Wakati baadhi ya wanamichezo hujikuta wanashindwa kutumia umaarufu wao katika kutengeza utajiri pale wanapostaafu, hali ni tofauti kwa Michael Jordan, ambaye utajiri wake wa dola za Marekani bilioni tatu, umemuingiza kwenye orodha (The Forbes 400) ya watu matajiri nchini Marekani.
Kwa mujibu wa TRT Afrika, hii inamfanya Jordan kuwa mwanamichezo wa kwanza kuingia kwenye orodha hiyo, kwani kiwango cha chini cha thamani kinachohitajika kutinga katika orodha hiyo ni pale mhusika amefikia rekodi ya kuwa na utajiri wenye thamani ya dola bilioni 2.9
Licha ya mchezaji huyo wa mpira wa kikapu kujipatia dola milioni 90 katika kipindi kile alichokuwa akicheza, amejizolea mapato zaidi nje ya uwanja kupitia uwekezaji ambao sasa umemfanya awe miongoni mwa Wamarekani matajiri zaidi.
Kwa miongo kadhaa, Jordan amekuwa akipata pato kutoka kwa kila kiatu cha Jordan, shati au soksi zilizouzwa na kampuni ya Nike ambayo ilikuwa inatosha kumletea mapato ya dola milioni 260 katika mapato ya makadirio (kabla ya kodi) katika mwaka uliopita pekee.
Aidha, pato lake kuu pia limetoka klabu ya Charlotte Hornets. Mnamo Agosti, Jordan aliuza hisa nyingi katika timu hiyo ya NBA kwa thamani ya dola bilioni 3, ikiwa ni mara 17 ya thamani yake wakati alipokuwa mmiliki mkuu mnamo 2010.
Mapato hayo ni takriban mara tatu dola milioni 90 alizopata katika enzi alipokuwa akicheza kwa miaka 16.