioshiriki ufisadi nchini mwao na kuathiri maslahi ya Marekani ambayo ni pamoja na shughuli za biashara za kimataifa na uchumi za nchi hiyo.
Green alitaja maslahi mengine ya Marekani yanayopaswa kulindwa kuwa ni malengo ya misaada yake kwa nchi husika, usalama wa nchi hiyo, ujenzi wa demokrasia na mambo yanayokiuka sheria mpya ya rushwa inayofanyika katika matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Mpango huo wa Marekani umeanza kuwa maarufu duniani baada ya kuanza kutekelezwa na karibu nchi zote zilizoendelea (G8) kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya nchi hizo yaliyofikiwa mwaka 2003.
Katika Mkutano huo wa Juni 2003, Rais George Bush wa Marekani na viongozi wengine wa nchi hizo walikubaliana kutoruhusu nchi zao kuwa kimbilio la Mafisadi kutoka nchi zinazoendelea.
Marekani na wenzake pia wamekubaliana kushirikiana na nchi zinazoendelea kuwatambua, kuwatafuta, kufuatilia mali za mafisadi na kuzikamata kisha kuzirudisha kwa wahusika na kuwafungulia mashtaka.
Hivi karibuni viongozi hao katika mkutano mwingine uliofanyika Hokkaido, walikubaliana kuendeleza ushirikiano huo unaoongozwa na Umoja wa Nchi za Amerika (OAS) na Jukwaa la Kiuchumi la Asia Pacific Cooperation (APEC)