Na Gianna Amani
Inawezekana kuwa hujui hili lakini taarifa za kihistoria zilizopo zinaeleza kuwa chai na kinywaji cha chai asili yake ni nchini China na Myanmar na jambo la kushangaza zaidi mataifa mengine yameijua Chai katika karne ya 16.
Chai ni kinywaji maarufu duniani kinachokadiriwa kutumiwa na watu zaidi ya bilioni 2 chai kila siku, zaidi ya nchi 60 huzalisha zao hilo ambalo ni maarufu kama zao la biashara duniani kwa miongo mingi, lakini inaelezwa kuwa ni katika karne ya 17 ndipo kinywaji hicho kilipata umaarufu.
Mataifa mengi duniani watu wake hutumia chai hususan kama kifungua kinywa au kinywaji cha wakati wa baridi. Nchini China utapata hisia halisi kuwa kweli huenda chai ilianzia hapo, kwa unywaji wa chai katika taifa hili linaloongoza kwa watu wengi duniani ni utamaduni uliopo kwa muda mrefu.
Karibu kila mahali utakapokwenda utakaribishwa kwa chai, katika mikutano mikubwa midogo na ya kati lazima utakuta chai, chai kwao ni ukarimu kwa mgeni tofauti na ilivyozoeleka katika sehemu nyingine, na huku chai haina sukari na si ya moto sana.
Kuna aina nyingi za chai na pengine wengi hawawezi kutofautisha ladha isipokuwa wazoefu na wabobevu katika eneo hilo. Kuna nchi nyingi zinazalisha chai kwa wingi Afrika ikiwemo Kenya, Uganda, Malawi, Tanzania, Rwanda na Msumbiji lakini ukitaka kupata ladha tofauti za chai, utazipata China.
Katika kuenzi utamaduni wa Chai, mkoa wa Fujian ambao ni maarufu kwa kilimo cha chai una bustani mahsusi kwa ajili ya Chai iitwayo Yanzike Ecological Tea Garden ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 2018 ikiwa na ukubwa wa ekari 66.7.
Bustani hiyo unaweza kuiita kama shamba darasa tu, maana kilimo cha chai k kimeenea maeneo mengi lakini katika eneo hilo kilimo ni cha aina yake hakuna matumizi ya kemikali kama mbolea na mbinu za kupambana na wadudu na magonjwa ya mimea zinatumika zile za asili.
Mbinu za kisasa zinatumika kutoa taarifa za hali ilivyo katika bustani hiyo sanjari na kupima udongo ili kupata taarifa za kuongeza ufanisi katika uzalishaji na ubora wa bidhaa yenyewe hata umeme nishati inayotumika hapo ni ya nishati ya jua.
Mwezi machi mwaka jana wakati wa ziara ya Rais Xi Jinping mkoani Fujian, alitembelea bustani hiyo na kusisitiza kuhimiza utamaduni wa chai na kukuza sekta ya kilimo cha zao hilo.
Vyombo vya habari v viilielezea ziara hiyo kama ya kukumbusha historia ya huko ambako Rias Xi alifanya kazi huko kwa muda mrefu, na wakati huo alilisistiza kilimo cha zao hilo kama mkombozi wa uchumi. Katika Mji wa Wuyishan iliko bustani hiyo ya chai, watu wengi wamepata ajira kuanzia uzalishaji wa chai yenyewe, uongezaji wa thamani na bidhaa za chai kwa ufupi mnyororo wa thamani ya Chai katika eneo hilo unaonekana.
Ili kuwa na uendelevu, Serikali ya Wuyishan pamoja na ile ya mkoa wa Fujian kwa pamoja wameanzisha taasisi ya utafiti wa zao la chai katika eneo hilo.