hii story imeishajeishaje mbona sielewi?.
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ndugu zangu bila shaka mwenyezimungu anaendelea kutupigania hadi sasa.
Ndugu leo naona nilete story kidogo kuhusu safari yangu moja hivi nchini DRC mikasa na visa mbali mbali kwa kipindi chote cha safari wakati napambana na maisha kwenye udereva ili niweze kuishi kama mnavyojua maisha ni popote na kujaribu ni muhimu kuangalia kila sehemu ili uweze kutoka ukinzingatia kuwa wengine shule yetu ni kidogo hivyo ni muhimu kijipambania kwa kila hali ili uweze kujikimu kimaisha tukawa tunashike hili na lile ili mrasi tuweze kuishi.
Story yangu ni ndefu kigodo ila ntajitahidi niimalize kwa wakati ili kuepuka zile maneno za kakimbia sijui nini ila naomba tuwe na uvumilivu tu kwani swala la kuandika nalo ni mtihani ukizingalia device tunazo tumia sio rafiki .kwa wale wasio wavumilivu naomba tupite tu hakuna haja ya kulalamika.
Story inaanzia hapa...
Miaka 2000's kulitokea wimbi kubwa la usafirishaji wa magari kutoka bandarini Dar kwenda DRC kipindi kicho ikitwa congo (kama sijakosea) kipindi hicho nilikuwa najishughulisha na udereva taxi pale Mapambano kijitonyama nikipindi ambacho biashara ya taxi ilikuwa na hela kiasi kwani biashara ya Bajaji na bodaboda ilikuwa bado na watu walikuwa hawajazoea kupanda vyombo hivyo, basii maisha yakawa yanasonga mbele kama sijasahau mwishoni mwa miaka ya 2001 ndo vita congo ilikuwa imepowa japo nilikuwa siwahi kufika huko hata mara moja.
Kijiweni kulikuwa kuna mshikaji alikuwa anaitwa Rama kwanza nikili kuwa huyu jamaa alikuwa mjanja kupitiliza na alikuwa anasafiri sanaa inasemekana hata nganda alikuwa anabeba japo tulikuwa wote pale pale kijiweni nae ana kigari chake mwenyewe anabeba abiria ndipo akanipa mchongo wa kusafiirisha magari ya wa kongo kwenda Congo kipindi hali haikuwa nzuri kwakweli hivyo madereva wengi walikuwa hawapendi kwenda huko japo wacongo walikuwa wanapanda offer ya mpaka dolla 250 kuifikisha gari KASUBALESA boda ya Congo na zambia then unamwachia anamilizia kipande chake.
Hapo ndipo jamaa yangu Rama alipopata hiyo fursa kwa jamaa yake alieoko pale bandarini ambae alikuwa na kampuni yake ya clearing na fowarding pale bandarini na kumwambia kuwa kuna wacongo wanahitaji magari yao yafike lumbumbashi then wao watayasafirishi kwa ndege kwenda kinshasa ila wao hawapandi hizo gari wao tutakutana lumbumbashi sehemymu moja sehemu moja kunaitwa KOTA naona nikaribu na soko kubwa la Lubumbashi mjini katikati.
Cha ajabu jamaa walitoa pesa yote kwa jamaa yao wa pale bandarini na kampuni ndo ilitakiwa isimamie kila kitu hapo ndipo mwanangu Rama akanitustua nakumbuka ilikuwa ni kati ya mwezi wa tano kwenda wa sita. Mvua zinanyesha Dar hakuna mfano abiria hakuna nikaona bora nitoe gari kwa jamaa nikimbize IT kwanza nami nipate uzoefu.
Baada ya jamaa yangu kuweka mambo sawa ikiwemo kupata passport ya karatasi na chanjo ya homa ya manjano mzes mzima siku ikawadia jamaa yule akatupa dolla 100 advance, 50 maillage na 50 ya barabarani nikiongea bararani mnilewe hiyo ya wazee .Gari mpya kutoka kiwandani yani bado zina makaratasi mitusubishi dabo cibin mpya kabisa wazee tukawekewa full tank. Zikabandikwa number za IT .siku ya j2 ndo safiri ikawa imeanza rasmi mara ya kwanza kusafiri na magari ya IT ila mwenzangi rama yeye alikuwa mzoefu hata kwa njia hio pia alikuwa anaijua vizuri na alikuwa anajua hata kizambia kidogo na kikongo kisawahili chao kile cha kuya Papa uko na makuta ngapi? Hhhhaaaa...
Safari imeanza.
ITAENDELEA JIONI...
Inaendelea sehemu ya Pili.
Kwanza nikili tu kuwa sintojibu comments za watu ntakuwa straight moja kwa moja kwenye story yangu.
Haya basi tuendeleee safari ikawa imeanza alfajiri ya j2 ile wanaume tukaanza kupiga gia kwakweli mwendo wa magari ya IT si wa mchezo kumbuka kesho tumeshaambiwa ifikapo jumanne asubuhi tunatakiwa tumeshavuka boda ya tunduma upande wa pili NAKONDE kuna mizigo pale tunatakiwa tubebe ya wale jamaa imeachwa pale na bus la TaQwa .wazee tukaamsha mashine kama unavyojua gari ikiwa mpya ni kutembea tu mwanzo mwisho...
Jamaa yangu Rama alikuwa mzoefu wa njia check point za maaskali na tochi zinapokaa hivyo ilibidi mimi nikae nyuma yake akiaamsha nami naamsha akipunguza mwendo nami napunguza na kweli bwana mbele unakuta wazee na vitochi vyao wanaomba document na hela ya soda sisi tunachapa mwendo saa nne asubuhi tukanywa supu msamvu-morogoro tukafungasha nyama choma pale duma mwendo hapo sasa speed ikawa ni noma yanii jamaa yangu Rama anakimbia hadi naogopa aise .
Basi mwendo ukawa mwendo kweli kweli pia usisahau abiria tulikuwa tunabeba wa hapa na pale ili kupata kusave angalau kale ka hela ketu kasiishie njiani saa mbili usiku tunaingia Mbeya aise kama sijasahau tukapata hotel pale mwanjelwa sehemu safi tukapaki magari yetu lodge tukala tukalala mapema ili asubuhi tuwahi Tunduma ili tusubiri bus la Taqwa tuchukue mizigo yetu.
Tukalala pale kila mtu nachumba chake kama kawaida Rama akawa na mchuchu wake pale chumbani sijui alikomtoa ila mimi nilivyochoka hakika sikuwa hata na hamu ya demu mzee nikaangusha mapema saa kumi na mbili asubuhi tupo kwenye chuma zetu tunaitafuta Tunduma taratibu kama kawaida tuna vichwa vyetu viwili vitatu .
Saa tatu tupo Tunduma tunakunywa supu tukaonana clearing wa jamaa akafuta bond na kuclear baadhi ya document sisi tukawa tunasubiri mizigo japo jamaa alitutaka tuvuke siku hiyo hiyo upande wa pili lakini tulikata tukamwambia tutasubiri hapa hapa mizigo. Saa nne taqwa ikaingia tukaenda chukua mizigo tukapakia kwa gari mizigo yenyewe ni makapeti ya nyumbani tukafunga vizuri kabisà tulala .
Mapema asubuhi tukaamka tukaka kwenye foleni ya kuvuka boda baada ya kugonga passport zetu kufikia saa nne tukawa tumevuka boda ya tunduma tupo Nakonde jamaa yangu akanishauri tupumzike ili tutembee usiku lli tusipisha na maroli pia kuna kuwa na atuluvi hivyo akashauri tukapumzike mahala jioni ndo tuamshe .ikabidi nimsikilize tukaenda eneo pale pale boda ukiwa pale nakonde unaweza dhai upo tanzania kumbe ni upande wa zambia yani kunamchanganyiko wa wabongo na wazambia kibao.
Saa kumi na mbili tukaamsha aise sikujua.kumbe Zambia kubwa aise tulitembea giza likaingia aise unatembea kilomita hata mia hupishani na gari lolote halafu pori tupu.
Nyie tukafika kwenye kimji fulani kinaitwa SELENJI tukapaki hapo ili tule na tupumzike ebwanae kulala huo mji ni bora kulala kwenye gari kuna baridi seleenji njombe ikasome tukala pale kwenye hotel ya wasomali tukapaki na magari yetu pale tukalala pale asubuhi mapema bila hata kuoga tukaamsha mapema hapo ndipo nilipo anza kuona usumbufu wa askali wa zambia aise mnasemaga askali wetu wetu wanapenda rushwa nenda zambia yani gari mpya anakwaMbia kosa lako gari ni chafu gari hiyo ipo transit aise yote umwachie hata kwacha elfutano tu aise jamaa wana njaa sijapa ona.
Tukawa tunaitafuta mji wa KAPIRI MPOSHI hapo unajionea watu wana uolima aise kule jamaa wanalima serious sijui kwanini kuna njaa namna ile ...zambia kupata wali maharage ni ishu.
Kama sijasahau kutoka selenji kuna mji unaofuata pale unaitwa MPIKA ( mtanikumbusha kama ntakuwanimesahau) aise kile kipande ni hatari kutembea asubuhi sanaa au usiku kumbe wanapiga mawe hatariii wazambia ni washenzii.
Itaendelea.....soon.
Inaendelea sehemu ya tatu ..
Basii safari ikaanza asubuhi na mapema aise hapo tunaitafuta MPika hapo Rama anaamsha mashine vibaya nami nipo nyuma yake ,kama unakumbuka aliniambia nikiamasha nawe amsha hakuna kuniacha hata kwa mita ishirini chuma zinatembea baridi kali unawasha heater ya gari lakini wapi baridi inapenya hadi kwenye vitundu vidogo vya madilrisha aise selenji hapana si kwa baridi ile
Baada ya mwendo kama nusu saa hivi karibia na kilima kwenye kona nilishuhudia kitu cha ajabu sanaa kinatokea angani upande wa kulia kwanza mimi sikutambua chochote niliona mfano wa kimombo hivi unaanguka kutoka juu kuja chini kumbuka mimi nipo nyuma ya Rama chuma tumeziachi la vibaya yani hata mashimo tulikuwa tunafukia kumbe bwana rama ile michezo ya wazambia kurusha mawe anaijua ndo maana aliniambia nikitoka speed nawe kanyaga mafuta hadi mwisho kumbe garii ikiwa speed kukadiria uangushaji wa jiwe kutoka kilimani unakuwa mgumu kwani speed ya gari na jiwe unakuwa tofaouti sasa hakuniambia ila baadae aliniambia ningekuambia ungejawa na hofu hivyo ungepoteza comfidance ndo maana akakaa kimya kwani matokeo hayo huwa hayatokei mara kwa mara huwa wanakuwa na timing ya wa watu wao kutoka boda kuwatonya na ndo maana kule boda jamaa alivyotwambia tuvuke boda j3 Rama alikataa akataka tuvuke j4 tu kama tulivyokubaliana ,ndugu tembea uone yani unakuta jitu lipo customer pale na tai shingoni na simu kubwa kumbe ni informer wa majambazi njiani.
Sasa tuongee kidogo kuhusu huu uhuni wa kurusha mawe kwenye hicho kipande kuna vishimo vishimo hivi sasa kama wewe mgeni unapofika lazima utembee mwendo wa wastani sasa ukitembea mwendo huo ndo unawapa mwanya wale wezi kukurushia jiwe kubwa zaidi mara nyingi huwa hawakosei lazima likupate kama kawaida ukipigwa lile lazima uyumbe utasimama tu hapo hapo waliochini wanakuvaa unaporwa kila kitu na hata kukua hapo hapo barabarabi ndani ya dakika hilo gari linabaki na chasisi wanang'oa kila kitu.na maeneo hayo machuma ya magari kibao yaliyoungua moto.
Basi bana tupo mia ishirini fukia shimo likarushwa jiwe mara gafla nikaona kama Rama anatoka barabarani gafla kwa speed kali yani akawa anaendesha gari kwa pembeni huku anapiga honi kali kumbe ananipa ishara nami nitoke katikati ya barabara niendeshe pembeni mara ya kwanza nikajua labda anasinzia likini alivyozidi kukaa pembeni bila kuingia polini akili kengere ikalia kichwa ni nikakumbuka rama aliniambia kila nachokifanya nawe nifuate hivyo nami nikatoka road nikawa upande wa barabara pembeni barabara za zambia nyingi ni pana sanaa nikaona ameacha kupiga honi sasa mara nikaona jiwe kubwa kwa mbele linakatiza ktk ya barabara mara ghafla rama akarudi road chap chap nami nikarudi chap jiwe litapita vuuuupp niseme tu ukweli lile jiwe ni kubwa na kama lingetupata hiyo gari haiwezi kuwa gari tena sasa ngoma hapo niseme tu ukweli sijawahi kukimbia na gari katika maisha yangu kama tulivyokimbia kile kipande cha selenji - Mpika tulikimbia na zile gari yani kama tupo kwenye mashindano hapo uoga wote umeisha yani unaona kama umenusurika kifo kwente tundu la sindano.
Tukaendesha kwa speed kubwa sanaa tunakaribia mji wa kapili mposhi ndo nikaona rama anawasha indicator kuonyesha ishara ya kusimama pembeni mwa barabara tukapaki hapo mzee tukapumzika kidogo ndoa akawa ananipa story ya lile eneo aise kwa kweli niliogopa sanaa mbaya zaidi akaniambia alishampotezaka rafiki yake eneo lile na mbaya zaidi wale wezi baada ya kulipiga gari walimchoma moto ndani ya gari ili ionekane ni ajari tu ali kupoteza ushahidi aise kwakweli niliogopa sanaa ila Rama alikuwa jasiri aise usiombe, akagundua hilo akanipa moyo na maneno ya ujasiri ya hapa na pale tukatulia tukaanza safari ya kuukaribia mji wa wa kapiri mposhi saa nne asubuhi hiyo tukafika kwa mama msomali tukaagiza wali na nyama tukala unajua ukiwa mgeni wa safari unaweza dhani watu wanakosea kupika kumbe zambia wakipika waLi badala ya kuweka chumvi wao wanaweka sukari aisee nilishanga sanaa nikamuuliza rama akaishia kucheka na kunitania vijimaneno vya hapa na pale ..tukacheka pale akaniambia nimfuate tukapaki magari yetu maeneo hayo hata maroli huwa yanapaki akampa.kijana moja kwacha kidogo naona nikijana wa mama wa hotel wa kisomali akaniambia nimfuate nikamfuata tukavuka barabara hadi nyuma ya msikiti ndo tukamkuta mzee moja akamsalimia kumbe wanafahamiana akumuomba tuoge tukaingia pale bafuni zipo nyingi tukaoga safiii kabisa tukarudi kujipumzisha pale hotelini rama ananiambia safari tunaendelea saa nane mchana sasa tutulie tu tuzicheki cheki chuma kutoka pale hotelini mbele kidogo kuna shell mara nikaona kuna jamaa wawili wanakuja na madumu ya mafuta petrol sijui walitokea wapi rama akaniambia hao ndo tulikuwa tunawasubiri tukajaza mafuta tena top zile gari unajaza full tank halafu inakijitank kingine pembeni cha akiba mafuta ya kiisha unabonyeza batani u akitumia kama dharura unaweza tembea kilomita hata 50 .
Basi kufika saa nane safari ikaanza mdogomdogo rama mbele mimi nyuma tunauacha mji wa kapili.mposhi taratibu speed ya wastani tukachapa gia hadi njia panda kuelekea njia kuu ya Lusaka na boda ya LUBUMBASHI-ZAMBIA wanakuita KASUBALESA. Yanii hapo ndo safari yetu ilitakiwa iishie kulingana na makubaliano ya awali ila wakati tunafika boda kukutana na jama mpokeaji tukalizimike kuambiwa lazima tuingie lumbumbashi kabisa waliotakiwa kuja wameshimdwa kutokana mapigani ya waasi katikati barabara kuu ya lumbumbashi Tobaaa nyongeza dola 75. Mara ya kwanza nilimbishia sanaa Rama tuachane na huo mpango lakini Rama aligoma kabisa lazima atoboe hata kama vipi pale kuna kama 12okms hivi ntaelezea mbele nini kilitokea pale boda hadi mimi na Rama tukataka kuhitirafiana nafsi ilishahisi hatari mbeleni..tuendelee.
Na safari yetu tukakunja barabara kuu tukawa ndo tunaiacha kapili mposhi rasmi hapo tunaitafuta barabara ya kuu ya mwelekeo wa mji wa NDOLA nyiee ukifika ndola unaweza dhani upo masaki ni kamji kadogo kazuri sanaa halafu wageni wengi na supermerket kibao aise tukapita pale jamaa akaniambia tuchepuka barabara kuu twende ndola kidogo tukasuuze macho wenzetu wazambia namba za IT Hazina shida ukichepuka barabara kuu tofauti na sisi yaniii utoke bandarani na namba za IT wende masaki kutoka barabara kuu . lazima njau wakudake zambia unaweza tembea na namba zai IT mtaani hata siku mbili mle mle ndani...
Basi tukaelekea ndola bana huko tulienda kusuuza macho tukakaa kama masaa mawili tukarudi njia kuu kuelekea boda kuna sehemu kunaitwa CHILABOMBWE kilomita 30 kutoka boda rama alifanya kitu ambacho kilinifanya hata mimi nianze kumuogopa aise .....wakati tunaendelea na safari taratibu nikashaanga kuna mtu katokea tu polini ghafla kuna mtu karukia nyuma ya gari la Rama nikampigia honi...rama badala ya kupunguza mwendo yeye akaongeza kumbuka tuko porini hapo na tulikuwa mwendi mdogi wa wastanii kabisaa..
Itaendelea ......
Inaendelea sehemu ya nne...
Ndugu nilikuwa napata Iftari kidogo nikawa nimesitisha kidogo kuandika kama mmnavyojua bado tuko ndani ya mwezi mtukufu wa ramadan ishallah tunaendelea kuwa pamoja .
Naomba nishauri kitu kimoja kwa wafutiliaji wa hii story ndugu ili uweze kusoma kitu na kujifunza au hata kupata burudani ni vyema ukapata story hiyo kwa hatua ili nawe uweze kutafakari mafunzo yaliyomo ndani yake hivyo basi kwa wale ambao wanafikiri kuwa kuandika tu story mwanzo mwisho ndo ujanja basi hakuna sababu ya kuifuatilia hii story mpite tu .kama nilivyosema mwanzo lazima niimalizie yote .
Twende kazi sasa wakati jamaa yule aliedandia pale nyuma anaendelea kuhangaika pale juu mara paapp akateleza bwana hadi chini kama unajua tulikuwa tumepakia mazulia na mahema ya wale jamaa nafikiri aliteleza kutokana na utelezi wa zile turubai aise jamaa akaanguka mzima mzima hadi katika ya lami mimi niko nyuma nikamkwepa kwa pembeni nikawa niko upande wa kulia cha kushangaza yule jamaa kumbe wakati anapanda alikuwa na simr anajaribu kutoboa zile turubai ndo kushikashika akajikuta ameteleza hadi chini.
Aise ghafla tu nikashangaa rama amesimama na akapiga revasi akarudi nyuma kumlenga yule jamaa pale chini na kumgonga kwa nyuma yanii gari ikapita juu yake yote halafu akarudia tena kwa mbele halafu akatoa kalele na vishindo vya maumivu ya yule binadamu nilivyokuwa navisikia nikiwa kwenye gari aise mwili mzima ulinisisimka yani unaona kabisa binadamu anamuua binadamu mwenzi wazi wazi tena kwa kumfinyanga na gari kwa maksudi kabisa nikiwa naangalia kwenye site mirror rama akanipa ishara ya tuendelee na safari tukaenda kidogo hadi mbele kama kilometer tano tukapaki akatoa maji ya chupa akaanza kusafisha damu kwenye plate namba na maeneo mengine ya mbele na nyuma hakika chini gari ilijaa damu tupu baada usafi tukaendelea na safari..
Mpaka boda hiyo saa kumi na moja ndo tumefika boda KASUBALESA.
Turudi nyuma kidogo pale jamaa yangu alipoua mtu.....tulivyofika boda
Rama ananihadithia kwa kunionyesha kovu upande wa kushoto wa jicho lake na kuniambia kovi hilo alolitoa hapo wakati akiwa tanboy wa magari makubwa alikuwa akifika maeneo hayo basi dereva anamwambia apende juu na panga kulinda wezi maeneo hayo kuna kilima flani hivi ambapo gari kubwa ikifika lazima ipande taratibu hivyo hao wezi walikuwa wanatumia mwanya kukata turubai na kuvunja kufuri kuiba bidhaa mbalimbali zinaelekea congo na humtanguliza moja akifanikiwa kukudhibiti linatokea kundi la wezi polini linakomba kila kitu unaambiwa vikundi hivyo hufadhiriwa na wafanyabishara wa mji mdogo wa Ndola kuiba na kwenda kuwauzia wao bidhaa za wizi kwa bei ya kutupa.
Sasa rama anahadithia kuwa kipindi gari lake lilivyofika tu pale yeye akakwea juu kama kawaida kumbe alikuwa na usingizi, kijiusingizi kikampitia bwana njemba ikapanda kustuka njemba ipo juu nae yupo juu ndo mapambano yakaanza lakini pamoja na kumshinda alimwachia majeraha kadha a yaliyomweka hospitali week nzima ndo akajiaza kuwa iwe isiwe siku ikitokea maeneo hayo likatokea tukio lolote likamuhusu lazima alipize kisasi na ile ndo akawa amelipizia kisasi siku .
Sasa tupo boda tunafanya mawasiliano.na wenyeji tumefika boda waje wachukue mzigo wao sisi tugeuke .maboss kubigiwa simu kuambiwa gari zao zipo salama wakafurahi sanaa wakaagiza kwa jamaa yao moja anauwezo flani pale kwa boda atuchukue kwake tukale na kulala yule jamaa akaja mpaka tulipo tulikopaki magari yetu boda na askali akapewa chake alinde magari ,sasa pale kuna
Askali analipwa na boda lakini usipompa chochote unaweza ibiwa na ukienda kulalamika hakuna wa kukusikiliza watu wako busy aise. Tukaenda kulala kwa ajili ya kuwa asu uhi kuonana na wenyeji wetu tuwakabidhi mali zao sisi turudi zetu home. Tukawa tunasikilizia pia lile tukioa la kuua kule. madereva wakija wanatoa taarifa ya maiti kwa askali sisi tukawa tunasikilizia tu hadi tulipochukuliwa na jamaa kulala hadi kesho.
LEO TU NIMEWEKA EPISOD NNE NAOMBA KWA USIKU NIWAACHIE HII NIPUMZIKE KESHO TUTAENDELEA NA ZINGINE ISHALLAH HADI TUMALIZE
Inaendeleaa sehemu ya tano....
Haya wandugu sasa tuendelea na kipindi hiki cha kutafutia usingizi naamini mlikuwa mnanisubiri kwa hamu japo afya bado mgogoro kidogo...
Kwanza niwashukuru wote mlionipa pole asanteni na mungu awabariki wote mnaocoment na wala ambao mnachungulia kiaina uzi ...
Sasa tuendelee .. giza likaingia mwisho kukakucha mapema tupo kwa jamaa japo nililala chumba kimoja na rama lakini nilivyoamka sikumuona ila mabegi yetu yapo chumbani nikajua tu huyu amedamka kumbe mpuuzi huyu kanikimbia usiku mwingi sanaa kwenda kutafuta mabibi huko aise yani ugenini lakini bado unaonyesha uhuni wako shukrani chumba tulichopewa ni chumba cha njee tena kipo karibu na barabara kabisa yanii ukifungua mlango tu upo barabarani ..duuhh .
Nikaamka ila aise nilikuwa na uchovu wa kufa mtu nilitamani nilale hadi saa sita lakini ikawa haiwezekani mtu mzima nikaamka nikajiweka safi nikatoka nje nikawa nimekaa tu kwenye jiwe nje ya chumba na msikilizia rama kama atakuja unajua miaka ile simu ilikuwa ishu ni watu wachache walikuwa na simu ila rama alikuwa nayo ya alcatel kubwa kubwa hivi ndo alikuwa anatumia kufanya mawasiliano njia nzima na jamaa wale .
Sasa kwakuwa sikua na simu nikawa nimetulia nasikilizia na kweli saa moja kamili jamaa akafika ameongezana na yule mwenyeji wetu cha kushangaza kanisalimia tu na kuniomba passport sasa nikajiuliza huyu vipi pass yangu ya nini tena mbona kazi imeishia hapo nikaona nisilete ujeuri mbele ya mwenyeji nisije onekana mkorofi labda kuna mambo anaweka sawa ili tukabidhi mzigo tusepe nikamkabidhi likawa kosa .
Akasema dogo nisubiri hapo akaondoka na yule jamaa wakakaa kama nusu saa hivi akarudi pekee yake akanikabidhi pass yangu kuangalia mama yangu kucheki imeshagongwa tayari muhuri wa zambia na congo tobaaa kwanza nikamshangaa nikamuuliza sasa ndugu si tunaishia hapa akajibu tena simple tu dogo tunatoboa hatuwezi acha dola 75 kwa kilomita 100 jiandae twenzetu wanaokuja kupokea haya magari wameshindwa jana zilichapwa njia ya kuu ya lubumbashi hivyo hawawezi kuja tumeambiwa tumalizie kazi aise nilimuangalia rama kwa hasira iliyochanganyika na hofu kubwa moyoni hadi nikajuta kwanini nimemsikiliza huyu kichaa tukaanza malumbano mle chumbani ya kwanini yeye anafanya mambo bila kunishirikisha yeye yupo kimya tu anapanga nguo zake hana habari anacheka tu .
Yani hakuna kitu kibaya kama kuongozwa na mtu ambaye hakushirikishi katika kuamua njia ipi upite yani kwanza njia huijui hujui unarudi vipi ? Pesa yote hujamaliziwa maboss wanamjua rama wewe hawakujui maanake rama ndo angenilipa.mimi sio wao nikatafakari sanaa nikasema ni kimbishia au nikiendele kuwamkaidi ntakosa haki zangu zote yani ataniacha na hela sintopata nikapiga moyo konde ngonja nione ila tukawa sasa tunatembea kuelekea kwenye gari lakini hatuongei yani tumenuniana yani jamaa ana roho ngumu vibaya .
Madereva wa maroli nauzoefu wao wote wa njia waligoma kuanzaa safari siku hiyo mpaka escort kutoka lubumbashi lakini huyu chizi analazimisha tutembee hivyo hivyo njia ambayo janaa yake tu usiku zimipigwa tena sio kupigwa tu askali wa congo walikimbia kabisa mapigano huyu mwehu analazimisha nikawa nawaza huyu jamaa ni chizi au ...
Ebwana baada ya kumaliza kuweka kila kitu sawa nafikiri sisi ndo tulikuwa wa kwNza kukaguliwa sikuona mtu pale custom anagonga nadhani walikuwa wanasikilizia kwanza .tukawasha gari tukavuka upande wa congo ila wakati tunakaguliwa macho ya wale jamaa custum ya zambia kama yalikuwa yanatuangalia kwa huruma vile yanii kama wanataka kuniambia jambo lakini wanasita.
Sasa ikawa ni zamu ya upande wa kongo , boda nzima imejaa wanajeshi tupu yani utafikiri vita jana ilipiganwa hapo wamechafuka vibaya yanii inaoenakana janaa walikuwa na shughuri nzito na kweli wakawa wanahadithia mapigano ya usiku wanaongea kiswahili chao kibovu lakini nikawa nawaelewa wamebeba silaha nzito za kivita hadi zile za kuchomeka kwenye gari nyuma.
Naomba niongee kitu.
Kuna utofauti mkubwa kati ya ujasiri na uoga unaweza ukawa commando au hata General lakini usiwe jasiri lakini unaweza ukawa mtu wa mtaani tu huna mafunzo hata ya mgambo lakini ukawa jasiri vibaya mno , na swala la ujasiri sio swala la kufundishwa ujasiri mtu anazaliwa nao akiwa jasiri na yale mafunzo ya sijui jeshi ,polisi sio ya kukupa ujasiri ni kwaajili ya kukufanya usiwe muoga fanyeni uchunguzi utakuja kukubaliana na mimi
Sasa wakati mimi sina hili wala lili akili.iko mbali sanaa hili.jamaa(rama ) linabonga tu na wala wanajeshi linapiga story linacheka vibaya tena kwa sauti tena wanalipa.kabisa bunduki linashika kama linalenga shabaha nao wanashangilia kama vile wamempata mwanajeshi mpya wa kujitolea aise.
Wakati tuka bado boda pale mimi sijui kinachoendelea na rama lipo kwa wanajeshi tena wameliweka mtu kati linapiga maneno kama lienyeji akaja mtu moja hivi dirishani kumbuka mimi nipo ndani ya gari nimejikunyata nasubiri kupokea amri kwa rama twende ama laa
Akagonga nikashusha kioo akawa anaulizia kuwa tunaenda lumbumbashi unajua pale mara nyingi madereva wa IT huwa wanakula vichwa vya abiria sasa nikamjibu ndio akaniuliza saa ngapi nikamwambi sii mda mrefu akaniambia yeye kaja janaa usiku hapo boda ni mfanya biashara ila njiani walikuta maiti nyingi za wanajeshi wamekufa na raia sasa iweje sisi tuharakishe kabla hali haijawa shwarii ? Ndugu zangu niseme tu ukweli nilihisi kimkojo kinanitiririka kwa mbali nikajaribu kuuzia lakini wapi hakuna kitu kibaya kama hofuu licha takuuzia mkojo lakini ulitoka.....mamaaee nikaon kifo hiki.
Itaendelea ..........ngoja niangalie beyhadh( chizi wa mapenzi ) nitarudi ishallah.
Inaendelea sehemu ya sita....
Nawasalimu ndugu bila shaka mnaendelea powa sasa baada ya mechi kuahirishwa hadi saa moja naomba tuendelee sasa .
Tumeshavuka boda tuko upande wa congo huku nipo kwenye gari nafanya mazungumzo na yule jamaa anaetaka lifti mimi sikuwa na chakuongezea tena nikamshukuru jamaa nikamwambia kuna mtu ndo mwenye magari kama atakuja ntamwambia kuna kichwa akikubali tukubebe ntakubeba usijali ila.usikae mbali sanaa na hapa mimi nikapandisha kioo nikaendelea kuwaza huku nawazua aise nikiri kuwa katika maisha yangu yetu siku ile ndo nilipa msongo mkubwa wa mawazo haijapata kutokea imagine nina dolla 130$ mfukoni lakini sio raha hata kidogo kipindi hicho hiyo pesa ilikuwa juu ukiabadilisha kwa madafu unapata hata kodi ya nyumba ya mwaka mzima na chenji inabaki.
Wakati naendelea kuwaza mara ghafla rama akaja akawa ananiongelesha kuhusu hali ilivyo njiani yani linaongea utafikiri lilikuwepo anasema sasa hakuna kitu askali.wa congo walisafisha njia hakuna tena wakutusumbua tusubiri tu maboss waje watupe hela sisi tutoboe halafu anaongea huku anacheka wakati huo mimi mawazo yapo mbali sanaaa.
Kuna kosa kubwa nilifanya pale boda wakati wa kumsikiliza yule jamaa anaetaka lifti nilimwambia kuwa tutaondoka pale mda si mrefu halafi nilivyocheki ila sehemu aliyokuwa aamekaa kwenye kibanda sikumuona yani alipopea ghafla sasa katika kumpa taarifa rama kuhusu yule jamaa ghafla akabadilika akawa ananilaumu nikashangaa kumbe huo ndo mchezo wao majambazi na na watekaji wengine wanakuwa na. informer wa vikundi vya waasi mfano MaiMai yani wanatengeneza mpango kuanzia boda ili kufanikisha utekaji sasa ukiwapa taarifa zako muda wa kutoka wanajipanga vizuri nakutoa taarifa kwa wenzao walipo polini katika ya poli huo ndo unakuwa mwisho wako .wazee wa tank za mafuta wanajua hii michezo , wajinga wanaweza teka tank zima likaingizwa porini wakanyonya disel au petrol yote na wakaichoma gari moto wakikusamehe mnaachiwa gari tupu sasa kimbembe kujieleza kwa majiri lokapu lazima ukae kwanza.
Basi rama akawa ananipa hizo story nikajua kumbe ndo maana jamaa alikuwa ananihoji maswali mengi sanaa kuhusu hata aina ya gari Unajua zile gari zilikuwa mpya tena na makaratasi yake bado hivyo nikawa nimeelewa sasa ghafla tu rama akatoka kidogo akarudi tena baada ya kama nusu saa akaniambia kijana umeshaharibu ratiba sasa ngoma hapa tunaondoka saa kumi jioni hela imeshatumwa na maboss customer kwa jamaa yao tukale tupumzike kidogo ila kuna askali miongoni mwa wale alikuwa anaongea nao pale boda wanataka lift hadi lubumbashi hivyo tutakuwa nao na sasa tumepata ulinzi wa chee
Ebwanaeee nikasema sasa naingia vitani bila kupenda yanii tupo na wale askali kwenye gari na mibumduki yao ile mikubwa mikubwa hivi tukifika katika polini wakatwambia simameni tuzipige kwanza na waasi tutakataa nikawa nawaza najiuliza sasa maisha yangu ndo yamefika mwisho ...
Wakati nawaza likaja roli la jeshi la congo pale boda likaanza kuwapakia askali kadhaa kwenye roli wakapanga mle walikuwa wengi takribani kama mia nakitu hivi wakapanda waliokuwa na rama kama 15 wakagoma wakasema wao wana gari za kupanda watangulie tu wao watakuja na sisi .
Yani lile roli limejaa matundu ya risasi ubavuni aise halafu hata vioo halina halafu kilichonifurahisha lile roli alikuwa anaenda mwanamke inaonekana ni shupavu kweli kweli , waozijua zile benz za mitairi mikubwa na mfano wa gari alilokuja nalo yani lile gari kwanza halina vishukio yani nikurukia tu na kushuka unaruka tu sasa yule dereva mdada lakini shupavu kweli kweli yani alivyokata kona kuingia boda nikasema labda mwanaume aise alifungua mlango akaruka kutoka juu hadi chini bila kuteteleka hata kidogo halafu yupo full combati chini na bastora na kisu kiunoni na bomu la granade, juu yule mdada alivaa tu kusinglendi cha jeshi ebwana ee yani niseme tu ukweli yule dada aliniongezea ujasiri yanii mwanamke kwanza mwanajeshi halafu katoboa katika njia chafu kama ile mimi kwanini niogope tena mtoto wa kiume lakini nafsi nyingine inaniambia huyo ndo kazi yake kazoea lakini kwakweli alinifanya mipate faraja ya japo nilimuona tu kwa mbali wala sikupata hata nafasi ya kuongea nae.
Naomba niongee kitu kidogo kabla sijaendelea kuna mdau kwa comment anasema askali.kukupa bunduki ushike shike ni ngumu sanaa nami nakubaliana nae kabisa ila sio askali wa congo kwa kipindi hicho yani wale sio askali ni washenzi yani yule ukashampa beer zile prisner mbili tu unaweza muomba bunduki ukaenda ukafanya yako ukarudi zako hamna askali mle labda sasa sijui nidhamu sifuri halafu kipindi hicho kumuona raia anatembea na bunduki tena zile raifo za masniper mtaani ilikuwa jambo la kawaida kabisa wala hakuna wa kumshangaa mwenzio.
Kama mnafuatilia taarifa kule GOma mashariki mwa DRC haya mambo yalikuwa yanaendelea hadi majuzi mwajeshi mzalendo wa kitanzania GEneral james Mwakibolwa alivyoenda kukomesha huu ujinga kupitia operation ya ondoa waasi wa waADf na wale waliokuwa wanapata ufadhiri kutoka serikali ya Rwanda mwanajeshi muasi kibaraka wa kagame sultan Makanga mpiganaji hodari wa vita ya msituni .siku moja ntaleta story nini alifanya kule mashariki mwa drc hadi wacongo wakiona siraha wanaikimbia kwa kifupi hii ni mbinu yakuchanganya jeshi la serikali yani waasi hugawa silaha kwa raia na kuwaambia wajilinde wenyewe hivyo huvichanganya vikosi vya usalama kujua muasi ni nani ?
Itaendelee....wazee sasa tumefika patamuuu urojo.iftar inakaribia karibuni.
Inaendelea bandugu .......
kwanza niendelee na msimamo wangu kuwa lazima niimalize story halafu hizi mambo za kuja inbox kuni criticise sio kabisa wengine naona mnakoment ujinga tu kama story ni chai kwanini unaifutalia?
Mh.rais Mama samia ana kazi sanaa asipowakomalia wabongo kama alivyokuwa anafanya magu nchi itamshinda yanii mtu anakaa anabisha jambo ambalo hata halijui vizuri kisa umesoma vijivitabu vya waandishi uchwara .
Kuna siku nilimuuliza mkongoman moja ni kwanini vita haishi kongo yeye akanijibu kwa kifupi tu. kwa sababu tumetanguliza maneno kuliko vitendo yani mkongo anaongea sanaa lakini kwenye battlefield anakimbia mbio adi waasi wanateka mji mkubwa kama Goma.
Haya sasa wakulungwa muda ukawadia mzee mzima chuma zikawashwa wale wanajeshi wakaanza kupanda magari yetu, walijinga vizuri kweli naomba nieleze kidogo kuhusu kujipanga yani ni hivi wanajeshi wakikaa kwenye gari huwa na mielekee minne yani kuna wanao angalia mbele ,pembeni ,nyuma na mbele na kila mwanajeshi anapewa siraha kulingana na uelekeo alipo yani kwa mfano mwenye RPG anakaa juu uelekeo wa mbele yani ina maana hiyo silaha huwezi itumia ukiwa juu ya gari halafu unaelekea kwa nyuma labda gari spesho unless unaweza enda nayo chini wakati wa kufyatua pale inapotokea dharura..
Wazee wakajipanga safari ikaanza kama kawaida rama mbele mimi nyuma yani wajinga wanapiga story gari ya mbele wewe unasikia huku nyuma yani ni makelele full yani kwa ujumla zile gari zilibadilika.zikawa kama mali ya jeshi vile Wazee tukazidi kukataa poli.
Mwanzoni nimesema kunatofauti mkubwa kati ya ujasiri na uoga yani mtu kuwa jasiri na kutokuwa muoga amini usiamini baada ya kama kilomita tano hizi zile kelele za wanajeshi zikaanza kupungua mara ghfla nikasikia mwanajeshi moja anasema attansio hii ni lugha ya kifaransa yani kwa kiingilleza nahisi alimaanisha attantion yani wajuvu wa lugha mtasaidia kidogo naamini ilikuwa ni kama tahadhari flani nikaona rama amepunguza mwendo mara ghafla nikaona wale wajeshi niliokuwa nao kwenye kibin ndani ya gari wanavunja usalama yanii wakaweka risasi kwenye chemba halafu kilichonishangaza kitendo cha kukoki walikifanya ndani ya dakika moja tu wote yani chuma zipo tayari ,mzee hapo akili imesharuka kitambo njia nzima kimyaa wazee wanaangaza kila mahali uongo mbaya sikujishughulisha hata kuanganilia pembeni mimi nilikuwa straight yani akili inaniambia lisasi zikianza tu nachochea moto mia ishirini kama ni kufa ntafia mbele tu wala sintojari kumpita tena rama.
Kuna kitu niliijifunza katika lile tukio ni kwamba unapokuwa katika eneo la hatari kama lile kwa upande wa wanajeshi lakini ,unatakiwa kuwa katika speed ya wastani ambayo hata ukiruka huwezi umia ndo maana mwaanjeshi alie kaa nami katikati aliniambi a petit fungula milango yani alimaanisha vioo viwe chini na lock ziwe off .
Yaani hivi waasi wakirusha Rpg gari ikiwa speed kwanza ni ngumu kuruka pili hata mkiruka gari ikiwa speed lazima muumie au mfe kabisa ila.mkiwa mwendo wa wastani ukisikia neno rpg wewe rukaa tu pembeni unakuwa umesave ndo sababu ya eneo lilie speed ikapunguzwa tukawa tunaenda taratibu.
Sas kipindi hicho kulikuwa na vizuizi kama vitatu hivi basi tukafika kizuizi cha kwanza jamaa wakapigiwa saluti tukapita hamna ukaguzi wa gari wala nyaraka kisa tu gari wamepanda wanajeshi congo banaa ...basi tukawa tunaendelea na safari tukaenda mbele tukakuta kuna gari imeingia porini naona ilikuwa na namba za zimbabwe roli moja hivi single deef basi tukasogea kwa mbele wanajeshi wakashuka kwenda kuliangalia eneo hilo wakakagua pale hakuna kitu wala yeyote kulikuwa na nguo nguo na vijibegi wakakomba safari ikaendelea tukaenda tukafika sehemu hapo ni ndani ya pori sehemu kama kuna barabara mbovu hivi yani lami imelika kimtindi...
Kuna mjinga moja alichomeka zile bunduki kubwa kubwa za mashine zanakuwa na cheni ya risasi yani aliifunga kabisa kwenye ngao za kibini ya gari ya rama sasa bwana tumefika yale maaeneo si yule mpuuzi akaanza kurusha risasi huku na huku ndo ile bomba ione tu kwenye tv yani ile bunduki ina sauti nzito halafu kali sanaa.yani kama una presha unaweza zimia .
Kuona vile na wale waliopo kwemye gari yangu nao wakatoa vyuma wakaanza kumimina risasi polini yani wa upande wa pembeni wanafyatua pembeni kila mtu na upande wake yani mwanajeshi tulieka wote akapitishi sMG juu ya open roof anaachia risasi daah mimi kihoro kimenipanda naona sasa vita imeanza mara nikasikia tumepitaa..kumbe lile eneo ndo lamatukio sana sanaa hivyo waakifika iliwalazimu warushe tu risasi ili kujiweka tayari nilikuja elezwa baadae kwamba kama waasi wangekuwepo basi lazima wengejibu tu na zingepigwa ila kwa kuwa hawajajibu basi wako mbali na eneo hilo au hawana mpango wakufanya chochote siku hiyo...
Basi safari ikasonga inafika saa kumi na mbili kasoro ndo tunafika checkpoint ya kwanza ya congo imeandikwa KARIBU LUBUMBASHI kwa juu moyo nikasikia unasema uwiii....i sasa napumzika kumbe mle mjini ndo nuksi zaidi bora hata huko polini tukaenda kidogo kuna custum gari zikakaguliwa na wale wanajeshi wakawa ndo wamefikia mwisho safari tukaachana nao sisi tukaingia town sasa kwende kulala kigiza kimeanza kuingia ....jamaa ram huwa anajua vigest vya kule tukaenda sehemu hata sipajui tukapaki akaniambia sasa ndugu tumefika ila wenyewe tutaonana nao kesho mchana wakati tunaenda kuwakabidhi magari yao .
Rama akafanya mawasiliano na wale wacongo wKafurahi sanaa wakasema kwa kuwa ni usiku itabidi tuoname nao kesho saa nane kwa kuwa wote wale ni watumishi wa serikali hivyo asubuhi isingewezekana .
Aise kipindi hicho disel na petrol ilikuwa shidah sanaa congo yani unaweza kuta foleni kubwa tena kubwa sanaa yani unakaa foleni kuanzia asubuhi hadi jioni ndo inaingia zamu yako haafu hupewi zaidi ya lita ishirini.
Tukalala usiku ule kwenye vile viguest vyso sikumbuki kama hata nilikula zaidi ya kula mikate yao ya chumvi na soda , kukakuchaa Sisi kwenye gari zetu tulikuwa na mafuta ya kutosha kabisa rama akapita huku na huku mara akaja na masela wana vidumu vya mafuta basi tukakubaliana tutoke nje kidogo mbali na zile guest tukapige nyoka yale mafuta si tunajua wenyewe mchana watakuja zichukua tulikubaliana tuwaachie lita hata tano tano tu zingine zote tuuzie zitatusaidia mbele..tukawasha gari kuna sehemu tukaenda kidogo kuna kama kumezungushiwa fance hivi tukapaki palee hakuna pilikapilika nyingi hivi...tukaanza kujipakulia mafuta tunakaribia kumaliza kujaza kidumu cha mwishoo ebwanaee kumbe tulikuwa nimefanya kosa kubwa pale bora ndo tungepigia nyoka pale pale guest ebwanae kufumba na kufumbua nissan dabo kibini hiyo imejaa wanajeshi kibao tayari apo tulipo wale vijana wakikongo wakaruka ule ukuta hadi ng'ambo wakakimbia wale wanajeshi wakawasindikizia na risasi huko huko sasa sijui walikufa au vipi nikabaki mimi rama amini usiamini rama hakuonekana kutetereka hata kidogo hata walivyotuelekezea bunduki rama alitulia tuli ana waangalia tu. mimi tayari akili haipo nikasema leo ndo mwisho wangu nakufaa..........uwiiii.
Itaendelea....usikose mda wa ifatr huu.
Inaendelea sehemu ya nane..... nawasalimu kwa kicongo mko byee ?
Haya tusonge tena ebwanae sasa bunduki zikawa zimeelekezwa kwetu vijana wa mafuta wameshasepa zao kwa kusindikizwa na risasi nyingi tu kimbembe kwetu tuliobaki niseme tu siku hiyo nikaona sasa sina uhai tena nasubiri kifo tu basii akili ikawa imeruka kitambo lakini rama katulia tu anawacheki tu harakati zao yani jamaa wanarusha hewani lisasi hatari kama wameona magaidi vile sasa niseme kidogo sehemu tuliyokuwa ni kama pale ambako hata mtu akikupiga robo huwezi kupata msaada yani tupo chaka kama sehemu kulikuwa na godauni hivi halafu kuna ukuta mlefu hivi ...ambao ndo wale vijana waliuruka .
Ghafla kikatoka kibao kwa yule kiongozi wao rama akakiona akajikinga kwa mkono hakikufika usoni kumbuka mimi niko nyuma ya rama na tetemeka kishenzi yani kiongozi wao akawa anafoka akaamriklsha ikala chini (yani tukae chini) .
Ngoja niseme kitu kidogo kuna hali ya kiasili huwa inatokea vitu viwili vikikutana na vikiwa na haiba( sifa ) yenye ufanano amini usiamni haviwezi shikamana matokeo yake vitapatana na kuheshimiana sasa wakati watwambia ikala chini mimi mtu mzima nipo chini kitambo lakini rama kakomaa hakukubali kabisa kukaa chini askali moja akageuza bunduki akataka kumpiga nakitako rama akakwepa kwa kuzuia kwa mikono kumbuka hapo sasa mimi kihoro juu najiuliza huyu jamaa rama ana akili kweli sasa ya nini kwa nini asikae tu chini .
TUHAME STORY KIDOGO.
Kama nilivyosema hapo nyuma kuna utofauti mkubwa sanaa kati ya mtu ambae sio muoga na mtu jasiri sasa pale rama alikutana na mtu jasiri mwenzio ndo maana nikasema majasiri wawili wa kikutana lazima pachimbike na mwisho lazima lazima waheshimiane yani mtu jasiri hata kama moja ana siraha mwingine hana asiekuwa nasilaha huwa haogopi chochote inakuwa sawa na yule kama vile wote wana silaha
Kipindi cha vita kuliibuka vitoto niseme kama vile vilikuwa vina sumbua Dar sijui mnaviita PANYA ROAD wale ndo wajasiri ninaowaongelea yani vinajua kabisa nchi hii ina dola ngumu lakini wao wanaingia nakusimamisha mtaa bila uoga tena na visilaha vya kienyeji lile sasa ndo chimbuko la watu jasiri sasa kutokana na ugumu wa maisha na makuzi congo vijana kama wale walikuwa wengi sanaa kwenye majimbo mbali mbali .
Sasa wakati vita inaendelea askali wakongo wakawa wanaasi hivyo kukatokea upungufu mkubwa sanaa wa wanajeshi wapiganaji ndo kiaina serikali kupitia viongozi wa majimbo na chama tawala wakawa wanawapenyeza jeshini kiaina kwa makubaliano vita ikiisha wataajiriwa lakini halikuwa lengo la serikali za majimbo kadhaa sio kongo nzima na ndo hivyo vikundi vya waasi vilivyokuja kujitokeza baadae ya vita na wengi wao walikuwa under 25 yani walikuwa wanachukuliwa miaka kama kumi na sita 16 na kuendelea anafundishwa kurusha risasi basi .
Kazi imeisha kesho asubuhi wanapandishwa kwenye roli frontline kupigana yani vikawa vinapiganishwa wao kwa wao katika majimbo yenye waasi vilikufa sanaa sasa baada ya vita kupoa waliorudi sasa mjini ndo kasheshe yake hiyo kama hao tuliokutana nayo yanii hata makanali wa jeshi walikuwa wanaviogopa hivyo vitoto kumbuka vimetoka kupigana vita tena vita ya uso kwa uso vimerudi mjini vimezaga yani nimwendo wa vurugu vina siraha nzito nzito na kombati mchamganyiko wa rangi yani wanaweza kupora gari wakawa wanatembea barabarani tena kwenye line ambayo sio yao wole wako umzibie barabara utajuta yanii ukiona gari linakuja usoni kwako wewe pisha hata kwa kuingia mtaroni lakini yeye apite .
Jiji lao so walikuwa wanajulikana migari yao mibovu haina taa wala madirisha yanii nimwemdo wa kuendesha tu ilimradi vurugu tu mtaani sasa ujichanganye uwe mgeni yani utapata tabu vingenevyo uwe na mtu ambae ni mcongo na maarufu au uwe na watu ambao wapo kwenye system angalau utanusurika.
TURUDI KWENYE STORY.
Sasa walitukamata pale nao hawakuwa wanajeshi wenyewe walikuwa wale vijana yani wale madogo ndo walikuwa wametuotea tena tuna mali mafuta pesa na gari mpya .
Sasa kama nilivyosema majasiri wanaheshimiana amini usiamani swala rama ukakata kutii maelekezo yao likaibuwa maswali sasa yakutaka kutujua sisi ni akina nani na kwanini tupo pale halafi cha kushangaza pembeni tumepaki gari mpyaa kabisa hili nalo nafikiri liliwachanganya kidogo kwa kifupi tu ni kwamba kwa kipindi hicho hadi sasa wanaoununua gari mpya ni serikali na watu wazito serikalini basii nadhani liliwatisha halafu hapo hatujaongea so hawajajua kuwa sisi ni raia wa wapi
Maswali ya kaanza ...
Wao :Nyinyi ni akina nani ?
Sisi: hatukujibu rama akatoa passport akawapa .KOSA
kile kiongozi chao kikasema sasa nyie na madocoma( document) mbele ya lisasi zinasema nini?ý
Moja akawa anamwambia wenzie wachukue mafuta chukua hiyo petrol mgari ( yani achukue zile dumu za mafuta.
Rama ndo akaonge sasa wakasikia kiswahili kimenyooka wakasema nyinyi batized ( alimaanisha wataanzania)?
Rama akasema ndio .
Wakauliza sasa mko mnafanya nini apa mnaiba mazutu(mazutu ni mafuta) mcongo .
Hapo ndo rama akawa anawaelezea kuwa tumeishia mafuta hivyi kuna rafiki zetu walikuja kutuuzia mafuta sasa walivyowaona nyie ndo wakakimbia kuogopa sisi tumeishiwa yani akabadili story kutoka sisi kuuza hadi kuwa wanunuzi na hiyo baadae ilitusaidia na kama tungesema tunauza mafuta labda hali ingefika kulazima wenye magari wafike pale tungeoneka sisi sio waaminifu tena wale maboss wangetuharibia kumbuka mpaka.mda huo wanajua tupo guest kule tumepaki .
Sasa katika kuhoji hoji maswali.ya hapa na pale ila kwa ukali na mikwara kibao kumbe kuna mmoja anajua kusoma akachukua ile pasaport akaisoma akaelewa kweli sisi ni watanzania ishu nikawa wanataka yale mafuta rama nae akawa anakoma nao .
Kuna kijana moja katika lile kundi akaamuuliza rama hizi gari niza kuprezince? ( yani kamaanisha gari niza ikulu si mpyaa?) Rama akaitikia ndio pale pale hawakukaa tena wakaondoka fasta hawakutaka hata kukaa tena yani ujanja wao wote sema hizi gari ni za ikulu huguswi tena wanakuwa wanajua ni za wakubwa na kuharibiwa kutawatia hatiani hata kuuawa
Congo kuna wababe wapo kwenye system ya chama tawala asikwambie mtu yani uguse gari lake atakusaka popote pale hata roho atakutoa sasa kumbe yale magari wale jamaa nao ni watu wa system kwenye chama tawala naona ujio wa zile gari walishajua ni za kina nani wakaona isiwe tabu wakasepa za sisi tukachukua mafuta yetu tukageuka tukarudi guest tukatulie kwanza .
Saa nane wale jamaa wakafika wakatupa chetu tukawakabidhi magari yao ila wakafurahi sanaa walikuja na dereva wakamwambia asubuhi atupitie lifti hadi boda wakati wakuondoka kwakweli walifurahi na walituongezea hela kidogo na yale mafuta tuliwaauzia madereva wengine
wa IT pale pale . Asubuhi tukaanza safari ya kurudi homeland tanzania na ndo mwanzo wa kuanza kazi za magari ya IT ukawa umeanza yakawa ndo Maisha yangu kuzunguka nchi mbali mbali ila katika harakati zangu nimeenda kongo zaidi kuliko nchi zingine.
Asante kwa kunifuatilia
MWISHO.