Wakati Rais Samia Suluhu akiahidi kulitafutia Jeshi la Polisi Sh125 bilioni ili lisimamie vizuri uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na uchaguzi mkuu, wadau wameainisha mambo linalopaswa kufanya na wasiyostahili kuyafanya.
Wadau hao wakiwemo wasomi, wanasiasa na watetezi wa haki za binadamu, wametaka jeshi hilo litimize wajibu wa kikatiba na kisheria wa kulinda raia na mali zao, na lisigeuke kuwa mwamuzi wa ndondi ambaye ana bondia wake mfukoni.
Kulingana na wadau hao, dalili zinaonyesha uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025 utakuwa na ushindani mkubwa kwa vyama na wagombea, hivyo polisi wasiwe chanzo cha vurugu kwa kupendelea upande wowote.
Wakili David Shillatu ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha Mawakili nchini (TLS), kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga alienda mbali na kusema Jeshi la Polisi lina wajibu mkubwa kuhakikisha chaguzi hizo zinakuwa za haki na huru. “Kama alivyosema Rais, polisi wana dhamana ya kuhakikisha huu uchaguzi unapita salama.
Niwasihi sana wafanye majukumu yale tu yanayowahusu na wasiwe na upendeleo katika maamuzi yao,” alisema.
Chaguzi hizo mbili zinaenda kufanyika huku wadau wakiwa na kumbukumbu ya kile kilichotokea katika chaguzi kama hizo zilizopita, huku jimbo la Kawe kukiwa na taarifa za kukamatwa watu walioshukiwa kuwa polisi wakiwa na vibegi vye kura.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus alisema Jeshi la Polisi linatakiwa kubadilika kulingana na mabadiliko ya nyakati, kwa kuwashauri wa mamlaka za juu badala ya kupokea maelekezo.
“Wanasiasa siyo wajuzi wa masuala ya ulinzi, amani na usalama, wao matakwa yao ni kushinda uchaguzi na kuendelea kuwa madarakani, kwa hiyo hivi ni vitu viwili ambavyo mara nyingi huwa vinashindana.
Migogoro mingi Afrika inatokea kwa sababu hiyo,” alisema Dk Kristomus.
View attachment 2741711