DOKEZO Maghala ya SHIRECU yanataka kuuzwa kwa 'bei ya kutupa', TAKUKURU fuatilieni kuhusu hizo mali za Umma?

DOKEZO Maghala ya SHIRECU yanataka kuuzwa kwa 'bei ya kutupa', TAKUKURU fuatilieni kuhusu hizo mali za Umma?

Hili ni dokezo maalum toka kwa mwananchi mtumiaji wa JF mwenye nia ya kuusaidia umma kuwa na taarifa 'maalum'
A

Anonymous

Guest
Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Shinyanga (SHIRECU) inadaiwa kipo kwenye mchakato wa kuuza maghala yake yaliyopo Kurasini Jijini Dar es Salaam kwa bei ya 'kutupa' (bei hisiyo na thamani halisi) huku yakiwa ndiyo tegemeo kubwa la mapato katika ushirika huo.

Hali hiyo ambayo inahofiwa kuwa ina msukumo wa rushwa imebainika hivi karibuni kwenye mkutano mkuu wa kawaida wa 30 ambapo Bodi ya Ushirika huo ilitoa taarifa kwa wanachama wakiombwa kuridhia kuuzwa kwa maghala hayo kwa mpangaji wao wa hivi sasa kwa makubaliano ya kulipwa viwanda viwili vya kuchambulia Pamba.

Inasemekana shinikizo la kuuzwa kwa maghala hayo linatoka kwa baadhi ya viongozi wa juu wa Serikali wakiongozwa na Waziri mmoja wa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan (jina tunalo) ambaye iwapo yatauzwa na wao watakuwa na mgao wao.

Pamoja na taarifa hiyo kutolewa kwa wajumbe wa mkutano mkuu, wanachama wa SHIRECU wamekataa maghala hayo yasiuzwe, huku moja ya hoja wanayoisimamia ni kwamba iwapo yatauzwa itakuwa ni kumsaliti vibaya Rais Hayati John Magufuli aliyeyakomboa baada ya kuuzwa nje ya utaratibu miaka ya nyuma.

“Ni kweli taarifa hii imetolewa kwenye mkutano wetu mkuu wa hivi majuzi, lakini tumekataa, na tumeielekeza Bodi badala ya kuyauza waongeze majengo mengine katika eneo hilo, na tumesema hata kama viongozi wa Serikali wataendelea kushinikiza suala hili, uitishwe mkutano mkuu maalumu haraka.

“Tumesema haiwezekani mali ambayo kwa sasa ni sawa na roho ya Ushirika iuzwe kinyemela, hili tumelikataa na kulipinga kwa nguvu zote hata kama kuna mkono wa Waziri (anamtaja) kushinikiza tuuze, hapana haikubaliki, maana tutakuwa tumemsaliti Hayati Magufuli,” ameeleza mmoja wa wanachama.

Mmoja wa wanachama ambaye miaka ya nyuma aliwahi kuwa Mjumbe wa Bodi ya SHIRECU kwa sharti la kutotajwa jina amesema kitendo cha Waziri kushinikiza kuuzwa kwa maghala hayo ni hujuma ya waziwazi ya kutaka kukiua Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Shinyanga.

Amesema haiwezekani Waziri ambaye Serikali anayoitumikia kila siku inahimiza kuimarishwa kwa Ushirika hapa nchini, leo awe ndiye mtu wa kati kutaka kuuzwa kwa mali ambazo Rais wake aliyepita alizikomboa kutoka mikononi mwa mabebari.

“Nimeshangazwa na taarifa hizi, ninaungana na wajumbe wa mkutano mkuu wa SHIRECU kupinga suala hili, maghala haya kwa sasa ni LULU ya SHIRECU, mpangaji anayetaka kuyanunua anawalipa takribani milioni 900 kwa mwaka, leo ameona yana faida gani ili yeye ayanunue kabisa?”

“Viwanda viwili ambavyo anataka kuvitoa kama bei ya kununulia gharama zake ukichunguza ni sawa na fedha ya pango kwa miaka miwili. Naamini baada ya kuona kuongezeka kwa mahitaji ya maghala katika eneo hilo baada ya Serikali kuboresha bandari yetu, ameona uwepo wa hitajiko kubwa la maghala na kutaka ayanunue,” ameeleza.

Amesema yeye binafsi anashangazwa na kitendo cha Waziri kushinikiza kuuzwa kwa maghala hayo kwa bei ya hasara wakati kwa mujibu ya uthamini uliofanyika hivi karibuni ilibainika kwa sasa yana thamani ya shilingi bilioni 13.300 thamani ambayo hailingani hata kidogo na malipo ya yanayotaka kutolewa ya viwanda viwili vya kuchambulia pamba.

Ameendelea kueleza kuwa kibaya zaidi pamoja na SHIRECU kutakiwa kupewa viwanda viwili vya kuchambua pamba bado watatakiwa kuvifunga katika majengo yao ya zamani ya Uzogore ha Kishapu kwa gharama zao wao wenyewe kitu ambacho kitaongeza gharama zaidi kwa Ushirika.

“Hali ya kibiashara kwa sasa kwenye zao la pamba imeporomoka sana, kiasi hata baadhi ya wanunuzi binafsi wa zao hilo wameanza kuachana na biashara hiyo maana bei ya pamba inazidi kuporomoka kwenye Soko la Dunia.

“Pia hata thamani ya viwanda viwili wanavyotaka kupewa SHIRECU kama malipo ya kununuliwa kwa maghala yao ni sawa na kodi ya pango ya miaka miwili wanayolipwa kwa upangishaji wa maghala hayo kwa hivi sasa, hii ni kichekesho na sijui kama Waziri alitafakari haya!!” ameeleza.

Mjumbe mwingine wa mkutano mkuu huo kutoka Chama cha Msingi cha Ushirika Mwongozo Amcos ambacho ni mwanachama wa SHIRECU Kwiyolecha Nkilijiwa amesema kitendo cha SHIRECU kutakiwa kuuza maghala hayo ni sawa na kumsaliti Hayati Rais John Magufuli.

“Haya maghala miaka ya nyuma tuliyapoteza baada ya waliokuwa viongozi wetu kuyauza kwa njia za “kinyemela” bahati nzuri Hayati Rais John Magufuli wakati wa utawala wake alisimama kidete na kurejesha mali zote za Ushirika zilizokuwa zimeuzwa kinyume cha utaratibu ikiwemo Nyanza kule mkoani Mwanza,” ameeleza.

Amesema maghala hayo kwa hivi sasa yamebaki kuwa tegemeo kubwa kwa SHIRECU kutokana na kuchangia asilimia 75 ya mapato ya Ushirika na kwamba iwapo yatauzwa basi itakuwa ni kuichimbia shimo kubwa SHIRECU na huenda ikatangazwa kufilisika rasmi.

Alisema kutokana na umuhimu huo, kwanza kwa kuendelea kumuenzi Hayati Magufuli lakini pili maghala hayo kwa sasa ndiyo tegemeo pekee la uhakika wa mapato ya SHIRECU wanachama kwa kauli moja wamekataa yasiuzwe hata kama patakuwepo shinikizo lolote la Serikali.

“Kwa sasa kuyauza maghala haya ni sawa na kutaka kuiua kabisa SHIRECU, tumekataa kwa nguvu moja na badala yake tumeomba pafanyike uboreshaji kwa kuongeza majengo mengine, haiwezekani kitu kinachotuingizia zaidi ya shilingi milioni 900 kwa mwaka tukiuze kwa bei ya kutupa,”

“Huyu mnunuzi anayeshinikiza tumuuzie hayo maghala inasemekana ndiye mpangaji wetu kwa sasa ni wazi ameona kuna faida kubwa pale akiyamiliki moja kwa moja yeye, na jambo la ajabu eti tunashauriwa badala ya kupokea fedha taslimu tupewe viwanda viwili vya kuchambua pamba, pamba yenyewe kila siku inapoteza soko,” alieleza.

Chanzo cha ambacho kimewai kushika moja ya nafasi za juu ndani ya SHIRECU (jina linahifadhiwa) kimethibitisha kukataliwa na wanachama ombi la kutaka kuuzwa kwa maghala hayo ya Kurasini ambapo amesema Bodi imetakiwa kuhakikisha wanajenga majengo mengine katika eneo hilo kuongeza wigo wa uwekezaji.

“Ni kweli moja ya agenda iliyowasilishwa kwenye mkutano mkuu wetu hivi karibuni ilikuwa ni suala la kuuzwa kwa maghala yetu yaliyoko kule Kurasini jijini Dar es Salaam, hata hivyo kwa kauli moja wanachama wote walipinga na kuagiza maghala yasiuzwe kwa vile kwa sasa ndiyo chanzo kikuu cha mapato ya Ushirika,” ameeleza

Amefafanua, kwamba hivi sasa maghala hayo yanawapatia kiasi cha shilingi milioni 900 kwa mwaka kama kodi ya pango na kwamba viwanda hivyo viwili vya kuchambua pamba wanavyotaka kupewa na mpangaji wa sasa kama malipo ya ununuzi ni sawa na kodi ya miaka miwili anayowalipa.

Hata hivyo habari za udadisi ambazo bado hazijathibitishwa rasmi, zimedai kuwa Waziri anayedaiwa kuratibu mpango huo yupo Shinyanga akiwa katika jitihada za kushawishi mpango huo ukubalike ambapo inasemekana wajumbe wa Bodi ya SHIRECU wanadaiwa kuitwa kwenye kikao cha dharura ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Kufuatia hali hiyo baadhi ya vyanzo vinalihusisha suala hilo na msukumo wa rushwa katika hatua za uamuzi hasa baada ya baada ya wajumbe wengi awali kuonesha kutokukubali suala hilo, hivyo wanatoa wito kwa mamlaka za juu ikiwemo TAKUKURU pamoja na vyombo vya usalama kufuatilia kwa ukaribu suala hilo huku wakitoa wito kwa Rais Samia kulifuatilia kwa ukaribu zaidi suala hilo ili kuepuka utata unaoweza kujitokeza mbeleni.
 
Back
Top Bottom