Wakati matukio ya watuhumiwa kufia mikononi mwa polisi, gerezani yakiibua sintofahamu, Chama cha Majaji Wastaafu (Tarja), kimependekeza kurudishwa kwa utaratibu wa mahakama kuwa ndio chombo kitakachochunguza vifo vyote vyenye utata.
Chama hicho kimesema huko nyuma mtu akifariki gerezani, kituo cha polisi au sehemu nyingine yenye wasiwasi, kifo hicho kinachunguzwa na Mahakama inayotafuta ushahidi.
Majaji hao wastaafu wametoa mapendekezo hayo jijini Dar es Salaam, kwa Tume ya Hakijinai inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Othuman Chande inayoendelea kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali.
Tume hiyo inakusanya maoni na mapendekezo hayo baada ya kuundwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuboresha mfumo wa haki jinai ambao umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu na wananchi.
Mapendekezo ya majaji hao yaliwasilishwa na mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Thomas Mihayo kipindi ambacho kumekuwa na matukio ya watu kufia vituo vya polisi kwa kujinyonga na au gerezani, hali inayozua maswali lukuki.
Mijadala hiyo imekuwa ikiibuka hususan mitandaoni baada ya wanaojinyongwa wakiwa mahabusu kuelezwa na jeshi la polisi kuwa walitumia mashati waliyovaa ama dekio.
Majaji hao wanatoa mapendekezo hayo wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam Kivukoni (Kinondoni) ikiwa katika harakati za uchunguzi wa sababu za kifo cha mwanamke aliyedaiwa kujinyonga katika kituo cha Polisi Mburahati, Dar es Salaam, Stella Moses.
Mahakama hiyo inasikiliza kesi hiyo kutokana na shauri la maombi lililofunguliwa na familia ya marehemu inayopinga taarifa za ndugu yao kujinyonga kituoni hapo Desemba 20, 2020. Uchunguzi wa kifo chake unafanyika kwa amri ya mahakama hiyo iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga Desemba 19, 2022, kutokana na shauri la maombi lililofunguliwa na familia ya marehemu.
Shauri hilo la maombi ya jinai ya uchunguzi wa sababu za kifo hicho, namba 3 la mwaka 2022, lilifunguliwa na shemeji wa marehemu Stella, Emmanuel Kagongo kwa niaba ya familia, miaka miwili baada ya kifo hicho, ikipinga maelezo ya Polisi kuwa alijinyonga.
Tukio jingine ni la Machi 4 mwaka huu, Sheikh Said Ulatule (80) anayedaiwa kupoteza maisha katika gereza la Ukonga, Dar es Salaam ambalo liliibua mjadala juu ya mazingira ya kifo chake. Siku mbili baada ya gazeti hili kuripoti utata wa kifo chake, Mkuu wa Magereza Dar es Salaam, George Wambura alitoa ufafanuzi kuhusu kifo hicho akisema kilitokana na ugonjwa wa shinikizo la moyo uliokuwa unamkabili tangu mwaka 2017 alipoingia gerezani.
Hata hivyo, Kituo cha sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilijitokeza kuzungumza na waandishi wa habari Machi 16, mwaka huu na kimeungana na familia ya marehemu kutaka kufanyika kwa uchunguzi zaidi wa kifo chake.
Walichokipendekeza Majaji
Baada ya kutoka kuwasilisha mapendekezo hayo, Jaji Mihayo alizungumza na waandishi wa habari alisema, “hakimu akijiridhisha kwamba kuna mtu anapaswa kushtakiwa kutokana na kifo hicho, basi ataagiza fulani au kundi fulani wakamatwe na kushtakiwa kwa kosa la mauaji.
“Hatasema nani ana makosa hapana...bali atasema kulingana na mazingira haya kifo hiki kinaweza kusababishwa na watu kadhaa...basi polisi wanafanya upelelezi na kukamata, ndivyo ilivyokuwa huku nyuma,” alisema Jaji Mihayo.
Jaji Mihayo alisema miaka ya nyuma kulikuwa na utaratibu huo, lakini hivi sasa hakuna, ndiyo maana mambo yanapotokea ikiwemo mtu kufia kituo cha polisi kunakuwa na sintofahamu, mara inasema amejinyonga huku ndugu wa marehemu wakikataa.
“Lakini kukiwa na utaratibu huu wa hakimu akisema huyu mtu amekufa kituo cha polisi lakini sio kifo cha kawaida maana yake ameuawa au kuteswa, kwa hiyo upelelezi ufanyike. Sheria yake haijafutwa, lakini watekelezaji wake hawajulikani kina nani, zamani ilikuwa mahakama,” alisema.
Katika hatua nyingine, Tarja kimependekeza maagizo, ikiwemo kuwaweka watu ndani yanayotolewa na wakuu wa mikoa au wilaya yatolewe kwa maandishi na si midomo, ili mhusika akitaka kushtaki uwepo ushahidi.
“Ili maagizo yafuatiliwe na utekelezaji wake uwe wa maana lazima yatolewe kwa maandishi,” alisema Jaji Mihayo.
Pia, Tarja kimesema kazi za kamati za ulinzi na usalama sio kukamata watu, bali kuangalia hali ya kiusalama katika wilaya au mikoa, ikitokea kuna viashiria vya uhalifu kutaka kufanyika basi polisi watachukua utaratibu wa kuwakamata.
Jaji Mihayo alisema utaratibu wa kamati ya ulinzi na usalama kuagiza kukamata sio sahihi, akisema haina mamlaka, bali wenye mamlaka ya kukamata ni jeshi la polisi. Pia, chama hicho kimependekeza wananchi kuheshimu taaluma zao na sio vyeti, akisema hivi sasa Watanzania wameingia katika wimbi la watu kuheshimu vyeti zaidi kuliko taaluma.
“Ndio maana hivi sasa wanachipuka madokta wengi kama uyoga, wanafikiri udokta ndio maana, lakini hauna maana kama huna ujuzi wa kazi. Hivi sasa kwa sababu ya watu kuheshimu vyeti hata waziri katika wizara hajipi muda wa kujifunza.
“Waziri anaamini anajua, kwa sababu ana cheti anaanza kutoa maagizo ambayo yapo kinyume. Tumetoa mapendekezo ya kwamba wananchi waheshimu taaluma za watu na uzoefu wa kazi,” alisema Jaji Mihayo.
Alichopendekeza Profesa Kabudi
Mtaalamu wa sheria, Profesa Palamagamba Kabudi ni miongoni mwa watu waliotoa maoni, akisema ni wakati muafaka kuwepo na mfumo wa fidia kwa waathirika kwa vitendo vya uhalifu, kudhalilishwa au vitendo vya ukatili wa kijinsia badala ya kukazana na wahusika wanaotekeleza vitendo.
“Tumekazana na wanaotenda vitendo hivi ikiwemo kuwapa adhabu, lakini suala la fidia au utaratibu wa kuwarejesha waathirika wa vitendo hakuna.Mfano mwathirika wa kubakwa, mtu kufungwa sawa miaka 20, lakini aliyefanyiwa kitendo lazima aangaliwe.
“Pia anahitaji kusaidiwa kisaikolojia na matibabu ili kutoka katika hali ya kuathirika, kwa muda mrefu mkazo wetu ni kumuangalia mhalifu tu na kumsahau mwathirika wa uhalifu ambaye anachukuliwa kama shahidi katika kesi,” alisema Profesa Kabudi. Profesa Kabudi ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, katika maoni yake alikwenda mbali zaidi akitaka pia uwepo wa skimu ya fidia kwa waathirika wa uhalifu.
Profesa Kabudi ambaye pia ni mbunge wa Kilosa mkoani Morogoro, alipendekeza mfumo wa magereza uangalie zaidi namna ya kuwapa ujuzi wafungwa badala ya kubadilisha tabia zao pekee. Ameshauri wapewe ujuzi na elimu ili wakitoka wawe na shughuli za kufanya.
“Tuwe na mpango maalumu wa mafunzo magerezani, tuwe na Veta, pia wahalifu wenye umri mdogo na vifungo virefu wawezeshwe kusoma na kuhitimu katika ngazi mbalimbali,” alisema Profesa Kabudi.
Pia, alisema watu ambao makosa yao si ya mauaji au ukatili Serikali ifikirie kuwepo kwa magereza ya wazi yatakayowawezesha watu hao kufanya shughuli nyingine za Taifa.
Katika hatua nyingine, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu, Simon Sirro ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe aligoma kuzungumza na wanahabari, akisema hana cha kusema kwa sababu ameshavieleza mbele ya Tume ya Haki Jinai.
MWANANCHI