Nimesoma andiko lako lote neno kwa neno na mstari kwa mstari.lakini napingana na Baadhi ya maneno yako ambayo yanaharibu kabisa andiko lako zima.
Unaposema kuchagua na kuangalia aina ya Damu za kumwagwa unakuwa unamaanisha nini? Je Damu zipi zinatakiwa na kustahili kumwagwa na zipi hazistahili?
Nani anayepima ,kuthibitisha ,kuidhinisha na kutoa ruhusa ya kuwa Damu hii imwagwe na ya huyu isimwagwe au imwagwe kidogo?
Huyo mtu anatumia kigezo kipi kutoa idhinisho juu ya Damu ipi imwagwe na ipi isimwagwe? Huo mfumo wa kumwaga Damu za watu unasimamiwa na nani? Kwa sheria zipi? Kwa katiba ipi? Kwa mahakama ipi? Na kwa mamlaka ipi?
Kwanini kama mtu kafanya kosa asipelekwe tu mahakamani ili mahakama iamue? Kwanini Damu zingine zimwagwe kifichoni bila kufikishwa mahakamani na watu kusikiliza mwenendo mzima wa kesi na ushahidi wake?
Kwanini usingetoa ushauri wa kuwa hakuna anayestahili kumwaga Damu ya mtu yeyote yule wala kukatisha uhai wa yeyote yule na wala haitakiwi vitendo hivyo kufanyika hapa Nchini?
Kwanini unaziweka Damu za watanzania katika madaraja? Kwamba huyu Damu yake inastahili kumwagwa kutokana na makosa haya na huyu haitakiwi kumwagwa? Vipi kama mtoa idhini,ruhusa na mamlaka akatoa na kuruhusu kumwagwa kwa Damu ya mtu fulani kwa chuki zake tu binafsi au kwa kulinda cheo chake? Nani atarudisha uhai wa huyu aliyeonewa? Maana kama ni mahakamani kuna kukata rufaa na hatimaye mtu kupata haki yake.
Ningependa kukwambia na kukushauri kuwa usiweke Damu za watanzania katika madaraja wala usiwe mtoa hukumu ya kuwa huyu anatakiwa kuuwawa na huyu hastahili. Ni lazima tuseme kuwa hakuna mwenye haki ya kutoa wala kukatisha uhai wa mtanzania yeyote yule bila kujali itikadi za kisiasa au sababu ya aina yoyote ile. Ni lazima utawala wa sheria uzingatiwe na siyo watu kujichukulia sheria mkononi.
Kama mtu ana kosa la aina yoyote ile basi afikishwe mahakamani na ushahidi utolewe juu ya makosa ya mhusika na uamuzi ufanyike.haki itendeke na ionekane imetendeka.
Ni lazma tukatae Damu ya mtu yeyote yule kumwagwa.iwe ni ya kijana au mzee au mwanamke au mwanaume au Raia wa kawaida au Albino au vyovyote vile ni lazima tusema HAPANA kumwaga Damu katika ardhi yetu. Tusipande laana katika ardhi yetu na kuleta mikosi na nukusi hapa Nchini.
Mwisho naomba upitie maandiko yako yote ya siku za nyuma uone ulichokuwa ukiandika siku za nyuma na uone kama ulikuwa sahihi na vipi watu wanakuchukuliaje kwa sasa hasa unapotoa andiko kama hili.
Naweka kalamu yangu chini .nitakuja kushusha hoja zingine hapa .ngoja kidogo.