Je mhe zito kabwe amevuta kutoka dowans ili awatetee
1. Pepo baya la kisiasa laanza kuinyemelea Chadema,mambo si shwari
Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema ambacho kinadaiwa kuingiliwa na pepo baya la kisiasa.
Na Ramadhan Semtawa
2. UPEPO wa kisiasa katika kambi ya upinzani unavuma vibaya, kufuatia hali ya mambo ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwa tete. Hali tete ya kisiasa ndani ya Chadema imekuja wakati viongozi wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), wakiwa katika hali ya malumbano makali kuelekea kwenye uchaguzi. Nacho chama cha CUF kiliingia kwenye hali ya wasiwasi kisiasa kipindi cha uchaguzi wa viongozi wake hivi karibuni.
3. Wakati upepo huo mbaya ukizidi kuvuma kwa kambi hiyo, Chadema moja ya vyama makini chenye historia ya kutatua mambo yake kimyakimya na kuwa na misingi imara ya uongozi kutoka kwa waasisi akina mzee Edwin Mtei na Bob Nyanga Makani, sasa nacho mambo si shwari. Tathimini ya kichambuzi na duru za kiuchunguzi juu ya mwelekeo wa mambo kwa kuangalia mtiririko wa matukio, mpasuko huo ndani ya Chadema unatokana na suala la ununuzi wa mitambo ya Dowans.
4. Kutofautiana kwa mawazo na misimamo kwa viongozi wa juu ndani ya Chadema kuhusu Dowans, ni jambo ambalo limesababisha mgawanyiko ndani ya chama. Msuguano huo wa fikra na misimamo, ambao umeonekana katika kipindi cha muda wa wiki takriban tatu sasa, ukiwahusisha zaidi Naibu Katibu Mkuu ambaye pia ni mwanasiasa mwenye nguvu, Zitto Kabwe na viongozi wenzake kama akina Dk Wilbrod Slaa, unaonyesha chama hicho sasa kinapita katika wakati mgumu kisiasa.
5. Chadema tayari, kilipita katika wakati mgumu kisiasa baada ya kuondokewa na akina Dk Amaan Kabour, aliporejea Chama Cha Mapinduzi( CCM) na wakati kifo cha Makamu Mwenyekiti marehemu Chacha Wangwe. Wakati wa kuondoka kwa Dk Kabour, Chadema ilipigwa na mawimbi mazito kisiasa kisha ikaweza kuvuka, ndipo mwaka jana ukatokea mvutano mwingine kati ya Wangwe na viongozi wa juu hasa Mwenyekiti Freeman Mbowe katika kutaka kuchukua nafasi ya Mwenyekiti taifa.
6. Hata hivyo, joto hilo la kisiasa la sasa ambalo linatokana na ununuzi wa mitambo ya Dowans ambao umekuja katika kipindi kigumu cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na mkuu hapo mwakani, unaweza kuisumbua Chadema. Tayari, nyufa ndani ya Chadema zinazotokana na ununuzi wa mitambo ya Dowans, zimeanza kujitokeza kufuatia viongozi hao kutoa kauli zinazoonyesha misimamo tofauti kuhusu ununuzi wa mitambo ya Dowans.
7. Wakati Zitto ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, akisimamia kidete ununuzi wa mitambo hiyo, viongozi wengine wa Chadema wakiongozwa na Dk Slaa pamoja na Mwenyekiti Mbowe, wanapinga.
Katika kudhihirisha ufa huo, wakati Zitto alimtaka mbunge wa Kyela Dk Harrison Mwakyembe, atangaze maslahi yake katika Kampuni ya Power Pool East Africa, Dk Slaa alinukuliwa na gazeti la Mwanachi Jumapili akisema hakupaswa kutangaza maslahi.
8. Dk Slaa katika kauli hiyo, anaonekana kupingana na msaidizi wake wa karibu ambaye ni Zitto katika msimamo kuanzia Dowans na hata uanahisa wa Dk Mwakyembe katika Power Pool. Msuguano huo unaangaliwa kama moja ya chanzo, kinachoweza kuleta mpasuko ndani ya Chadema.
9. Tayari, msimamo huo wa Zitto kuhusu ununuzi wa mitambo ya Dowans na kurusha makombora kwa Dk Mwakyembe, umekuwa ukimfanya ahusishwe na harufu ya ushawishi wa nguvu ya fedha za watuhumiwa wa ufisadi. Hivyo, kauli za vigogo hao wa Chadema kupinga ununuzi wa mitambo ya Dowans, ni sawa na msimamo wa chama kukana kauli ya Naibu Katibu Mkuu wake.
10. Kauli hiyo ya Mbowe ambaye ni Mwenyekiti, ilikuja mahususi kujibu swali kuhusu vipi Zitto aunge mkono ununuzi wa mitambo ya Dowans na msimamo wa chama ni upi. Hata hivyo, kauli hiyo bado inaonekana kushindwa kuondoa wingu zito ndani ya Chadema, kwani Mbowe alimtaka Dk Mwakyembe ahamie chama hicho kwa maelezo kwamba hawezi kupambana na ufisadi ndani ya CCM.
11. Mbowe katika kauli hiyo, alisema mfumo ambao Dk Mwakyembe anautumikia hauwezi kupambana na ufisadi, kauli ambayo ilikuwa ni pigo jingine kwa Zitto kwani tayari amekuwa katika malumbano ya kisiasa na mbunge huyo wa Kyela hadi kurushiana makombora akimtaka ajiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Madini.
12. Pia, tangu mjadala wa Dowans, Zitto hajawahi kushiriki vema katika mikutano ya operesheni Sangara mkoani Kilimanjaro, huku mara nyingi akiwa Dar es Salaam.