Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Félix Tshisekedi amesema yuko tayari kuzungumza na mwenzie wa Rwanda Paul Kagame ili kukomesha machafuko mashariki mwa Kongo.
Kauli imekuja baada ya mkutano wa ana kwa ana wa dakika 180 uliofanyika Luanda, Angola na kuwahusisha Rais Felix Tshisekedi na mwenyeji wake Joao Lourenco ambao hata hivyo hawakutoa kauli yoyote mbele ya Waandishi lakini Waziri wa mambo ya nje wa Angola, Tete Antonio baadae ndio alitoa kauli hii kwamba Tshisekedi amekubali kuzungumza na Paul Kagame, @dw_kiswahili wameripoti.
‘’Matokeo ya mkutano huu ni kwamba Rais Tshisekedi amekubali kimsingi kukutana na Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Angola kama Mpatanishi sasa ina jukumu la kufanya kazi ili kufanikisha mkutano huo” — Tete.
Hatua ya Tshisekedi kukubali mazungumzo na Kagame imekuja miezi mitatu baada ya Kiongozi huyo kuapa kwamba hawezi tena kukutana na jirani yake huyo hadi mbele ya Mungu ambapo Ikulu ya Congo ilitoa masharti na kusema kabla ya mkutano wowote kufanyika kati ya Tshisekedi na Kagame ni lazima kwanza Wanajeshi wa Rwanda waondolewe katika eneo la Congo lakini pia Kundi la M23 lipokonywe silaha.