BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,165
Date::5/16/2009
Makamu wa Rais Kenya akiri nchi yake kufaidi Mlima Kilimanjaro
Na Leon Bahati
Mwananchi
Makamu wa Rais Kenya akiri nchi yake kufaidi Mlima Kilimanjaro
Na Leon Bahati
Mwananchi
MAKAMU wa Rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka amekiri kuwa mlima Kilimanjaro umekuwa ukiisaidia nchi yake kukuza sekta ya utalii kutokana na Wakenya wengi kuutumia katika kujitangaza hasa wawapo kwenye nchi za ulaya.
Pamoja na kufaidika huko, alisema kuwa hiyo haifuti ukweli kwamba mlima huo mrefu kuliko yote Afrika, upo Tanzania, ingawa pia huweza kuonekana kutokea Kenya.
Musyoka alisema hayo kwenye hafla fupi ya chakula cha mchana alichoandaliwa na mwenyeji wake, Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Ali Mohamed Shein.
"Wakenya wanapoenda Ulaya wanawaambia wazungu: Njooni Kenya ili muone mlima Kilimanjaro," alisema Musyoka katika ziara hiyo ya kiserikali kwa mwaliko wa Tanzania.
Kauli hiyo ya Musyoka imethibitisha malalamiko ya siku nyingi kuwa Tanzania imeshindwa kuvitangaza vivutio vyake vya utalii, na fursa hiyo kutumiwa na majirani zao wa Kenya na kuufanya ulimwengu udhani mlima huo uko nchini humo.
Lakini, Musyoka hakusita kueleza kuwa jambo hilo limekuwa likizua ubishi kati ya wananchi wa pande zote mbili, lakini akasisitiza kuwa halivunji uhusiano wa karibu ambao umeasisiwa na viongozi wa pande zote.
"Huwa tunabishana hivyo… Lakini ukweli tunajua (Mlima Kilimanjaro) upo Tanzania," aliweka wazi Musyoka ambaye katika hotuba yake alisisitiza mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Kenya na Tanzania ambayo yana faida kwa pande zote.
Kwa mara nyingine, Musyoka aliwahakikishia Watanzania kuwa serikali ya Kenya haina mpango wa kuweka shinikizo la kuhamisha Makao Makuu ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) kutoka Arusha.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo msimamo wa serikali ya Kenya ni kwamba Arusha itaendelea kuwa makao makuu ya EAC hasa ikizingatiwa kuwa imepewa heshima hiyo na viongozi waasisi.
Akizungumzia nafasi ya nchi hizo mbili kufaidika kiuchumi na Jumuia hiyo, Musyoka alisema zote zinajivunia kuwa na idadi kubwa ya watu, hivyo kujihakikishia kuwa na soko kubwa la kibiashara.
Tanzania ina zaidi ya watu milioni 40 na Kenya inaifuatia kwa karibu. Nchi nyingine za Afrika Mashariki ni Uganda, Burundi na Rwanda.
Naye, Dk Shein aliisifu Kenya kwa kuwa nchi ya pili baada ya Uingereza kuwekeza Tanzania na sasa mitaji yao imefikia dola za Marekani 1,284.7 milioni.
Dk Shein aliainisha fedha hizo kuwekezwa kwenye miradi 374 kwenye sekta za kilimo, ujenzi, fedha na katika maendeleo ya rasilimali watu.
Mbali na kuifaidisha Tanzania kutokana na kodi mbalimbali wanazotoa serikalini, Dk Shein alisema kuwa miradi hiyo imetoa ajira kwa Watanzania 41,560.
Alifafanua zaidi kuwa biashara kati ya nchi hizo mbili imekuwa kwa kiwango kikubwa na kwamba imekuzwa zaidi baada ya kuundwa kwa Umoja wa Forodha wa Jumuia ya Afrika Mashariki tangu mwaka 2005.
Alitoa mfano kuwa kiwango cha biashara ya bidhaa katika nchi hizo mbili kimepanda kutoka dola za Marekani 117.7 milioni, mwaka 2005 hadi kufikia dola 214.2 mwaka 2007.
Pamoja na mazingira hayo mazuri, Dk Shein alibainisha kuwa Kenya ndiyo imekuwa ikifaidika zaidi kwenye biashara hizo.
"Biashara kati ya Tanzania na Kenya kila mara imeendelea kuongezeka, ingawa Kenya ndiyo inayofaidika zaidi," alisema Dk Shein.
Kwa kutambua mazingira hayo, Musyoka alisema Watanzania wana nafasi nao kufaidika kwenye ushirikiano huo wa kibiashara kwa kujitokeza kwa wingi kuwekeza nchini Kenya.
Alitoa mwaliko wa Dk Shein kuitembelea Kenya katika siku chache zijazo, akiwa na wafanyabiashara wa Tanzania ambao wako tayari kuwekeza nchini humo.
Alisema kuwa Wakenya watawapokea kwa mikono miwili hasa kwa kuzingatia kuwa Watanzania ni wakarimu na wenye roho ya kiutu.
Katika kuthibitisha hilo alisema kuwa Watanzania hata wanapoenda kununua kitu, hutumia lugha ya kiuungwana ya kutumia neno ‘naomba' jambo ambalo kwa Wakenya hulitumia tu pale mtu anapotaka apewe kitu bila malipo.
Kuhusu amani nchini Kenya, alisema kwa sasa kuna utulivu wa hali ya juu huku akisema kuwa ni matunda yaliyotokana na juhudi za Rais Jakaya Kikwete.
Alikiri kuwa baada ya uchaguzi mkuu uliopita, Wakenya walianza kuuana kwa silaha za jadi, lakini juhudi za siku mbili za Rais Kikwete ziliweza kuwarejesha kwenye amani.
Alisema kwa sasa Kenya kuna amani baada ya kuundwa kwa serikali ya mseto inayoshirikisha pande zilizokuwa zinahasimiana.