mHAMAS-shaji
Member
- May 31, 2024
- 63
- 177
- Thread starter
- #121
MAISHA YA DEPO
SEASON-2
EPISODE 26
Hali hiyo ilikuwa ikiwashinda watoto wengi wa kishua na siku moja Wini alinipa dili la swahiba yake mmoja waliosoma wote kuwa anataka kutoroka nilivyompelekea dili hilo Shukrani aligoma kulifanya.
Kiukweli nilikuwa na ukata hivyo nikaichukulia kama fursa nililipiga dili hilo nikitumia nondo zilezile za dili lililopita nikalitoboa na kujivutia tembo wawili.
Kifupi hiyo ndiyo ikawa kazi yangu ambayo haikunitupa kwenye maokoto na baada ya kufanikisha dili hilo Shukrani alianza kunielewa na tukawa tunapiga wote na malipo yakawa ni pasu kwa pasu kwa madili yaliyokuwa yanapitia kwangu.
Sifahamu kwa upande wa Shukrani maana kazi alizokuwa akizileta yeye zilikuwa ni za hela ndogo nilikuwa nikihisi ananipiga ila ulikuwa ni kama msimu wa maembe ambao ulikuwa ni adimu kumkuta inzi ama ngedere aliyekonda.
Hela hizo zilikuwa zikinipiga tafu kwenye shida ndogondogo na nilikuwa sikatiki KIWANI kulikokuwa kukiuzwa mihogo, maandazi na vitafunwa vingine.
WAZALENDO wengi tulikuwa tukijazana huko maana ule muda tuliokuwa tukisimuliwa ulikuwa umefika kwani tulikuwa hatushibi chakula cha MZABUNI kutokana na kazi tulizokuwa tukizifanya si kwamba walipunguza kipimo hapana ila ni matumbo yalikwishatanuka na kibaya zaidi hakukuwa na nyongeza.
Kipindi hiki ndicho kilichoikuza misamiati kama vile KUBASTI yaani kula zaidi ya mara moja ila kwa kujificha maana haikuruhusiwa kwani ukila zaidi ya mara moja ina maana wengine watakosa kwa maana hiyo ule msemo wa SIFA WEPESI haukucheza mbali wakati wa KUBASTI.
Msamiati mwingine ulikuwa ni KIJOGOO ambao unamaanisha kiporo ama chakula kinachohifadhiwa usiku kwa ajili ya kuliwa alfajiri kabla ya kwenda kwenye FATIKI ili upate nishati ya kuisogeza siku nyingine.
Ikumbukwe KIJOGOO ambacho nimekipiga sana si chakula kinachotolewa na MZABUNI ila ni wewe mwenyewe unakitunza aidha baada ya KUBASTI, kubakiza ama kununua KIWANI.
Siku zilizidi kukimbia huku idadi ya watu ikiongezeka hali iliyopelekea kuundwa KOMBANIA ya tano na pia majina ya KOMBANIA yalibadilika kutoka majina ya wanyama hatimaye zikawa herufi.
KOMBANIA ya chui chini ya ST Fred wao waliitwa ALPHA COY (A-Coy), nyingine ni ile ya ST Ustadhati Rehema yaani tembo ikaitwa BRAVO COY (B-Coy), simba ya akina Linda iliitwa CHARLIE COY (C-Coy) na ile ya kwetu ikaitwa DANGER COY (D-Coy).
KOMBANIA iliyoongezeka ilifahamika kwa jina la EAGLE COY (E-Coy) na katika kipindi hiki tukatakiwa tuanze kuvaa vipensi vifahamikavyo kama PICKSHORT na kukatishwa kuvaa suruali za track.
Katika moja ya watu walioathirika na mabadiliko haya alikuwa ni Ustadhati Rehema ambaye aliwagomea kabisa kuvaa nguo hizo.
MADAWILI wengine walikuwa wakiona aibu kuvaa nguo hizo ila iliwabidi wavae maana kila pale walipokuja KOMBANIA walikutana na adhabu.
Rehema yeye adhabu hizo zilionekana kutofua dafu ingawaje wakati mwingine alikuwa akitetewa na maafande.
Haijawahi kuisha nguvu misemo ya wahenga na pale waliposema “Hakuna marefu yasiyo nan cha” ndicho kilichokuwa kikitokea kwa Rehema ambaye alikuwa akibadilika kidogokidogo maana kuna baadhi ya siku alikuwa akifoleni KOMBANIA bila ya kufunika kichwa.
Kutokana na mabadiliko hayo ya siku baada ya siku SERVICEMEN waliokuwa wakitusimamia kwa kipindi hicho walikuwa wakituambia “Kunyweni maji mengi mioyo ielee maana kozi inakaribia kuanza”.
Hatukuwaelewa walikuwa wakimaanisha nini kwani tulikuwa tukiona kozi imeanza kitambo kilichokuwa kimebadilika ni mavazi pekee.
Ratiba ya shamba haswa kuvuna haikuwahi kukoma kwa siku chache kutokana na ukubwa wa shamba na hata hivyo tulikuwa tukivuna kwa nusu siku hatukuwahi kushindia huko.
Siku moja baada ya kutoka shamba tulipewa jukumu la kuhamisha vitu vyetu kwa ajili ya kuishi kwenye MAHANGA ya KIKOMBANIA.
Yaani awali kipindi tunafika walikuwa wakitupeleka kwenye HANGA lolote lile lililokuwa wazi kwa kipindi hicho kabla ya kutuhesabisha namba na kutugawa KIKOMBANIA hivyo ukawa ni wasaa wa kuishi kwenye MAHANGA ya KOMBANIA.
Hali hiyo ilikuwa ikileta wepesi kwenye usimamizi kama ST nina ushuhuda nalo lakini pia haikucheza mbali na kauli ya kihenga isemayo “Ndege wafananao huruka pamoja”.
Tulikuwa tukipata ugumu pale karani akitaka kujua majina ya walinzi wa HANGA na pale anapokosekana mmoja wetu aidha kwa kudoji ama kuumwa tulikuwa tukishindwa kujua HANGA alilopo kwa ajili ya kujiridhisha kama uongozi wa KOMBANIA😆.
Tukiwa katika zoezi hilo tukufu tulisikia filimbi zikipigwa za kutosha kutokea UWANJA WA DAMU ambako kwetu tulishangaa maana haukuwa muda wa chakula na tuliambiwa TUFOLENI huko baada ya chakula cha jioni yaani tulikuwa na KAUTAWALA fulani hivi ka chinichini.
Kitu cha kushangaza ni kuwa waliokuwa wakipiga filimbi hizo walikuwa ni BAKABAKA ambao walikuwa na Matroni Neema na tulipojipeleka sisi tuliambiwa turudi maana yajayo hayatuhusu.
Basi WALIFOLENI askari wa JKT wakiwa na sare zao za KARANGA full combat juu na chini na walifoleni wakiwa na ndoo kila mmoja.
Walianza kupitishwa lokoo na baada ya muda akasikia Matron Neema akisema “Sikia kutoka kwangu, kwa yeyote asiyekuwepo hapa na anastahili kuwepo basi mfikishieni taarifa mwambieni kuwa awe na maelezo ya kutosha kwanini hayupo mahala hapa”.
Aliendelea kusema “Tukianzia kwenye lokoo ya jana tuliwataarifu kuwa leo asubuhi mnatakiwa kwenda shamba kwa ajili ya kutoa mahindi yetu ila nimesikitishwa sana na kiburi mlichokionesha sijui kama mnaweza kunieleza ni sababu zipi ziliwafanya msiende au hamkunielewa”.
Kilitawala kimya cha sekunde kadhaa na baadaye akaendelea “Kimya maana yake hakuna majibu sasa bila kupotezeana muda ambaye anajijua hajaenda naomba ajisogeze pale mwenyewe haijalishi ana sababu au hana tutaelezana tukiwa pale”.
Zoezi hilo lilifanyika na mchujo mkali ukachukua nafasi ambao ulizalisha makundi mawili ya waliosafi na wasiosafi yaani madoja wa kazi.
Baada ya hapo ilisikika kwa mara nyingine sauti ya Matroni Neema “Jana kipindi tunawaambia mkawa mnatuona kama Mchinga Sound vile tuko stejini tunatumbuizasiyo, sawa sasa leo nasisi tutakuwa tunawatizama ninyi mkitumbuiza naomba makamanda wangu kazi ianze”.
Ebwana eeh ilitokea shoo siyo ya kitoto yalikuwa ni masaa matatu yenye ujazo wa DOSO la machozi, jasho na damu.
Wale jamaa walivurugwa siyo kawaida nashindwa hata nisimulie lipi alafu niache lipi ila tulishaanza kuelewa ni kwanini walituambia tunywe maji mengi mioyo ielee.,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
************Itaendelea………………………………...
MAISHA YA DEPO
SEASON-2
EPISODE 27
Jioni yake tukiwa KOMBANIA habari ilikuwa ni hiyo makarani wao walipona maana ukiwa karani tafsiri yake una kitengo hivyo kazi za hovyohovyo kama hizo zinakupitia kushoto hivyo mtu kama karani wetu wa KOMBANIA afande Jala alikuwa yupo kundi la walio safi.
Tukiwa KOMBANIA afande Jala alituambia kuwa ule ni mfano tu wa itakavyokuwa kipindi cha Six Week hivyo tuwe tayari maana kwa wale imetokea kwa masaa machache lakini kwetu sisi itakuwa ni ndani ya siku 42.
Tulipomwambia kuwa wale walikuwa na makosa ndiyo maana yamewakuta mabalaa yale akasema kwamba “kipindi cha Sixweek hakuna tofauti kabisa kati ya adhabu na mazoezi yaani afande anaweza kuja akawaambia kuruta mbona mmepoa haya kunja ngumi”.
Akaendelea kutuhabarisha “Yaani hapo kosa linakuwa ni kupoa na ili mchangamke inabidi awape DOSO la kwenda yaani nyie ponapona yenu ni mkiwa kwenye bustani wakati wa kumwagilia mboga na hapo muombe msiende na afande wa BAKABAKA”.
Siku zilizidi kukatika japo tulikuwa tukiona zinachelewa haswa pale tulipoambiwa kozi bado haijakolea huku tukiogopeshwa zaidi na hiyo siku iliyoitwa introduction to the camp ambayo ni shoo ya ufunguzi wa wiki sita.
Siku moja baada ya chai tuliitwa UWANJA WA DAMU ambako tulikutana na mazingira tofauti kabisa kwani kulikuwa na meza na viti pamoja na maafande wengi wa BAKABAKA vuta picha uoga tuliokuwa nao mioyoni mwetu.
Mungu si Athumani mvua ikashuka ikabidi walighairishe zoezi lao ambalo hatukulijua lilihusiana na nini tukaruhusiwa kurudi zetu MAHANGANI hali iliyotufanya tupige makelele ya furaha kwa kunusurika na zoezi ambalo tulihisi ni lile la utambulisho wa kikosi.
Siku hiyohiyo baada ya chakula cha mchana huku mvua ikinyesha ilibidi TUFOLENI kwenye bwalo la chakula la SM kuna zoezi lilionekana kutakiwa kufanyika ila kwa mara nyingine lilishindikana tena maana eneo hilo lilionekana halitoshi kwa wingi wetu.
Basi ulipofika usiku wa siku hiyo ambayo tulikuwa tukila chakula cha jeshi bila kukitolea jasho lolote tulifoleni KOMBANIA kama ilivyo ada.
Mvua ilikuwa imekata hivyo hali ilikuwa shwari kabisa tulikuwa tukila ngoma mbalimbali zilizofahamika kama CHENJA ambapo afande Jala ndiye aliyekuwa akituimbisha alituataka tumpe beat ndipo yakaanza kusikika makofi paah! paah! paah! paah!“
"Afande: Embe dodo sijalila, embe dodo bwana sijalila, embe dodo sijalila, embe dodo bwana sijalila.
Sisi: Embe dodo sijalila, embe dodo bwana sijalila, embe dodo sijalila, embe dodo bwana sijalila.
Afande: Na barua nimetuma, na barua bwana nimetuma, na barua nimetuma, na barua bwana nimetuma.
Sisi: Na barua nimetuma, na barua bwana nimetuma, na barua nimetuma, na barua bwana nimetuma.
Afande: Na majibu sijapata, na majibu bwana sijapata, na majibu sijapata, na majibu bwana sijapata.
Sisi: Na majibu sijapata, na majibu bwana sijapata, na majibu sijapata, na majibu bwana sijapata.
Afande: Embeh(paah!), embeh(paah!), embeh(paah!), embeh(paah!).
Sisi: Embeh(paah!), embeh(paah!), embeh(paah!), embeh(paah!).
Afande: WAZALENDO Wiih
Sisi: Waah Afande: Ewiih
Sisi: Ewaah
Afande: Ewiih
Sisi: Ewaah”.
“Eti mchana WAZALENDO mlikuwa mnafurahia mvua kunyesha mkiona mmeikwepa introduction acheni kujidanganya hakuna kipindi makamanda wanaenjoy kozi kama kipindi cha mvua”.
Karani wetu alianza kutujaza gesi tukajikuta tunaguna “mnnnh” akasema “Khaah mmeamua kuning’ong’a sawa ning’ong’eni tu ila ukweli ndiyo huo”.
“Sixweek yenye mvua ni tamu mno kuliko ya jua tuulizeni sisi tuliofanya kipindi cha masika nyie simmekuja kipindi hiki cha mavuno kidogo kozi yenu itakuwa mtelezo” aliendelea kujazia hoja yake.
Afande aliendelea kusema “Yaani ndani ya usiku wenye baridi kali na mvua yenye ujazo mnakesha na afande MKALAKALA ambaye anawapa DOSO la nguvu na asubuhi yake mnaamkia shamba mnaenda kulima huku mvua inanyesha yaani ni hatari tupu si mmeshawahi kulima kwenye mvua nyie? najua hamjawahi ila mtalima tu”.
Afande huyo aliendelea kutupa mfano mmoja ambao tulijiona sisi wenyewe ile siku KARANGA walioharibu kazi wakidosolewa kunako UWANJA WA DAMU.
Kwanza wale wasio na makosa walikuwa na kazi moja ya kusombelea ndoo za maji kutoka mtoni ambayo walimwagiwa wale walioharibu kazi na wakatakiwa kujigaragaza chini mithili ya nyoka waliomwagiwa mafuta.
Katika moja ya tukio la kufikirisha moja ya BAKABAKA aliyefahamika kwa jina la “Shona tulia” alikuwa akichukua ndoo za maji na kujimwagia yeye mwenyewe yaani vuta picha anayetaka kukuadhibu anajiadhibu kwanza yeye sasa niambie itakuwaje ukifika muda wa kukuadhibu mkosaji.
Kifupi wale jamaa mpaka yanaisha yale masaa matatu walikuwa hawana hali na walichafuka mno.
Mfano huo ulianza kutufungua kwamba huenda kinachozungumzwa ni kweli maana tulizidi kumdodosa na kumuuliza kama mvua siyo shida kwao mbona walikuja tofauti na meza zao ila baada ya mvua wakaghairisha.
Karani Jala alituambia kua ni kweli walisitisha zoezi lao kutokana na mvua kunyesha ila sababu ni kuwa kuna fomu tulitakiwa tuzijaze kwaajili ya kuandaliwa vyeti hivyo isingekuwa rahisi kufanya hivyo kwenye mvua.
Maneno ya karani huyo yalikuwa yakituingia maana ni kweli muda ule tuliona marundo ya makaratasi kwenye meza.
Siku iliyofuata hali ilikuwa shwari na baada ya chai tuliitwa tena UWANJA WA DAMU na mazingira yalikuwa ni sawa kabisa na yale ya jana.
Kweli bwana tulipewa fomu za jeshi tuakajaza baadhi ya taarifa zetu na baada ya zoezi hilo Matroni Neema alitusisitiza kuwa tunywe maji mengi tukae tayari kwa lolote maana siku yoyote kitanuka.
Maneno hayo yalizidi kutupandisha joto na mbele yetu tukawa na siku mbili ambazo hatukujua zitafika lini yaani kiyama na hii ya utambulisho wa kambi.
Siku iliyofuata ilikuwa mahususi kwa ajili ya vipimo vya hali ya afya zetu lakini zilihusika KOMBANIA tatu pekee yaani A-Coy, B-Coy na E-Coy wengine tuliungana na SM tukaelekea zetu shambani kuendelea na mavuno.
Siku hiyo KARANGA zilikuwa za kutosha inaonekana DOSO walilopewa lilitosha kuwarudisha kwenye mstari hivyo walikuja kwa idadi ya kutosha kwani bado walikuwa kwenye siku za matazamio alizozitoa Matroni daboli N. ,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
***************Itaendelea…………………......…...
The season 3 is ready to arrival
Stay ON................