Makapuku Forum

Makapuku Forum

Screenshot_20231003_064624_Opera%20Mini.jpg
Screenshot_20231003_064641_Opera%20Mini.jpg
 
Mwalimu Furaha Msule anayefundisha Shule ya Sekondari Kidegembye iliyopo Lupembe Halmashauri ya Wilaya ya Njombe amesimamishwa kazi kwa kosa la kuwachukua Wanafunzi na kuwapeleka kupakia kuni zake kinyume na sheria na kupelekea kupata ajali ya gari wakati wakirudi majira ya saa moja usiku.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Christopher Sanga amethibitisha kusimamishwa kazi kwa Mwalimu Msule na kutoa wito kwa Watumishi kufanya kazi kwa kufuata sheria kanuni na taratibu.

"Ofisi ya Mkurugenzi kwa kushirikiana na Tume ya Walimu imechukua hatua ya kumsimamisha kazi Mwalimu aliyehusika huku utaratibu, sheria na kanuni nyingine zikiendelea"

Sanga amesema October 01,2023 ofisi yake ilipokea taarifa ya kutokea kwa ajali ambapo Mwalimu Furaha aliwachukua Wanafunzi na kwenda kupakia kuni zake lakini kwa sasa Wanafunzi wote 11 wakiwemo 6 waliokuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Kibena wameruhusiwa na kurejea Shuleni.
Screenshot_20231005_145108_Instagram.jpg
 
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), limesema hakuna kiongozi wa Serikali aliyewahi kutumia ndege za shirika hilo kwenda ama ndani au nje ya nchi bila kulipia.

Limesema safari zote za viongozi zinazoshuhudiwa wakitumia ndege za shirika hilo, huwa wanazikodi na kulipia gharama kama ilivyo kwa wateja wengine.

Hayo yanaibuka kipindi ambacho, kumekuwepo na ukosoaji wa matumizi ya ndege hizo kwa viongozi wa Serikali na wastaafu.

Malalamiko dhidi ya matumizi hayo, yamekwenda mbali zaidi hadi kuhusishwa na sababu za kuahirishwa na kucheleweshwa kwa safari za ndege za shirika hilo.

“Safari zinaahirishwa ratiba hazieleweki kwa sababu ndege wanapewa viongozi wanaenda nazo nje bure, badala ya kuziacha zifanye biashara,” amesema Denis Don mkazi wa Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi Digital jana Oktoba 4, 2023 Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi amesema kila inapoonekana ndege ya shirika hilo imetumika na kiongozi kwa safari ama za ndani au nje ya nchi, sio kwamba amepewa bure, bali anaikodi na kulipia gharama.
Screenshot_20231005_145306_Instagram.jpg
 
Wakati baadhi ya wanamichezo hujikuta wanashindwa kutumia umaarufu wao katika kutengeza utajiri pale wanapostaafu, hali ni tofauti kwa Michael Jordan, ambaye utajiri wake wa dola za Marekani bilioni tatu, umemuingiza kwenye orodha (The Forbes 400) ya watu matajiri nchini Marekani.

Kwa mujibu wa TRT Afrika, hii inamfanya Jordan kuwa mwanamichezo wa kwanza kuingia kwenye orodha hiyo, kwani kiwango cha chini cha thamani kinachohitajika kutinga katika orodha hiyo ni pale mhusika amefikia rekodi ya kuwa na utajiri wenye thamani ya dola bilioni 2.9

Licha ya mchezaji huyo wa mpira wa kikapu kujipatia dola milioni 90 katika kipindi kile alichokuwa akicheza, amejizolea mapato zaidi nje ya uwanja kupitia uwekezaji ambao sasa umemfanya awe miongoni mwa Wamarekani matajiri zaidi.

Kwa miongo kadhaa, Jordan amekuwa akipata pato kutoka kwa kila kiatu cha Jordan, shati au soksi zilizouzwa na kampuni ya Nike ambayo ilikuwa inatosha kumletea mapato ya dola milioni 260 katika mapato ya makadirio (kabla ya kodi) katika mwaka uliopita pekee.

Aidha, pato lake kuu pia limetoka klabu ya Charlotte Hornets. Mnamo Agosti, Jordan aliuza hisa nyingi katika timu hiyo ya NBA kwa thamani ya dola bilioni 3, ikiwa ni mara 17 ya thamani yake wakati alipokuwa mmiliki mkuu mnamo 2010.

Mapato hayo ni takriban mara tatu dola milioni 90 alizopata katika enzi alipokuwa akicheza kwa miaka 16.
Screenshot_20231005_145415_Instagram.jpg
 
Kuelekea kusherehekea miaka 100 ya michuano ya kombe la Dunia, Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) limepanga michuano hiyo mwaka 2030 ichezwe katika mabara matatu tofauti kwa wakati mmoja.

Kwa mara ya kwanza michuano hiyo mikubwa na maarufu ya soka duniani ilichezwa mwaka 1930 nchini Uruguay.
Katika mpango huo Fifa imepanga michezo hiyo ifanyike katika bara la Ulaya, Afrika na Amerika Kusini.

Mchanganuo wa mpango huo unaonyesha kwa upande wa Afrika mechi zitachezwa katika nchi ya Morocco huku katika bara la Ulaya zitachezwa katika nchi za Hispania na Ureno na bara la Amerika Kusini mechi zitafanyika Argentina, Paraguay na Uruguay.

Hata hivyo, mpango huo bado unaonekana kutoungwa mkono na baadhi ya wadau wa soka katika mitandao ya kijamii.

"Fifa inaendelea na mzunguko wake wa uharibifu dhidi ya michuano hiyo mikubwa zaidi duniani", kilisema chama cha Football Supporters Europe kwenye X (zamani wa Twitter), kuchukizwa na mfumo huo.

Screenshot_20231005_145521_Instagram.jpg
 
Wananchi wa Kijiji Muwanda katika Bonde la Serenge, Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja wamelalamika kuwapo kikundi cha watu wasiojulikana walichodai kinawacharaza viboko bila sababu na kisha kutokomea kusikojulikana.

Wametoa madai hayo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa huo, Ayoub Mohammed Mahmoud alipofika kusikiliza kero zao.

Vuai Said, mkazi wa kijiji hicho alisema kumeibuka watu ambao hawajulikani wanatoka wapi, lakini wamekuwa wakiwacharaza wananchi viboko na kusababisha taharuki kwenye jamii.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kuna watu huwa wanatuchapa viboko bila sababu za msingi kisha wanatokomea, wakishafanya hivyo wanakimbia kusikojulikana,” alisema mkazi mwingine, Iddi Sultan.

Mkuu wa mkoa huo, Ayoub aliagiza Jeshi la Polisi la Mkoa huo kulifuatilia kwa umakini tatizo la kupigwa kwa wananchi wa kijiji hicho, jambo ambalo alisema linawakosesha amani ya kuishi.
Screenshot_20231005_145625_Instagram.jpg
 
Back
Top Bottom