Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,771
- 41,027
Na. M. M. Mwanakijiji
Wapo ndugu zetu kati yetu ambao wanapomwangilia Magufuli na utendaji wa serikali yake wanamuona ni mshamba aliyeula. Kwa kejeli zisizo kikomo na dharau zilizopitiliza wanaamini kuwa Magufuli hajachakaruka wala kujanjaruka kama wao wa “mjini”. Naomba kupendekeza kwako msomaji kuwa Jogoo wa Shamba anapowika mjini ujue wa mjini walishapoteza makeke yao. Kutawaliwa na kuongozwa na jogoo wa shamba manake jogoo huko kweli anawika! Aliyesema jogoo wa shamba hawiki mjini hajakutana na Magufuli bado.
Kwa muda mrefu Taifa letu limekuwa likiongozwa na kuendeshwa na watu ambao tuliaminishwa kuwa ni “wasomi” na “vijana wa mjini”. Walijua mitkasi, na madili yote ya mjini. Walijua nani wakuzungumza naye na ufanye nini ili upate nini. Walikuwa ni watu wa “madili madili” kwa vile wao ni wa mjini. Na katika makeke yao walijikuta wanatulisha maneno matamu ya ahadi zisizotimilika miaka nenda na miaka rudi. Hawa vijogoo wa enzi na zama hizo walinguruma mjini, hawakuulizwa, hawakubishiwa, walipoambiwa hapana walinuna, walipokaripiwa walijikunyata na kutaka wabembelezwe. Vijogoo hawa wa mjini walisumbua sana.
Miradi mingi ilikufa chini ya hawa “wa mjini”. Nani amesahau kufa kwa TRC, ATCL, UDA, na kuvurugika kwa makampuni mengi ya umma. Tuliambiwa kuwa sisi hatuwezi na hatuna uwezo wa kufanya lolote kubwa. Katika “kokolikoo zao” hawa walituambia kuwa ili tuendelee tunahitaji kubinafsisha kila chetu na kusubiri wajomba zetu toka majuu waje kutusaidia. Walituambia kuwa namna pekee ya kufanikiwa kama taifa ni kusubiri “uwezekaji kutoka nje”. Ndugu zangu, maisha na wa mjini hawa yalikuwa rahisi kwa sababu fedha zilikuwepo bila kuzitolea jasho, kila mjanja aliweza kupiga kama ana akili mbovu na hata walipokamatana walikamatana huku wanakonyezana!
Ndugu zangu, hawa wasomi wetu, waliojanjaruka waliliendesha taifa kama mifuko yao. Waliweza kupongezana na kupeana “hi” kama “elite” fulani. Sasa leo ametokea “mshamba” ambaye anawaendesha kama hawapo, wanaona huyu kweli “mshamba”. Wanasema hana “sophistication” za watu walioishi na kusoma majuu. Lugha ya Malkia haimudu na Kiswahili chake kimejaa lafudhi/lahaja nzito ya Kisukuma. Wanambeza, wanamdharau, wanataa watu wambeze na kumdharau. Kwa sababu hayuko kama wao. Wao wanaojiona ni wabora kuliko wengine.
Ndugu zangu, mambo ambayo Magufuli ameyasababisha – na nimeyaanisha haya mahali pengine – ni kweli kuwa hatuhitaji “waliojanjaruka” na “wa mjini” kutuonesha wapi tulikuwa tumekosea. Leo Watanzania wanajua kuwa nchi inaweza kwenda, kujijenga na kujiletea heshima bila hata kiongozi wao kila mwezi kwenda nje kuonesha sura yake. Yaani, huyu mshamba hakwenda kwa wakubwa kujitambulisha lakini nchi inakwenda vizuri na salama kabisa.
Ndugu zangu, nimewahi kujenga hoja huko nyuma kuwa mtu anaweza kumpinga Magufuli au sera za Magufuli; lakini ni makosa ya kihoja kujaribu kumshambulia mtu (ad hominem). Watanzania siyo wajinga au siyo kwamba hawaoni. Wanaona kinachofanyika na wanaona kile ambacho Magufuli anakifanya kwa ajili yao. Watu wanauona huo “ushamba” wa serikali ya awamu ya tano. Hawa “washamba” wanapofurahia yanayoendelea basi tujue kuwa jogoo wa shamba kweli anawika mjini.
Ndugu zetu wanapojitutumua kuonekana na wao wana sauti za kuwika wajue tu kuwa kuna vijogoo na majogoo; lakini sehemu nyingine yupo jogoo mmoja. Huyo akiwika wengi wote wanabakia kimya au wanawika kichini chini.
Salama kutoka kwa Mshamba Mwanakijiji kwenda kwa Washamba wengine…
Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com