Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amesema Ofisi yake imepokea zaidi ya Sh6.5 trilioni ambazo zimepelekwa moja kwa moja kwa Watanzania kutekeleza miradi mbalimbali huku akitangaza kiama kwa wale watakaowachezea fedha za miradi ya Tamisemi.
Waziri Mchengerwa amesema hayo leo Septemba 15, 2023 wakati akitoa salaam za wizara yake mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona Manispaa ya Mtwara.
“Katika eneo la elimu tumepokea zaidi ya Sh2 trilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Elimu nchi nzima na kugharamia elimu msingi bila malipo.
“Kwenye Afya msingi tumepokea zaidi ya Sh1.5 trilioni kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Hospitali za Halmashauri, ukarabati wa Hospitali kongwe, ujenzi wa vituo vya afya, ununuzi wa vifaa tiba, ujenzi wa zahanati pamoja na nyumba za watumishi,” alisema Mchengerwa.
Aidha kwenye eneo la miundombinu, Mchengerwa amesema kuwa zaidi ya Sh3 trilioni zimetumika kujenga, kuendeleza miundombinu ya barabara za vijijini na mijini ambapo katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2023, ujenzi wa daraja la Jangwani na uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi utatekelezwa.
‘Kwa fedha hizo ulizotoa sisi wasaidizi wako hatuna sababu ya kutokufanya kazi, kujituma kwa bidii na weledi wa hali ya juu sisi Kazi yetu kubwa ni kupanga namna bora ya kusimamia na kutekeleza ufanisi wa kazi zilizokusudiwa kukamilishwa kupitia fedha hizo’ alisema Mchengerwa
‘Ninakumbuka siku chache zilizopita wakati unatuapisha ulitusisitiza kufanya kazi kwa bidii, weledi na ubunifu kama ilivyo dira yako nami nilipoanza kazi nilishusha wizara yako kwa wananchi na kuwataka watendaji wote walio chini yangu kujishusha kwa wananchi na kutoka maofisini kwenda kuwahudumia wananchi na kutatua kero zao.
“Yeyote miongoni mwetu atakayewachezea wananchi wako kwa uvivu, uzembe au ubadhirifu wa fedha unazozitoa (Rais Samia Suluhu) kwa ajili ya huduma za wananchi, yule ambaye ni saizi yangu, nitashughlika naye kweli kweli,” amesema Mchengerwa.