Tujikumbushe
Tuesday April 14 2020
Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania imesema uchunguzi wa uraia wa baadhi ya watu wanaotiliwa shaka unaendelea kufanyika na ni mgumu
Uhamiaji wataja "ugumu" uchunguzi wa uraia wa Nondo, Eyakuze
N SUMMARY
Baadhi ya watu wanaochunguzwa uraia wao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze; Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe na mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo, Abdul Nondo.
Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania imesema uchunguzi wa uraia wa baadhi ya watu wanaotiliwa shaka unaendelea kufanyika na ni mgumu.
Baadhi ya watu wanaochunguzwa uraia wao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze; Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe na mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo, Abdul Nondo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Aprili 14, 2020 msemaji wa Uhamiaji, Paul Msele amesema bado idara hiyo inaendelea kufanya uchunguzi kwa kuwa kuna mambo mengi ya kuchunguza na wakati mwingine wanahitaji kuvuka nje ya mipaka ya nchi.
"Uchunguzi wa uraia ni mgumu sana wakati mwingine unahitaji kutoka nje ya mipaka kutokana na aina ya familia mtu aliyotoka na kuna vitu vingi katika kuchunguza uraia wa mtu,” amesema Msele.
Eyakuze aliingia matatani Julai 2018 ikiwa ni siku chache baada ya taasisi anayoiongoza kupewa barua na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), ikitakiwa kujieleza kwa nini isichukuliwe hatua kwa kutoa utafiti bila kibali.
Utafiti huo ni ule wa sauti za Wananchi ulioonyesha umaarufu wa baadhi ya viongozi umeshuka.
Mwingine ni Askofu Kakobe ambaye wakati wa sherehe za Krismasi mwaka 2017 alisema kanisani kwake kuwa ana fedha nyingi kuliko Serikali.
Siku chache baadaye aliyekuwa kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Charles Kichere alisema kuwa Kakobe hayumo kwenye kumbukumbu za ulipaji kodi wa mamlaka hiyo.
Mwezi Aprili, 2018 aliitwa na Idara ya Uhamiaji na kuhojiwa kuhusu uraia wake.
Naye Nondo alihojiwa na maofisa wa Uhamiaji wakati kesi yake ikiendelea Mahakama Kuu. Katika mahojiano hayo, Nondo alitakiwa kupeleka vyeti vya kuzaliwa vya wazazi wake pamoja na vya bibi na babu zake wa pande zote.
Kabla ya kuhojiwa, Nondo ambaye kipindi hicho alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alikamatwa na polisi mjini Mafinga, wilayani Mufindi, Iringa na kufikishwa mahakamani akidaiwa kuidanganya polisi kuwa ametekwa.
Source : Gazeti la Mwananchi