Wakazi wa Mtaa wa Mbutu Mkwajuni, Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam wamejikuta wakitumia Sh4,000 kufuata sokoni fungu la dagaa la Sh1,000 kutokana na ubovu wa barabara.
Mkazi wa eneo hilo, Frank Ngunda amesema hayo leo Januari 11, 2024 alipokuwa akitoa malalamiko yao kuhusu ubovu wa barabara katika eneo lao.
Ngunda amesema kutokana na ubovu huo wa barabara, gharama za maisha zimeongezeka huku akitolea mfano wanavyolazimika kukodi bodaboda kwa Sh3,000 kwa ajili ya kufuata dagaa wa Sh1,000, hivyo wanajikuta wakitumia Sh4,000.
“Tunaiomba Serikali katika hili, ituangalie kwa jicho la huruma kututengenezea barabara kwa kuwa tumekuwa tukiteseka kwa muda mrefu,” amesema Mbunda.
Kwa upande wa Ipuli Sagula pia mkazi wa mtaa huo, amesema ubovu huo wa barabara umechangiwa pia na malori ya kubeba mchanga yanayopita hapo, hali iliyosababisha waifunge ili yasipite.