Ripoti ya utafiti wa ujumuishi wa kifedha ya Finscope ya mwaka 2023 inaonyesha kuwa asilimia 22.2 ya Watanzania wenye miaka zaidi ya 16 wanatumia huduma za kibenki, idadi hiyo ikiongezeka kutoka asilimia 17 mwaka 2017.
Kutokana na ongezeko la idadi ya watu ambao kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ilionyesha kuwa Watanzania wapo zaidi ya milioni 61, maana yake ni kuwa idadi ya watumiaji wa huduma za kibenki inaongezeka.
Mwamko wa matumizi ya huduma rasmi za kifedha kwa ujumla ni mkubwa, kwani Finscope 2023 inaonyesha kuwa Watanzania watatu kati ya wanne wenye umri wa kuanzia miaka 16 wana uwezo wa kuzifikia huduma za kifedha na kuzitumia.
Hata hivyo, kadiri huduma zinavyozidi kuboreshwa hitaji la elimu ya fedha na mifumo yake linazidi kuongezeka ili kuhakikisha mali na amana za watu zinakuwa salama.
Je, ukiwa miongoni mwa wateja wa benki wa sasa au watarajiwa umewahi kujiuliza nini kitatokea endapo benki hiyo itafilisika?
“Kwa kweli sifahamu, ninachojua ikifilisika inakuwa haina kitu kabisa, lakini nikizipata taarifa hizo mapema nitawahi kwenda benki kuchukua kabla hazijaisha kabisa,” anasema Noel Desdelius, mkazi wa Dar es Salaam.
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa Tangu mwaka 2000 hadi Juni mwaka huu jumla ya benki 9 ziliwekwa kwenye mufilisi kwa sababu mbalimbali, kwa asilimia kubwa sababu ikiwa ni kutokuwa na uwezo wa kujiendesha.
Benki hizo 9 ni Greenland Bank Tanzania Limited (2000), Delphis Bank Tanzania Limited (2003), FBME Bank Limited (2017), Mbinga Community Bank Plc (2017), Njombe Community Bank Limited (2018), Meru Community Bank Limited (2018), Covenant Bank for Women (T) Limited (2018), Kagera Farmers' Cooperative Bank Limited (2018) na Efatha Bank Limited (2018).